Thursday, February 22, 2018

MAKAMU WA RAIS: ELIMU YA JUU NI NGUZO MUHIMU KATIKA KUFIKIA TANZANIA YA VIWANDA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Elimu hususani ya juu ni nguzo Muhimu ya kufikia Agenda ya Serikali ya kuwa na Tanzania ya Viwanda na kufikia Uchumi wa Kati ifikapo 2025.


Makamu wa Rais wa amesema hayo ,wakati wa akifungua kongamano la elimu ya juu na Tanzania ya viwanda lililofanyika mjini Bariadi, lililokuwa limeandaliwa na Chuo kikuu huria Tanzania kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu.

Amesema kutokana na umuhimu huo Serikali imeamua kuwekeza katika Elimu na Dira ya Maendeleo ya Mwaka 2025 imeweka elimu kuwa kipaumbele cha juu kwa kuwa ndiyo kitovu cha  kuleta mabadiliko ya kiuchumi katika jamii.

“Ninyi ni mashahidi kuwa Serikali imeweka mkazo kwenye elimu, tumeanza na shule za msingi, sekondari lakini pia tumeongeza bajeti kubwa kwenye mikopo ya Elimu ya Juu na tutakwenda polepole mpaka tuhakikishe Watanzania wanapata elimu ya kutosha ili kuendana na uchumi wa Viwanda” alisema.

Ameongeza kuwa  lengo kuu la ni Serikali kuongeza kipato cha wananchi kupitia viwanda ambavyo vitaongeza thamani ya mazao yanayozalishwa katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Aidha, amewataka washiriki wa Kongamano hilo kuja na majibu ya ni kwa  namna gani wahitimu wa Vyuo Vikuu walivyojipanga katika suala la uzalishaji viwandani na kubainisha  ikiwa fani, stadi na mafunzo waliyosomea yatakidhi mahitaji ya  viwanda vinavyotakiwa kujengwa hapa nchini.

Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Prof.Elifas Bisanda amesema nchi zote zilizoendelea katika Sekta ya Viwanda zina msukumo mkubwa na udahili mkubwa wa Wanafunzi wa Elimu ya Juu, hivyo  upo umuhimu wa kujadili Mchango wa Elimu ya Juu katika Tanzania ya Viwanda.

Aidha, Prof.Bisanda ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Simiyu kutumia fursa ya uwepo wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kwa ajili ya kujiendeleza katika masomo ya elimu ya juu.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka amewataka waajiri wote mkoani humo kuwaruhusu watumishi kwenda kusoma kwa ajili ya kuwaandaa watumishi hao kuwa na maarifa ya kutosha.

 Tuna shida kwenye ofisi zetu  tena wakati mwingine  ni roho mbaya tu, mtumishi anaomba kwenda kusoma Mkurugenzi anamkatalia, tukitaka nchi yetu iende mbele turuhusu watu wasome,  miaka ijayo tunataka mkoa wetu ushindane hatuwezi kushindana kama hatutawekeza kwenye maarifa” alisisitiza Mtaka.

Wasomi waliowasilisha mada mbalimbali katika Kongamo hilo la Elimu ya Juu na Tanzania ya Viwanda ni pamoja na Prof. Rwekaza Mukandala, Prof.Elifas Bisanda , Prof.Uswege Minga, Dkt. Adolf Rutayuga, Dkt. George Mgode, Balozi Nicholas Kuhanga na Mhe.Anthony Diallo.

Kongamano hili lililokuwa na Mada kuu isemayo: “Mustakabali wa Elimu ya Juu kuelekea Tanzania ya Viwanda” limehudhuriwa na wanafunzi wa shule za sekondari, walimu, Wanafunzi wa Vyuo Vikuu kutoka Mwanza pamoja na viongozi wa Serikali.
MWISHO


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan aifungua Kongamano la Elimu ya Juu na Tanzania ya Viwanda lililofanyika Mjini Bariadi.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na Washiriki wa Kongamano la Elimu ya Juu lililofanyika Mjini Bariadi.
Baadhi ya Washiriki wa Kongamano la Elimu ya Juu na Tanzania ya Viwanda kutoka ndani na nje ya Mkoa wa Simiyu wakifuatilia ufunguzi wa Kongamano hilo uliofanywa na  Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan mjini Bariadi.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Prof. Elifas Bisanda akizungumza na Washiriki wa Kongamano la Elimu ya Juu lililofanyika Mjini Bariadi(hawapo pichani)
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan(wa pili kushoto) akifurahia jambo na viongozi wa Mkoa wa Simiyu wakati wa Kongamano la Elimu ya Juu na Tanzania ya Viwanda lililofanyika Mjini Bariadi.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan(katikati walioketi ) akiwa katika picha ya pamoja na wawasilishaji wa mada  wa Kongamano la Elimu ya Juu na Tanzania ya Viwanda lililofanyika Mjini Bariadi.(waliosimama mstari wa nyuma) na viongozi wengine kutoka ndani na nje ya mkoa wa Simiyu.

0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!