Wednesday, November 29, 2017

BILIONI 375.4 ZATOLEWA KUTEKELEZA MRADI WA KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TABIANCHI NA KUTATUA TATIZO LA MAJI SIMIYU

Serikali ya Tanzania  kwa kushirikiana na Serikali ya  Ujerumani, Mfuko wa Mabadiliko tabia nchi (CGF) na wananchi, imetenga kiasi cha shilingi bilioni 375.4  kutekeleza Mradi wa kukabiliana na changamoto  zinazotokana na mabadiliko ya tabia nchi mkoani SIMIYU kwa awamu ya kwanza, ambao utakuwa suluhisho la kudumu la tatizo la maji mkoani humo

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Isack Kamwelwe wakati akifungua kikao cha wadau wa mabadiliko ya tabia nchi kilichofanyika Mjini Bariadi Mkoani Simiyu.

Waziri Kamwelwe amesema moja ya shughuli muhimu na kubwa katika utekelezaji wa Mradi wa kukabiliana na changamoto  zinazotokana na mabadiliko ya tabia nchi,  ni ufikishaji wa huduma ya Maji ya Ziwa Victoria katika Mji wa Bariadi , Busega na Itilima kwa awamu ya kwanza na baadaye katika Wilaya ya Meatu na Maswa.

Ameongeza kuwa upatikanaji wa maji katika Mkoa wa Simiyu uko chini ikilinganishwa na wastani wa Kitaifa na kwa kutambua hali hii,  Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ilibuni mradi huu,  ili kupata suluhisho la kudumu  la tatizo la maji kwa wananchi na mifugo ambayo ni moja ya shughuli za kiuchumi za wananchi wa Mkoa wa Simiyu.

Aidha, Waziri Kamwelwe amesema lengo la mradi huu ni kuboresha Afya na kuongeza uzalishaji  ili kuinua hali ya maisha kwa wananchi walioathirika na mabadiliko ya tabia nchi, ambapo amebainisha kuwa katika kufikia lengo shughuli mbalimbali zitatekelezwa katika nyanja za maji safi na usafi wa mazingira, kilimo endelevu na ufugaji.

Waziri pia amebainisha kuwa kutakuwa na ujenzi wa mabwawa ya kilimo cha umwagiliaji endelevu na maji ya mifugo, ujenzi wa mabwawa ya kutibu maji taka pamoja na vyoo vya mfano katika Shule na Vituo vya Afya.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka ameishukuru Serikali kwa kutekeleza mradi huo ambao utawasaidia wananchi wa mkoa huo na utakuwa chachu katika Ujenzi wa Viwanda mkoani humo kwa kuwezesha upatikanaji wa maji ya uhakika.

“Wananchi wa Mkoa wa Simiyu wote wanausubiri sana mradi huu wa maji ya Ziwa Victoria; pia Mkoa wetu unaenda kwenye uwekezaji wa viwanda vikubwa na changamoto tuliyonayo ni suala la upatikanaji wa maji ya uhakika, utekelezaji wa mradi huu utatusaidia sana katika viwanda” amesema Mtaka.

Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji Profesa Kitila Mkumbo amesema kuwa Simiyu ni Miongoni mwa Mikoa yenye kiwango cha chini cha upatikanaji wa huduma ya maji ambayo Serikali imetoa kiupaumbele cha kuipa fedha kutoka katika Fedha za Mfuko wa Maji ili kutekeleza miradi ya maji itakayoibuliwa na kuwasilisha maandiko yake wizarani.

Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Ndg.Jumanne Sagini amewahimiza Wataalam wa Halmashauri kwa kushirikiana na Mkoa kuandaa maandiko ya kuibua miradi ya Maji itakayowasilishwa wizara ya maji,  kwa lengo la kuomba fedha za  kutekeleza miradi hiyo ili kuongeza na kuboresha upatikanaji wa huduma za maji mkoani humo.

