Thursday, February 22, 2018

MAKAMU WA RAIS AWATAKA WANANCHI KUCHANGIA UJENZI WA MIUNDOMBINU YA ELIMU

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan amewataka wananchi mkoani Simiyu kuchangia ujenzi wa miundombinu ya elimu ili kuunga mkono jitihada za Serikali katika maendeleo ya Sekta ya Elimu.

Mhe.Makamu wa Rais ameyasema hayo wakati  akizungumza na Wananchi wa Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu kwenye  Mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Nguzo Nane wakati wa ziara yake mkoani humo.

Amesema Serikali imeamua kutoa elimu bila malipo na kuwapunguzia wazazi mzigo wa kulipia gharama za karo na michango mbalimbali ya uendeshaji wa shule lakini suala la kuchangia ujenzi wa miundombinu ya elimu wananchi wanapaswa kuunga kuchangia ili kuunga mkono juhudi hizo.

“ Tunapeleka fedha katika shule zote za Msingi na Sekondari ili wanafunzi waweze kusoma vizuri lakini kwenye suala la ujenzi wa matundu ya vyoo, madarasa, maabara pamoja na kwamba Serikali ina wajibu wa kufanya hayo na ninyi wananchi mnao wajibu wa kusaidia kufanya hayo” alisema Mhe. Makamu wa Rais.

Wakati huo huo Mhe.Makamu wa Rais ameipongeza Wilaya ya Maswa kwa kuongeza ufaulu kutoka asilimia 45 hadi asilimia 75 kwa mwaka 2017 na akakemea vikali tabia ya wanaume wanaoua ndoto za watoto wa kike kwa kuwapa mimba , ambapo amesema jicho la Serikali liko kwa watoto wa kike na itawachukulia hatua kali wote watakaobainika kufanya hivyo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dkt.Seif Shekalaghe amesema watoto wa kike 28 wameripotiwa kuwa na mimba katika kipindi cha mwezi Desemba 2017 hadi sasa na Serikali ya Wilaya kupitia Operesheni tokomeza Mimba imefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 15 na kati ya hao wawili wamehukumiwa miaka 30 jela kila mmoja.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi Mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki ambaye pia ni Naibu Waziri wa Madini , Mhe.Stanslaus Nyogo amewashukuru viongozi wa Wilaya kuleta mafanikio katika elimu ikiwa ni pamoja na ongezeko la ufaulu.

Katika hatua nyingine Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan mara baada ya kufungua Jengo la Upasuaji la Upasuaji Hospitali ya Wilaya ya Maswa ambalo limepewa jina lake “SAMIA SULUHU HASSAN OPERATING THEATER” amewataka Watumishi wa Afya kufanya kazi kwa bidii

Aidha, amesema Serikali itahakikisha inaboresha huduma za afya ikiwa ni pamoja na ujenzi wa vituo vya Afya katika kila kata na kuboresha huduma za Afya ya Mama na Mtoto ili kupunguza Vifo vya mama na mtoto.

Naye Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe.Josephat Kandege amesema Serikali imekusudia kujenga vituo vya Afya 286 kufikia  mwisho mwa mwaka 2017/2018  lengo likiwa ni kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa kupunguza mrundikano wa wagonjwa katika Hospitali za Wilaya.
Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi, Mhe.Mashimba Ndaki amesema pamoja na kuendelea kuboresha sekta ya Afya kwa kujenga miundombinu, ni vema Serikali ikaajiri watumishi wa Idara ya Afya kukabiliana na upungufu uliopo.

Mhe.Makamu wa Rais amemaliza Ziara yake Wilayani Maswa ambapo amefungua Jengo la Upasuaji la Upasuaji Hospitali ya Wilaya ya Maswa ambalo limepewa jina lake “SAMIA SULUHU HASSAN OPERATING THEATER” na kuzungumza na wananchi katika Uwanja wa Nguzo Nane.
MWISHO

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan akimwagilia mti wa mwembe alioupanda mara baada ya kufungua Jengo la Upasuaji la Hospitali ya Wilaya ya Maswa ambalo limepewa jina lake “SAMIA SULUHU HASSAN OPERATING THEATER” wakati wa ziara yake Mkoani Simiyu.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Maswa kwenye mkutano wa Hadhara uliofanyika katika uwanja wa Nguzo nane Mjini Maswa, wakati wa ziara yake wilayani humo.
Mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki, Mhe.Stanslaus Nyogo ambaye pia ni Naibu Waziri wa Madini akitoa maelezo kwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan wakati alipokuwa akikagua Jengo la Upasuaji la Hospitali ya Wilaya ya Maswa ambalo limepewa jina lake “SAMIA SULUHU HASSAN OPERATING THEATER” mara baada ya kulifungua wilayani humo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan akikagua Hospitali ya Wilaya ya Maswa mara baada ya kufungua Jengo la Upasuaji la Hospitali ya Wilaya ya Maswa ambalo limepewa jina lake “SAMIA SULUHU HASSAN OPERATING THEATER” wakati wa ziara yake Mkoani Simiyu, (kulia mwenye miwani) Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dkt.Seif Shekalaghe akimuongoza.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan(katikati) akia katika picha ya pamoja na viongozi wa Chama na Serikali wa Wilaya ya maswa na Mkoa wa Simiyu mara baada ya kufungua Jengo la Upasuaji la Hospitali ya Wilaya ya Maswa ambalo limepewa jina lake “SAMIA SULUHU HASSAN OPERATING THEATER” wakati wa ziara yake wilayani Maswa.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan akiagana na wananchi wa Wilaya ya Maswa mara baada ya mkutano wa Hadhara uliofanyika Uwanja wa Nguzo Nane mjini Maswa.
Mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki ambaye pia ni Naibu Waziri wa Madini , Mhe.Stanslaus Nyogo, akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Maswa kwenye mkutano wa Hadhara uliofanyika katika uwanja wa Nguzo nane Mjini Maswa, wakati wa ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan wilayani humo
Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi, Mhe.Mashimba Ndaki, akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Maswa kwenye mkutano wa Hadhara uliofanyika katika uwanja wa Nguzo nane Mjini Maswa, wakati wa ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan wilayani humo.

0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!