Wednesday, July 13, 2016

SERIKALI YA CHINA YAMUUNGA MKONO JPM KUELEKEA TANZANIA YA VIWANDA



Serikali ya CHINA imeahidi kushirikiana na Mkoa wa Simiyu katika uwekezaji  hususani katika maeneo ya viwanda. Kilimo na uvuvi ili kutimiza azma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Magufuli ya kuwa na Tanzania ya Viwanda.

Hayo yamesemwa na Balozi Mshauri wa China nchini, Bw.Zhang Biao wakati alipofanya ziara yake mkoani Simiyu na kufanya mazungumzo na Uongozi wa Mkoa wa Simiyu na wadau wa maendeleo mkoani humo.

Balozi Zhang amesema endapo  Serikali itatengeneza mazingira wezeshi kwa kujenga miundombinu kwa ajili ya uwekezaji, Makampuni kutoka China yatakuwa tayari kuwekeza mkoani Simiyu.

“ Mkoa wa Simiyu una maliasili nyingi na kwa kuwa mmeonyesha utayari Makampuni ya China yatakuja kuwekeza kwa kasi, Serikali isaidie kuwezesha huduma za maji na umeme zinapatikana na miundombibu ya kusafirisha malighafi kupelekeka viwandani na kupeleka bidhaa zetu zitakazozalishwa sokoni”, alisema Balozi Zhang.

Akitoa shukrani kwa niaba ya Serikali Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony. J. Mtaka amesema Serikali iko tayari kutenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji  na kuhakikisha miundombinu muhimu kama maji na umeme inapatikana kwa ajili ya kuwezesha uwekezaji na akamuomba  Balozi Zhang kuunganisha Mkoa wa Simiyu na Makampuni ya China yaliyo tayari kuwekeza.  

“ Mkoa wa Simiyu una fursa nyingi sana za uwekezaji katika eneo la viwanda vya nguo na nyuzi kwa kuwa unazalisha karibu asilimia 60 ya pamba ya nchini, lakini pia mkoa wetu ni wa tatu kwa kuwa na ng’ombe wengi kwa hiyo bado kuna fursa ya uwekezaji katika mazao ya ufugaji wa ng’ombe kama nyama, ngozi na maziwa” , alisema Mtaka.

Aidha, Mtaka alisema kupitia sehemu ya Ziwa Viktoria mkoa una fursa ya uwekezaji katika kilimo cha umwagiliaji ambacho alieleza kinaweza kusaidia kuinua uchumi wa wakazi wa wilaya ya Busega na Mkoa wa Simiyu kwa ujumla, ambapo Serikali inaandaa mpango wa kuwa na zao moja kwa wilaya moja (one product one district)  ili kila wilaya iwe na zao au shughuli moja inayowaingizia watu wake kipato.

Hii ni mara ya kwanza kwa Balozi Mshauri wa China nchini kufika mkoani Simiyu ambapo Balozi Zhang ameahidi kuendeleza urafiki wa nchi ya Tanzania na China ambao ulianza tangu enzi za Rais wa awamu ya kwanza Hayati Julius K. Nyerere na kuhakikisha uhusiano kati ya nchi hizi mbili unawanufaisha wananchi wa pande zote mbili.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony J. Mtaka  akimshukuru Balozi Mshauri wa China nchini Tanzania Bw.Zhang Biao mara baada ya kuzungumza na Viongozi na wadau wa maendeleo  (hawapo pichani) wakati wa ziara yake mkoani Simiyu. (Picha na Stella A. Kalinga 
Katibu Tawala mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne A. Sagini (kulia) akizungumza jambo na Balozi Mshauri wa China nchini, Bw.Zhang Biao (katikati) mara baada ya kumaliza mazungumzo  na Viongozi na wadau wa maendeleo (hawapo pichani) wakati wa ziara yake mkoani Simiyu,  (kushoto) Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony J. Mtaka. (Picha na Stella A. Kalinga)
Balozi Mshauri wa China nchini, Bw.Zhang Biao (wa nne kulia) akiwa katika picha ya pamoja na  Viongozi na wadau wa maendeleo wakati wa ziara yake mkoani Simiyu, (kushoto kwake) Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga, (kulia kwake) Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony J. Mtaka, anayefuata Katibu Tawala Mkoa, Bw. Jumanne A. Sagini (Picha na Stella A. Kalinga)

0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!