Mradi wa kukabiliana na changamoto  zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi Mkoani SIMIYU ambao zabuni yake imepangwa kutangazwa Januari 2018; utatekelezwa kwa awamu mbili awamu ya kwanza utaanza na Mji wa Bariadi, Busega na Itilima pamoja na vijiji 278 vilivyopo pembezoni mwa bomba kuu umbali wa Kilomita 12 kila upande,  baadaye maeneo mengine ya Wilaya za Maswa na Meatu.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi .Isack Kamwelwe  akifungua kikao cha Wadau wa Mradi wa  kukabiliana na changamoto zitokanazo na  Mabadiliko ya Tabianchi (hawapo pichani) unaotekelezwa katika Mkoa wa Simiyu kilichofanyika Mjini Bariadi kwa lengo la kujadili mikakati ya utekelezaji wa mradi huo

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na Wadau wa Mradi wa  kukabiliana na changamoto zitokanazo  na Mabadiliko ya Tabianchi (hawapo pichani) unaotekelezwa Mkoani humo, katika kikao kilichofanyika Mjini Bariadi kwa lengo la kujadili mikakati ya utekelezaji wa mradi huo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Profesa Kitila Mkumbo akizungumza na  Wadau wa Mradi wa  kukabiliana na changamoto zitokanazo na Mabadiliko ya Tabianchi (hawapo pichani) unaotekelezwa Mkoani Simiyu  kwenye kikao kilichofanyika Mjini Bariadi kwa lengo la kujadili mikakati ya utekelezaji wa mradi huo.
Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Jumanne Sagini akichangia hoja katika kikao cha Wadau wa Mradi wa  kukabiliana na changamoto zitokanazo na Mabadiliko ya Tabianchi, unaotekelezwa Mkoani humo kilichofanyika Mjini Bariadi kwa lengo la kujadili mikakati ya utekelezaji wa mradi huo.
Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Mhe.Dkt.Joseph Chilongani akichangia hoja katika kikao cha Wadau wa Mradi wa  kukabiliana na changamoto zitokanazo na Mabadiliko ya Tabianchi , unaotekelezwa Mkoani Simiyu,  kilichofanyika Mjini Bariadi kwa lengo la kujadili mikakati ya utekelezaji wa mradi huo.
Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi Mhe.Mashimba Ndaki akichangia hoja katika kikao cha Wadau wa Mradi wa  kukabiliana na changamoto zitokanazo na Mabadiliko ya Tabianchi , unaotekelezwa Mkoani humo kilichofanyika Mjini Bariadi kwa lengo la kujadili mikakati ya utekelezaji wa mradi huo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Bariadi, Mhe.Robert Lweyo akichangia hoja katika kikao cha Wadau wa Mradi wa  kukabiliana na changamoto zitokanazo na Mabadiliko ya Tabianchi ( baadhi hawapo pichani) unaotekelezwa Mkoani Simiyu kilichofanyika Mjini hapo kwa lengo la kujadili mikakati ya utekelezaji wa mradi huo.
PICHA H:-Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Itilima, Ndg.Mariano Mwanyigu akichangia hoja katika kikao cha Wadau wa Mradi wa  kukabiliana na changamoto  zitokanazo na Mabadiliko ya Tabianchi (baadhi hawapo pichani) unaotekelezwa Mkoani Simiyu kilichofanyika Mjini Bariadi kwa lengo la kujadili mikakati ya utekelezaji wa mradi huo.
Mwakilishi wa Tume ya Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi, Bi.Pili Msati akichangia hoja katika kikao cha Wadau wa Mradi wa  kukabiliana na changamoto zitokanazo na Mabadiliko ya Tabianchi (hawapo pichani) unaotekelezwa Mkoani Simiyu kilichofanyika Mjini Bariadi kwa lengo la kujadili mikakati ya utekelezaji wa mradi huo.
Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Simiyu, Mhe.Jeremia Shigala akichangia hoja katika kikao cha Wadau wa Mradi wa  kukabiliana na changamoto zitokanazo na Mabadiliko ya Tabianchi unaotekelezwa Mkoani humo kilichofanyika Mjini Bariadi kwa lengo la kujadili mikakati ya utekelezaji wa mradi huo.
Baadhi ya wadau wa Mradi wa kukabiliana na changamoto zitokanazo na Mabadiliko ya Tabianchi  unaotekelezwa Mkoani Simiyu akifuatilia masuala mbalimbali yalikuwa yakijadiliwa katika kikao kilichofanyika mjini Bariadi kwa lengo la kujadili mikakati ya utekelezaji wa mradi huo
Baadhi ya wadau wa Mradi wa kukabiliana na changamoto zitokanazo na Mabadiliko ya Tabianchi  unaotekelezwa Mkoani Simiyu akifuatilia masuala mbalimbali yalikuwa yakijadiliwa katika kikao kilichofanyika mjini Bariadi kwa lengo la kujadili mikakati ya utekelezaji wa mradi huo.
Mkuu wa Wilaya ya Busega, Mhe.Tano Mwera akichangia hoja katika kikao cha Wadau wa Mradi wa  kukabiliana na changamoto zitokanazo na Mabadiliko ya Tabianchi unaotekelezwa Mkoani humo kilichofanyika Mjini Bariadi kwa lengo la kujadili mikakati ya utekelezaji wa mradi huo.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe(katikati) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Mkoa wa Simiyu na wadau wa Mradi wa kukabiliana na changamoto zitokanazo na Mabadiliko ya Tabianchi  unaotekelezwa Mkoani humo mara baada ya ufunguzi wa kikao cha wadau hao kilichofanyika Mjini Bariadi.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe(katikati) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Mkoa wa Simiyu na wadau wa Mradi wa kukabiliana na changamoto zitokanazo na Mabadiliko ya Tabianchi  unaotekelezwa Mkoani humo mara baada ya ufunguzi wa kikao cha wadau hao kilichofanyika Mjini Bariadi.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe(kulia) na KATIBU Mkuu wa Wizara hiyo, Profesa Kitila Mkumbo wakisaini vitabu vya wageni katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,  baada ya kuwasili mkoani hapo kwa ajili ya kushiriki  kikao cha Wadau wa Mradi wa  kukabiliana na changamoto zitokanazo na  Mabadiliko ya Tabianchi  unaotekelezwa Mkoani humo, kilichofanyika Mjini Bariadi kwa lengo la kujadili mikakati ya utekelezaji wa mradi huo.

