Saturday, February 17, 2018

WAZIRI WA UJENZI AMTAKA MKANDARASI WA BARABARA YA BARIADI-MASWA KUKAMILISHA UJENZI JUNI 2019


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa amemuagiza Mkandarasi wa Mradi wa Ujenzi wa barabara ya Bariadi-Maswa yenye urefu wa Kilomita 49.7 kukamilisha mradi huo Juni 2019.

Waziri Mbarawa amesema hayo wakati alipotembelea Kambi ya Mkandarasi CHICCO anayetekeleza Mradi huo iliyopo kata ya Luguru wilayani  Itilima wakati wa Ziara yake Mkoani Simiyu .

Amesema barabara hiyo iliyopangwa kujengwa kwa miezi 24 kuanzia Mwezi Oktoba 2017,  itajengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 86.9 na tayari Serikali imeshamlipa Mkandarasi shilingi Bilioni 8.9.

Amemuelekeza Mkandarasi CHICCO kutekeleza ujenzi wa barabara hiyo na  kuahidi kuwa Serikali itamsimamia na kuhakikisha mradi huo unakamilika mwezi Juni 2019, jambo ambalo limekubaliwa na Mkandarasi huyo.

“Tutahakikisha tunamsimamia Mkandarasi  masaa yote usiku na mchana ili barabara hii imalizike kwa wakati na tutamlipa fedha kila anapoleta ‘certicate’ kazi hii isisimame tena, nawaagiza TANROADS na Mkandarasi Mshauri kusimamia barabara hii ili thamani ya fedha ionekane” alisema Mbarawa.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka ameshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. John Pombe Magufuli kutekeleza ahadi aliyoitoa mwezi Januari 2017 katika ziara yake Mkoani humo, ambapo amebainisha kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kutaufungua Mkoa huo kibiashara.

Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Mhe. Enock Yakobo ameshukuru juhudi zinazofanywa na Serikali kwa mkoa huo kwa kuwa ulipoanzaishwa mwaka 2012 barabara zilikuwa zinapitika kwa shida,  lakini sasa wananchi wanatumia muda mfupi kwenda maeneo mbalimbali, hivyo amesema barabara hiyo itakapokamilika nayo itachangia kurahisisha usafirishaji.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi wa Kijiji cha Banya wilayani Itilima mahali inapojengwa Kambi ya Mkandarasi CHICCO wamelalamikia suala la mkandarasi kuchukua vibarua wa kufanya kazi za mradi nje ya Mkoa pamoja na malipo yasiyoridhisha  kwa wale waliopata nafasi ya kufanya kazi katika mradi huo.

“Mhe.  Waziri hivi ni  sahihi kweli barabara ijengwe hapa kwetu halafu vibarua watoke mikoa mingine , mimi naona siyo sawa  tunaomba Serikali itusaidie na sisi wananchi wa hapa tupate kazi; pia hata hawa wanaofanya kazi hapa malipo ni kidogo elfu tano kwa siku haitoshi” alisema Samweli Jisena.

Waziri Mbarawa amemuagiza Meneja wa TANROADS Mkoa wa Simiyu, Mhandisi.Albert Kent kuhakikisha kuwa anasimamia suala la wananchi wa eneo la mradi kupewa kazi na mkandarasi na upande malipo amewataka wafanyakazi kukubaliana na mkandarasi juu ya malipo yao.

Ujenzi wa Barabara ya Bariadi-Maswa ni ahadi ya Rais wa Tanzania, Mhe.Dkt. John Pombe Magufuli aliyoitoa Januari 11, 2017 akiwa katika ziara yake ya siku mbili mkoani Simiyu mara baada ya kufungua barabara ya Lamadi-Bariadi yenye urefu wa Kilomita 71.8 mjini Bariadi.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa (wa pili kulia), Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka(kulia) wakichota udongo na makoleo kujazia sehemu inapojengwa Kambi ya Mkandarasi CHICCO anayetekeleza mradi wa Ujenzi wa Barabara ya Bariadi Maswa wakati wa ziara yake Mkoani Simiyu.


Meneja wa TANROADS Mkoa wa Simiyu, Mhandisi.Albert Kent akitoa maelezo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa(wa pili kushoto,  alipotembelea eneo la ujenzi wa Kambi ya Mkandarasi CHICCO anayetekeleza mradi wa Ujenzi wa Barabara ya Bariadi- Maswa wakati wa ziara yake Mkoani Simiyu.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa (wa tatu kulia) akitoa maelekezo kwa Mkandarasi CHICCO anayetekeleza mradi wa Ujenzi wa Barabara ya Bariadi- Maswa wakati wa ziara yake Mkoani Simiyu.
Mjumbe wa Halmashuri Kuu ya CCM (NEC), Gungu Silanga  akieleza juu Ujenzi wa mradi wa barabara ya Bariadi-Maswa kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa wakati wa ziara yake katika  eneo la ujenzi wa Kambi ya Mkandarasi CHICCO anayetekeleza mradi huo  Mkoani Simiyu.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Mhe.Enock Yakobo(kulia)akieleza juu ya Ujenzi wa mradi wa barabara ya Bariadi-Maswa kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa wakati wa ziara yake katika  eneo la ujenzi wa Kambi ya Mkandarasi CHICCO anayetekeleza mradi huo  Mkoani Simiyu.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa,  akimsikiliza Samweli Jisena mwananchi kutoka Kata ya Luguru  akitoa malalamiko yake, wakati alipotembelea  eneo la ujenzi wa Kambi ya Mkandarasi CHICCO anayetekeleza mradi wa Ujenzi wa Barabara ya Bariadi- Maswa Mkoani Simiyu.
Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Mhe.Benson Kilangi (kushoto) akieleza jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa (hayupo pichani) wakati wa ziara yake katika  eneo la ujenzi wa Kambi ya Mkandarasi CHICCO anayetekeleza mradi wa Ujenzi wa Barabara ya Bariadi- Maswa Mkoani Simiyu.

0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!