Thursday, November 2, 2017

WAKULIMA MKOANI SIMIYU WATAKIWA KULIMA MAZAO YA BIASHARA

Mkuu wa mkoa wa Simiyu,Anthony Mtaka amewasisitiza wakulima Mkoani humo kulima mazao ya biashara yenye  tija hasa zao la pamba kwa kuzingatia Mkoa huo upo katika mchakato wa utekelezaji wa ujenzi wa kiwanda cha bidhaa za afya zitokanazo na  zao la pamba.

Msisitizo huo ameutoa jana wilayani Maswa katika ziara yake ya kuhamasisha kilimo kuelekea msimu wa kilimo na kueleza kuwa wakulima wanapaswa kuutumia vema msimu huu kwa kulima zao la pamba ambalo litawapatia fedha nyingi.

Mtaka alieleza kuwa wakulima wa Maswa na Mkoa mzima wageuze ujenzi wa kiwanda cha bidhaa za afya kuwa ni fursa ya kujiongezea kipato kwa kuzalisha zaidi zao la pamba ambalo ndilo litakuwa  malighafi kuu katika uzalishaji wa kiwanda hicho.

Aidha alisema   katika msimu msimu huu mpya wa mwaka 2017/2018 wakulima hao wanatakiwa kuondoa mazalia ya pamba yaliyobaki mashambani mwao na kisha kulima kwa kufuata kanuni bora za kilimo hicho.

"Katika msimu huu ninawaomba wakulima wote waondoe mazalia ya zao la pamba yaliyobaki mashambani kwa kuyachoma moto ili wasije kuharibu na kuambukiza magonjwa katika mbegu mpya na bora watakazozitumia...pia katika kupanda mpande kwa kuzingatia sentimeta 90 hadi 40 zilizoainishwa kitaalamu kutoka mstari hadi mstari....alisema Mtaka

Aidha wakulima hao hawakusita kueleza kero zao na kuitupia lawama bodi ya pamba kwa kushindwa kusimamia zao hilo huku wakidai kutoichafua  kwa kuweka maji na mchanga katika zao hilo.

Irene Joseph mkulima kutoka katika kata ya Kadoto alifafanua kuwa wakulima wamekuwa wakionewa na kusingiziwa visingizio vingi juu ya uchafuzi wa  zao hilo ,huku akieleza tuhuma hizo kuwa  si za kweli na kubainisha kuwa bodi ya pamba inapaswa kutimiza wajibu wake  katika kulisimamia zao la pamba na kutoa  elimu ya kutosha kwa wakulima .

Naye afisa kilimo wa Wilaya ya Maswa Christopher Simwimba amewataka wakulima kutumia mbolea ya samadi katika kuongeza rutuba kwenye mashamba yao .

Afisa huyo aliongeza kusema kuwa wakulima wanatakiwa kubadilika na kulima kisasa ili waweze kuendana na falsafa ya serikali ya viwanda ambapo wakulima ndio wanategemewa wao kuwa ni wazalishaji wa malighafi za viwandani.

Naye mkuu wa Wilaya ya Maswa Dkt Seif Shekilage alisema kuwa katika kuhakikisha wanaboresha na kuliinua zao la pamba Halmashauri yake imeweza kuwasaidia vikundi vya vijana na wanawake wanajihusisha na kilimo kuwapatia mkopo wa Milioni 50 kwa vikundi 16 vinavyotarajia kulima zao la pamba kwa msimu huu.

 Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka katikati (wa tatu kushoto) akiteta jambo na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Maswa Paul Jidai,( kushoto ) Kaimu Katibu Tawala Mkoa Simiyu, Ndg.Donatus Weginah.

 Mkuu wa Wilaya ya Maswa Dk Seif Shekalage akitoa ufafanuzi wa namna Wilaya yake ilivyojipanga kuongeza uzalishaji wa zao la pamba.
Wakulima kutoka katika kata 36 za Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu wakiwa katika mkutano wa pamoja Viongozi wa Mkoa  na  Wilaya(hawapo pichani)  ukiwa na lengo la kujadili na kupokea maelekezo ya kilimo katika msimu mpya wa 2017/2018.

0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!