Tuesday, November 28, 2017

RC MTAKA AWAKABIDHI PIKIPIKI NA GARI MAAFISA UGANI ITILIMA

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka amekabidhi pikipiki za maafisa Ugani na Gari la Idara ya Kilimo  wilayani Itilima na kusisitiza kuwa vyombo hivyo vitumike kwa ajili ya kuwafikia wananchi ili kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao hususani zao la pamba.

Vyombo hivyo ambavyo awali vilikuwa vimeegeshwa vimefanyiwa matengenezo kwa gharama za Halmashauri ya Wilaya ya Itilima ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka, aliyoyatoa wakati wa ziara yake  aliyofanya katika Halmashauri zote Mkoani humo kwa lengo la kuhimiza kilimo.

Mtaka amesema zao la pamba linachangia mapato ya Halmashauri kwa kiasi kikubwa Mkoani humo  hivyo Wakurugenzi wanapaswa kuhakikisha vyombo vya usafiri vinafanya kazi muda wote wa msimu ili wataalam waweze kuwafikia wakulima(wananchi) na kuwasaidia kuzalisha kwa tija.

“ Mwaka 2016/2017 Itilima ilipata milioni 500 kutokana na pamba lakini Idara ya Kilimo iliyosababisha Pamba kuleta fedha hizo  haikutengewa fedha kwenye bajeti, haikuwa na gari wala pikipiki” amesema Mtaka.

“ Wakati wa kilimo hakuna  magari kwa ajili ya kuwafikia wakulima, wakati wa kukusanya ushuru magari yote yanakuwa mazima na yanawekwa mafuta ili kufuatilia ushuru, maelekezo yangu kwa Halmashauri zote ni kwamba wakati wote wa msimu wananchi kuanzia wanapoandaa mashamba ni lazima pikipiki na magari yafanye kazi kwenye Idara ya Kilimo ” amesititiza  Mtaka.

Wakipokea pikipiki na gari la Idara Maafisa Ugani hao wameahidi kufanya kazi kwa bidii na kuhakikisha wanawafikia wakulima wote walio katika maeneo yao, ili kupitia utaalamu wao waweze kuwasaidia kuongeza uzalishaji, ambapo wamekusudia kuongeza uzalishaji wa pamba kwa mwaka 2017/2018 kutoka kilo 650 hadi 1200 kwa ekari.

