Saturday, February 17, 2018

KAIMU MKURUGENZI MAMLAKA YA VIWANJA VYA NDEGE AIOMBA SERIKALI KUTOA KIPAUMBELE UJENZI WA UWANJA WA NDEGE SIMIYU

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka wa Viwanja vya Ndege nchini (TAA),  Richard Mayongela ameiomba serikali kutoa kiupaumbele cha ujenzi wa Viwanja vya Ndege kwa mikoa ya Simiyu na Lindi katika bajeti ya mwaka 2018/2019 ili kuongeza fursa za uwekezaji na utalii.

Mayongele ametoa ombi hilo leo katika kijiji cha IGEGU kata ya Sapiwi wilayani  BARIADI katika eneo linalotarajiwa kujengwa Uwanja wa Ndege wa Mkoa wa Simiyu, wakati wa ziara ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano  Prof. Makame Mbarawa mkoani Simiyu.

Amesema hatua za awali za maandalizi ya ujenzi wa Uwanja huo zimekamilika ambapo usanifu na upembuzi yakinifu vimeshafanyika na makadirio ya awali yanaonesha kuwa mradi huo utagharimu takribani shilingi bilioni 95.56 na utakapokamilika utawezesha ndege zenye uwezo wa kubeba  kuanzia watu 75 na kuendelea kutua.


Ameongeza kuwa Ujenzi wa Uwanja huo utakapokamilika utakuwa ni chachu ya maendeleo kwa Mkoa huo katika nyanja za uchumi na utalii  na utachangia kuufungua mkoa wa Simiyu kiuchumi pamoja na mikoa mingine ya kanda ya Ziwa.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema kukamilika kwa Uwanja huo itakuwa ni faida kubwa kwa kuwa utakuwa  Uwanja pekee wa Serikali hapa nchini ambao Watalii watautumia kuifikia Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa urahisi kuliko viwanja vingine.

“Tunajenga Uwanja ambao kimkakati unakaa mpakani mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, karibu na uwanja huu kuna hii barabara ya inayotunganisha na Mkoa wa Shinyanga kupitia Malampaka ambako kutajengwa Reli ya Kisasa, hapa jirani  tuna eneo ambalo tutajenga Kiwanda cha Vifaa tiba, mbele yeke tunaanzisha Kanda ya Nanenane ...tunaamini kukamilika kwa mradi huu kutakuwa na faida sana  kwa Serikali na wananchi”  alisema Mtaka

Waziri wa Ujenzi , Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amewahikikishia viongozi wa Mkoa wa Simiyu juu ya ujenzi wa uwanja wa ndege Simiyu, lakini akatoa angalizo kuwa wakati kufanya tathmini ya fidia ya eneo la ujenzi,  gharama ya fidia  isiwe kubwa vinginevyo Uwanja huo hautaweza kujengwa.

“Wale watakaokuja kufanya tathmini wahakikishe gharama ya fidia inakuwa chini sana na ifanywe kwa mujibu wa sheria, hatutaweza kuwadhulumu watu lakini tuhakikishe tathmini inafanyika kwa mujibu wa sheria” alisisitiza Waziri Mbarawa.

Akizungumza kwa niaba ya Wananchi wa Kijiji cha Igegu mahali unapotarajiwa kujengwa uwanja huo, Diwani wa Kata ya Sapiwi, Mhe.Kibuga Gamalieli amesema wananchi wanasubiria kwa shauku kubwa kuona Uwanja huo unakamilika na akamuhakikishia  Waziri Mbarawa kuwa wananchi hawatadai fidia kubwa katika eneo hilo kwa kuwa wanataka maendeleo.

Waziri Mbarawa yuko Mkoani Simiyu kwa ziara ya siku mbili ambapo leo pamoja na kutembelea eneo la ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Mkoa Simiyu amezungumza na watumishi wa Taasisi zote zilizo chini ya Wizara yake, amekagua Ujenzi wa Hospitali ya Mkoa na Nyumba za Viongozi wa Mkoa  na kutembelea Kambi ya Mkandarasi wa Mradi wa Ujenzi wa Barabara ya Bariadi-Maswa kata ya Luguru wilayani Itilima
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Nchini,  Richard Mayongele (kulia) akitoa maelezo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa(mwenye kofia)  kuhusu Uwanja wa Ndege wa mkoa wa Simiyu unaotarajiwa kujengwa Kijiji cha Igegu wilayani Bariadi wakati wa ziara ya Waziri huyo leo Mkoani Simiyu.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka (kushoto) akieleza juu ya umuhimu wa Uwanja wa Ndege wa mkoa unaotarajiwa kujengwa Kijiji cha Igegu wilayani Bariadi wakati wa ziara ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,Mhe. Prof. Makame Mbarawa leo Mkoani humo.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,Mhe. Prof. Makame Mbarawa  akizungumza na Viongozi wa Mkoa wa Simiyu wakati alipotembelea eneo la Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Mkoa wa Simiyu, unaotarajiwa kujengwa Kijiji cha Igegu wilayani Bariadi wakati wa ziara yake leo Mkoani humo.
Mkurugenzi Mtendaji wa  Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Ndg.Abdallah Malela akiwasilisha taarifa ya eneo la Igegu wilayani Bariadi linalotarajiwa kujengwa Uwanja wa Ndege Mkoani Simiyu  kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,Mhe. Prof. Makame Mbarawa alipokuwa kwenye ziara mkoani humo leo.

Diwani wa Kata ya Sapiwi wilayani Bariadi, Mhe.Kibuga Gamalieli( kulia) akimweleza jambo Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,Mhe. Prof. Makame Mbarawa(kushoto) alipotembelea eneo linalotarajiwa kujengwa Uwanja wa Ndege Mkoani Simiyu, wakati alipokuwa katika ziara Mkoani humo leo .
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,Mhe. Prof. Makame Mbarawa(mwenye kofia) akisalimiana na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji  wa Bariadi, Ndg.Melkizedeck Humbe mara baada ya kuwasili wilayani Bariadi kwa ajili ya kuanza ziara ya siku mbili mkoani Simiyu.

0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!