Wednesday, May 24, 2017

WANUFAIKA TASAF WAHIMIZWA KUWAPELEKA WATOTO SHULE, KLINIKI

Wanufaika wa Mradi wa Mpango wa Kunusuru kaya maskini TASAF III hususani wanaopewa ruzuku ya utimizaji wa masharti ya elimu na afya wamehimizwa kuwapeleka watoto kliniki na kuhakikisha watoto wao wanahudhuria shuleni.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Ndani kutoka TASAF Makao Makuu, Ndg. Christopher Sanga katika kijiji cha Migato wilayani Itilima wakati wa ziara ya tathmini ya utekelezaji mradi wa TASAF wilayani humo.

Sanga amesema Serikali ina mpango mzuri kwa wananchi wa kuhakikisha watoto wote wenye umri wa kwenda shule wanapelekwa shule na pia watoto wote wenye umri chini ya miaka mitano wanapelekwa kiliniki na kupata  huduma za afya zinazotakiwa, hivyo akawaasa kutorudisha nyuma juhudi za Serikali.

Aidha, amesema lengo kuu la Serikali ni kuhakikisha nguvu kazi inajengwa kwa kutoa elimu na kuangalia afya za watoto wakiwa bado wadogo ili watakapobainika kuwa na matatizo ya kiafya wapatiwe matibabu mapema kwa lengo la kuimarisha afya na  kutoathiri ukuaji wao.

Ameongeza kuwa utafiti uliofanyika kuhusu utekelezaji wa awamu zilizotangulia za Mpango wa TASAF ulionesha kuwa, kumekuwa na miundombinu mingi ya elimu na afya lakini kaya maskini zimekuwa hazipeleki watoto katika huduma hizo, hivyo Serikali ikatoa ruzuku ya elimu na afya na kuwawekea masharti wazazi ili kuhakikisha wanawapeleka watoto katika huduma hizo.

Amesisitiza kuwa Mpango wa TASAF unafuatilia mahudhurio ya watoto wanaopata ruzuku ya utimizaji wa masharti ya elimu na ili ruzuku hiyo iendelee kutolewa kwa wanafunzi hao ni lazima mahudhurio yao yasiwe chini ya asilimia 80 kwa muhula, wasipohudhuria kuna adhabu inayotolewa ikiwa ni pamoja na kupunguzwa kwa ruzuku hiyo.

“ Miongoni mwa madhara ya watoto kutohudhuria masomo katika muhula husika kwa kaya zinazonufaika na TASAF kwa kupata ruzuku ya elimu ambayo inasaidia kaya hizo, ni kupungua kwa ruzuku na inapopungua uwezo wa kaya katika kujikimu na kufanya mabadiliko ya kiuchumi  unaathirika” amesema Sanga.

Kwa upande wake Bibi. Ngolo Buzenganwa mkazi wa kijiji cha Migato ambaye ni mnufaika wa Mpango wa TASAF III amewataka wazazi wenzake kufuatilia maendeleo ya watoto wao na kukagua daftari zao mara kwa mara ili ruzuku inayotolewa isipunguzwe na iwasaidie kuwawezesha kupata mahitaji muhimu ya shule kwa ajili ya watoto wao.

Katika hatua nyingine wanufaika wa Mpango wa TASAF III wameshukuru mpango huo kwa kutatua changamoto ya upungufu wa maji kwa kuwachimbia visima vya maji kupitia programu ya kazi za ajira za muda na kuomba kuongezewa idadi ya visima hivyo katika awamu nyingine ya utekelezaji wa mradi.

“Tunaishukuru sana TASAF kutuletea maji kwa visima hivi, tulikuwa tunatembea muda mrefu sana zaidi ya saa moja kufuata maji, lakini sasa hivi maji yapo karibu tena ni maji safi na salama” amesema Maila Limbu mkazi  wa Migato.

Naye Mhandisi wa Maji wa Halmashauri ya Wilaya ya Itilima,Goodluck Masige amesema Serikali Wilayani humo imeweka mpango wa kuviwekea pampu visima vyote 194 vilivyochimbwa kupitia mradi wa TASAF ili kuwarahisishia wananchi kupata maji kwa urahisi zaidi kuliko teknojia inayotuika sasa ya kuvuta kwa kamba.


Wilaya Itilima ni moja ya Wilaya tano zinazofanyiwa tathmini ya utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru kaya Maskini (TASAF III) katika awamu hii, tathmini inayofanywa na wataalam kutoka TASAF Makao Makuu, Benki ya Dunia na wadau wengine wa maendeleo (wadau washiriki wa mradi) ambao ni UNDP, UNFPA, ILO pamoja na Umoja wa Nchi za Ulaya(EU).
Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Ndani kutoka TASAF Makao Makuu, Ndg. Christopher Sanga(wa pili kulia) akizungumza na wanufaika wa TASAF III katika kijiji cha Migato wilaya ya Itilima.
Ndg. Wolter Soer (wa pili kushoto) kutoka Benki ya Dunia akizungumza na baadhi ya wanufaika wa TASAF III katika kijiji cha Migato wilaya ya Itilima katika majadiliano yaliyofanywa katika vikundi kupata maoni ya tathmini ya utekelezaji wa mpango huo.
Mnufaika wa TASAF III kutoka kijiji cha Migato wilaya ya Itilima akichota maji katika moja ya visima vilivyochimbwa na TASAF kupitia programu ya kazi za ajira za muda katika kijiji hicho.
Ndg. Wolter Soer kutoka Benki ya Dunia(wa kwanza kushoto) na Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Ndani kutoka TASAF Makao Makuu, Ndg. Christopher Sanga(mwenye miwani) wakimsikiliza mmoja wa wanufaika wa TASAF III katika Kijiji cha Migato akiwaeleza juu faida anazopata kupitia fedha anazopokea kupitia mpango huo.
Mmoja wa wanufaika wa TASAF III katika Kijiji cha Migato akipokea fedha katika zoezi la uhawilishaji lililofanyika kijijini hapo
Baadhi ya wanufaika wa TASAF III wa Kijiji cha Migato wakiimba wimbo maalum wa kuwakaribisha wataalam kutoka TASAF Makao Makuu, Benki ya Dunia na wadau wengine wa maendeleo (wadau washiriki wa mradi) ambao ni UNDP, UNFPA, ILO na Umoja wa Nchi za Ulaya(EU) waliofika kufanya tathmini ya utekelezaji wa mradi wa TASAF III Wilayani Itilima.
Mnufaika wa TASAF III kutoka kijiji cha Migato wilaya ya Itilima akichota maji katika moja ya visima vilivyochimbwa na TASAF kupitia programu ya kazi za ajira za muda katika kijiji hicho.

0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!