Mkoa wa SIMIYU ni mkoa unaozalisha pamba kwa wingi ambapo  unazalishaji asilimia 60 ya pamba yote hapa nchini
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na Maafisa Ugani na Viongozi wa Wilaya ya Itilima (baadhi hawapo pichani) kabla ya kukabidhi pikipiki za Maafisa Ugani na Gari la Idara ya Kilimo , vyote vimetengenezwa na Halmashauri ya Itilima kutekeleza agizo alilotoa wilayni humo wakati wa ziara yake ya kuhamasisha Kilimo. MADC, WAKURUGENZI MKOANI SIMIYU WAAGIZWA KUUNDA TIMU ILI KUJIRIDHISHA JUU YA WANAFUNZI WANAODAIWA KUWA MAMLUKI

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka amewaagiza Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri Mkoani humo kuunda timu zitakazopitia na kujiridhisha juu ya  majina ya wanafunzi 633 waliotajwa kuwa Mamluki na kuondolewa shuleni kwa kukosa sifa za kusoma shule za sekondari za Serikali kutokana na sababu mbalimbali.

Agizo hilo amelitoa jana katika Shule ya Sekondari Nkoma wilayani ITILIMA kwenye  kikao chake na viongozi, watendaji wa Serikali na wazazi wa baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo walioondolewa katika mfumo wa Serikali kutokana na kutumia majina yasiyo yao, kukosa fomu  za TSM 9 , kukosa vibali vya kukariri/kurudia kidato na vibali vya uhamisho.

Mtaka amesema timu hizo zitakazoundwa kwa kila Wilaya zifuatilie na kujiridhisha kwa kupitia majina yote  pamoja na sababu za wanafunzi hao kuitwa Mamluki na kuondolewa katika mfumo wa Serikali zilizoanishwa, ambapo amebainisha kuwa watendaji wa Idara ya Elimu watakaobainika kusababisha kwa uzembe wanafunzi hao kuondolewa shuleni watachukuliwa hatua za kinidhamu.

Ameongeza kuwa Wakuu wa Wilaya kwa kushirikiana na Wakurugenzi wa Halmashauri na Maafisa Elimu Sekondari waitishe vikao na wanafunzi hao na wazazi wao, ili wazungumze na kuwaeleza hatua zitakazochukuliwa baada ya kujiridhisha, baadaye taarifa ya kila wilaya iwasilishwe mkoani.

“Kufikia Ijumaa wakuu wote wa Wilaya na Maafisa Elimu wawe wamekutana na wanafunzi waliopata matatizo hayo,wazazi wao na watoto wote waitwe kutoa ushuhuda wa nini kimesababisha wao kuitwa mamluki na kurudishwa nyumbani,  wakishajiridhisha watuletee hiyo taarifa na sisi Mkoa tutaipitia na kutoa maelekezo; tunaweza kusema wanafunzi 633 ni mamluki kumbe umamluki wa baadhi ya wanafunzi umesababishwa na  uzembe wa Watendaji wetu.” alisisitiza Mtaka.

Aidha baada ya kusikiliza hoja za baadhi ya  wanafunzi walioondolewa katika mfumo wa shule za Serikali pamoja na  wazazi wao shuleni Nkoma na kubaini kuwa baadhi ya sababu zilizopelekea wanafunzi hao kuondolewa zimechangiwa na uzembe wa baadhi ya Watendaji wa Idara ya Elimu ngazi ya Wilaya na Wakuu wa Shule Mtaka ameagiza wanafunzi hao warudishwe shuleni mara moja.

“Kuna wanafunzi hapa Nkoma tumewasikiliza kesi zao wapo ambao walipaswa kurudia darasa , taratibu za upatikanaji wa kibali cha kurudia darasa kama wanafunzi pamoja na wazazi wamefanya, lakini inaonekana kuna uzembe kati ya Wakuu wa Shule na Idara ya Elimu Wilaya, maagizo ya Serikali ya Mkoa vibali vya wanafunzi hao kufikia tarehe 29/11/2017 viwe vimetolewa na warudishwe shuleni” amesema Mtaka.

Sanjari na hilo Mtaka ameagiza wanafunzi wote wanaosoma shule za Sekondari kwa kutumia majina ya watu wengine waondolewe katika mfumo wa shule za Sekondari za Serikali na akatoa wito kwa wazazi wao kuwapeleka katika shule binafsi au katika utaratibu wa utahiniwa binafsi (QT) ili wafanye mitihani kama watahiniwa binafsi (Private Candidates).

Baadhi ya wanafunzi waliondolewa katika mfumo wa Shule za Serikali katika Shule ya Sekondari Nkoma Wilayani Itilima kwa sababu mbalimbali ikiwemo ya kutumia majina ya watu wengine wamesema wako tayari kuendelea na masomo ikiwa watapata nafasi katika shule binafsi, ambapo wazazi wao pia wamesema wako tayari kuwapeleka watoto wao katika shule binafsi ili kuwasaidia wafikie malengo yao.

“ Nilipata taarifa kuwa mwanangu ameondolewa shuleni kwa sababu anatumia jina la mtu mwingine na nimeshaanza kutafuta nafasi kwenye shule za binafsi ili aendelee na masomo kwa sababu alikuwa anafanya vizuri darasani, kwa mfano muhula uliopita aliongoza” alisema Sumuni Daudi mmoja wa wazazi walioshiriki kikao na Mkuu wa Mkoa.

Naye Mbunge wa Jimbo la Itilima Njalu Silanga ameomba kuwepo na darasa maalum kwa wanafunzi watakaobainika kuwa siyo halali waandaliwe utaratibu wa  kufundishwa na baadaye wafanye mitihani  kama watahiniwa wa kujitegemea ili waweze kutimiza ndoto zao.. 
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na viongozi wa Serikali, wanafunzi walioondolewa shuleni kutokana na sababu mbalimbali pamoja na wazazi wao(hawapo pichani) katika Shule ya Sekondari Nkoma Wilayani Itilima. 
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Nkoma Wilayani Itilima pamoja na wazazi wao wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka (hayupo pichani)  katika kikao maalum kilichofanyika shuleni hapo jana.
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Nkoma Wilayani Itilima pamoja na wazazi wao wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka (hayupo pichani)  katika kikao maalum kilichofanyika shuleni hapo jana.
Mbunge wa Jimbo la Itilima Mhe.Njalu Silanga akichangia hoja katika kikao kilichoitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu kwa lengo la kuzungumza na viongozi wa Serikali, wanafunzi walioondolewa shuleni kutokana na sababu mbalimbali pamoja na wazazi wao wilayani Itilima.
Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Mhe.Benson Kilangi akifuatilia kwa makini hoja mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa katika kikao kilichoitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka kwa lengo la kuzungumza na viongozi wa Serikali , wanafunzi walioondolewa shuleni kutokana na sababu mbalimbali pamoja na wazazi wao wilayani humo.
Mmoja wa wanafunzi walioondolewa shuleni kutokana na kukosa sifa za kusoma katika shule za Sekondari za Serikali akizungumza mbele ya Mkuu wa Mkoa na viongozi wengine wa Serikali juu sababu ya zilizopelekea kuondolewa kwake shuleni.
Mmoja wa wazazi wa wanafunzi walioondolewa shuleni kutokana na kukosa sifa za kusoma katika shule za Sekondari za Serikali akizungumza mbele ya Mkuu wa Mkoa na viongozi wengine wa Serikali katika kikao kilichofanyika Shule ya Sekondari Nkoma wilayani Itilima kujadili suala hilo.

Thursday, November 2, 2017

WAKULIMA MKOANI SIMIYU WATAKIWA KULIMA MAZAO YA BIASHARA

Mkuu wa mkoa wa Simiyu,Anthony Mtaka amewasisitiza wakulima Mkoani humo kulima mazao ya biashara yenye  tija hasa zao la pamba kwa kuzingatia Mkoa huo upo katika mchakato wa utekelezaji wa ujenzi wa kiwanda cha bidhaa za afya zitokanazo na  zao la pamba.

Msisitizo huo ameutoa jana wilayani Maswa katika ziara yake ya kuhamasisha kilimo kuelekea msimu wa kilimo na kueleza kuwa wakulima wanapaswa kuutumia vema msimu huu kwa kulima zao la pamba ambalo litawapatia fedha nyingi.

Mtaka alieleza kuwa wakulima wa Maswa na Mkoa mzima wageuze ujenzi wa kiwanda cha bidhaa za afya kuwa ni fursa ya kujiongezea kipato kwa kuzalisha zaidi zao la pamba ambalo ndilo litakuwa  malighafi kuu katika uzalishaji wa kiwanda hicho.

Aidha alisema   katika msimu msimu huu mpya wa mwaka 2017/2018 wakulima hao wanatakiwa kuondoa mazalia ya pamba yaliyobaki mashambani mwao na kisha kulima kwa kufuata kanuni bora za kilimo hicho.

"Katika msimu huu ninawaomba wakulima wote waondoe mazalia ya zao la pamba yaliyobaki mashambani kwa kuyachoma moto ili wasije kuharibu na kuambukiza magonjwa katika mbegu mpya na bora watakazozitumia...pia katika kupanda mpande kwa kuzingatia sentimeta 90 hadi 40 zilizoainishwa kitaalamu kutoka mstari hadi mstari....alisema Mtaka

Aidha wakulima hao hawakusita kueleza kero zao na kuitupia lawama bodi ya pamba kwa kushindwa kusimamia zao hilo huku wakidai kutoichafua  kwa kuweka maji na mchanga katika zao hilo.

Irene Joseph mkulima kutoka katika kata ya Kadoto alifafanua kuwa wakulima wamekuwa wakionewa na kusingiziwa visingizio vingi juu ya uchafuzi wa  zao hilo ,huku akieleza tuhuma hizo kuwa  si za kweli na kubainisha kuwa bodi ya pamba inapaswa kutimiza wajibu wake  katika kulisimamia zao la pamba na kutoa  elimu ya kutosha kwa wakulima .

Naye afisa kilimo wa Wilaya ya Maswa Christopher Simwimba amewataka wakulima kutumia mbolea ya samadi katika kuongeza rutuba kwenye mashamba yao .

Afisa huyo aliongeza kusema kuwa wakulima wanatakiwa kubadilika na kulima kisasa ili waweze kuendana na falsafa ya serikali ya viwanda ambapo wakulima ndio wanategemewa wao kuwa ni wazalishaji wa malighafi za viwandani.

Naye mkuu wa Wilaya ya Maswa Dkt Seif Shekilage alisema kuwa katika kuhakikisha wanaboresha na kuliinua zao la pamba Halmashauri yake imeweza kuwasaidia vikundi vya vijana na wanawake wanajihusisha na kilimo kuwapatia mkopo wa Milioni 50 kwa vikundi 16 vinavyotarajia kulima zao la pamba kwa msimu huu.

 Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka katikati (wa tatu kushoto) akiteta jambo na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Maswa Paul Jidai,( kushoto ) Kaimu Katibu Tawala Mkoa Simiyu, Ndg.Donatus Weginah.

 Mkuu wa Wilaya ya Maswa Dk Seif Shekalage akitoa ufafanuzi wa namna Wilaya yake ilivyojipanga kuongeza uzalishaji wa zao la pamba.
Wakulima kutoka katika kata 36 za Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu wakiwa katika mkutano wa pamoja Viongozi wa Mkoa  na  Wilaya(hawapo pichani)  ukiwa na lengo la kujadili na kupokea maelekezo ya kilimo katika msimu mpya wa 2017/2018.

HALMASHAURI YA MASWA YATOA MIL 50 KWA VIJANA NA WANAWAKE

Jumla ya vikundi 16 vya  wanawake na vijana vilivyopo katika kata 36  Wilayani Maswa  Mkoani Simiyu vimepatiwa mkopo wa shilingi Milioni 50 kwa ajiri ya kuboresha kilimo cha pamba katika maeneo yao.

Vikundi hivyo  ambavyo hujishughulisha  na kilimo cha pamba vimepokea hundi hiyo  katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, wakati wa uzinduzi wa msimu wa kilimo wa mwaka 2017/2018.

Akizindua msimu wa kilimo na kukabidhi hundi kwa vikundi hivyo Mkuu wa Wilaya ya Maswa Dkt Seif Shekalage alisema halmashauri imetekeleza sera ya kuwawezesha vijana na wanawake kwa kuwajengea uwezo katika kujiletea maendeleo ya kujikomboa na umaskini.

Alisema halmashauri imefanikiwa kutekeleza sera hiyo ya kutoa asilimia 5 kwa wanawake na 5 kwa  vijana ili kuhakikisha wanajenga uchumi na kipato cha kila mwananchi wa Wilaya hiyo.

Dk Shekalage aliongeza kuwa akinamama na vijana wanapaswa kutambua matumizi sahihi na makusudio ya mkopo waliopokea ili uweze kuwanufaisha katika shughuli zao za kilimo.

Aidha kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya Maswa Roggers  Limo alisema  kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita 2013/2014 hadi 2016/2017 Wilaya yao ilitoa mkopo wa kiasi cha shilingi Mil 75,955,000 kwa vikundi vya wanawake  na shilingi 105,182,500 kwa vikundi vya vijana  ambapo Milioni 30,162 ,500 ni mapato ya ndani ya Halmashauri.

Hata hivyo Afisa kilimo wa Wilaya hiyo Christopher Simwimba alivitaka vikundi hivyo kutumia mkopo huo ipasavyo na kuhakikisha kabla ya kuanza kupanda katika mashamba yao ni lazima waondoe mazalia ya pamba yaliyokuwa yamebaki ili yasije kuharibu pamba mpya itakayopandwa.

Simwimbi pia aliwasihi wakulima hao kupitia vikundi vyao kutumia mbolea ya samadi ili kurutubisha udongo wa mashamba yao sambamba na kupanda kitaalamu wa kuzingatia sentimeta 90 hadi 40  kwa kila mstari .

Nao baadhi wa wanakikundi vya vikundi hivyo wameishukuru Halmashauri hiyo kwa jitihada wanazozifanya za kuhakikisha wanainua na kufufua kilimo cha zao la pamba ambalo limeonekana kushuka kwa kiwango cha uzalishaji.

Haji Mwarabu mwanakikundi kutoka katika kikundi cha Huruma katika kata ya Mataba aliihakikishia Halmashauri hiyo kupitia Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri yao Dkt Fredrick Sagamiko kuwa watautumia vizuri mkopo huo ili waweze kubadilisha maisha yao kupitia kilimo cha pamba.
 Mkuu wa Wilaya ya Maswa Dkt Seif Shekalage akiwa katika picha ya pamoja na wawakilishi wa vikundi vya wanawake na vijana wakati wa makabidhiano ya hundi ya Milioni 50 kwa vikundi 16 wilayani humo.
Baadhi ya wanavikundi vya vijana na wanawake Wilayani Maswa ,watendaji wa Halmashauri na Baadhi ya madiwani wakiwa katika uzinduzi wa msimu wa Kilimo mwaka 2017/2018  na utoaji wa hundi ya shilingi Milioni 50 kwa vikundi vya  wanawake na vijana .
Baadhi ya wanavikundi vya vijana na wanawake Wilayani Maswa ,watendaji wa Halmashauri na Baadhi ya madiwani wakiwa katika uzinduzi wa msimu wa Kilimo mwaka 2017/2018  na utoaji wa hundi ya shilingi Milioni 50 kwa vikundi vya  wanawake na vijana .
Mkuu wa Wilaya ya Maswa Maswa Dkt Seif Shekalage (kushoto)akijiandaa zoezi la uzinduzi wa ugawaji wa mbegu kwa wakulima katika uzinduzi wa msimu wa kilimo
Mkuu wa Wilaya ya Maswa Maswa Dkt Seif Shekalage (KATIKATI) akiwa katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Mhe.Lucas Mwaniyuki ,pamoja na baadhi ya madiwani wa halmashauri ya maswa mara baada ya makabidhiano ya hundi ya Milioni 50 kwa vikundi 16 vya wanawake na vijana vinavyojihusisha na kilimo.
Mkuu wa Wilaya ya Maswa Maswa Dkt Seif Shekalage akimkabidhi mbegu za pamba aina ya YKM08 mwanakikundi cha mama na mtoto ni familia kutoka katika kata ya Kadeto Veronica Seloli wakati wa uzinduzi wa msimu wa kilimowilayani humo.

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!