Saturday, May 21, 2016

SAGINI: WAKUU WA IDARA ZINGATIENI USHAURI WA WAKAGUZI WA NDANI HALMASHAURI ZIPATE HATI SAFI




Wakuu wa Idara wametakiwa kuzingatia ushauri wa Wakaguzi wa Ndani wa kujibu hoja inavyotakiwa ili Halmashauri zao zisipate hati zenye masahaka au hati chafu..

Hayo yalisemwa na Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne A.Sagini wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya usimamizi wa fedha, mipango na bajeti, uwekezaji, uimarishaji ukusanyaji wa mapato, taratibu za ukaguzi wa ndani na manunuzi ya umma kwa wahasibu, wakaguzi wa ndani, maafisa ugavi na maafisa mipango wa Halmashauri zote za Mkoa wa Simiyu, yaliyofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya wilaya ya Meatu.

Mbali kuzisaidia Halmashauri  kutopata hati za mashaka au chafu kutoka kwa mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) taarifa za mkaguzi wa ndani zinasaidia menejimenti kutambua kasoro za mfumo wa usimamizi wa fedha ndani ya taasisi na kuziondoa kwa kuzingatia sheria na kanuni za umma.

“Mkaguzi wa Ndani ni Jicho la Afisa Masuuli kumwezesha kujua kama matumizi ya fedha za Umma yanafuata taratibu na miongozo ya usimamizi wa fedha za Umma iliyopo na anawakumbusha wakuu wa Idara na Vitengo kujibu Hoja za Mkaguzi wa Ndani ya siku saba kama sheria inavyotaka, ” , alisema Sagini

Sagini alisema kuwa mafunzo hayo yamelenga katika umuhimu wa usimamizi wa rasilimali fedha ikiwa kama kiungo cha kuwezesha kutoa huduma bora kwa wananchi, ambapo wataongeza utambuzi, namna ya kuanzisha wazo la uwekezaji na namna ya kupata fedha za miradi katika kufanya uwekekezaji katika sekta ya umma.

Kwa upande wake Thomas Magambo ambaye ni mtaalamu mshauri wa mradi wa PFMRP IV Mkoa wa Mara na Simiyu amesema kuwa mafunzo hayo yanalenga kuboresha mfumo wa manunuzi ya umma, ukusanyaji mapato na uwekezaji ndani ya halmashauri ili kuongeza ukusanyaji mapato na kuwezesha kupata hati safi.

Naye  Donatus Wegina, Katibu Tawala Msaidizi wa Mipango na Uratibu katika Sekretarieti ya Mkoa wa Simiyu, alisema kuwa mafunzo hayo yamefanyika ili kuwajengea uwezo wasimamizi wa fedha za ndani, ukaguzi wa ndani, manunuzi, mipango na bajeti ili mipango inayoandaliwa iweze kusaidia Halmashauri kupata hati safi na kuhakikisha kuwa fedha za Umma zinatumika kwa kufuata miongozo na taratibu za kibajeti kwa manufaa ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

Katika ukaguzi uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa hesabu za mwaka 2014/2015 Halmashauri za Itilima, Bariadi Mji na Busega zimepata hati safi wakati huo Halmashauri za Meatu, Maswa na Bariadi vijini  zimepata hati zenye mashaka.


Katibu Tawala Mkoa Simiyu, Jumanne A. Sagini akizungumza na wahasibu, wakaguzi wa ndani, maafisa ugavi na maafisa mipango wa Halmashauri za Mkoa wa Simiyu (hawapo pichani) wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya usimamizi wa fedha, mipango na bajeti, uwekezaji, ukusanyaji mapato na taratibu a ukaguzi wa ndani na manunuzi ya umma. Picha na Stella A. Kalinga
Katibu Tawala Mkoa Simiyu, Jumanne A. Sagini (wa nne kulia) akiwa katika picha ya pamoja na wahasibu, wakaguzi wa ndani, maafisa ugavi na maafisa mipango wa Halmashauri za Mkoa wa Simiyu na wawezeshaji , mara baada ya ufunguzi wa mafunzo ya usimamizi wa fedha, mipango na bajeti, uwekezaji, ukusanyaji mapato na taratibu na ukaguzi wa ndani na manunuzi ya umma,(wa nne kushoto ) Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Godfrey Machumu Picha. Stella A. Kalinga


Katibu Tawala Mkoa, Jumanne A. Sagini akiangalia vifaa vilivyowekwa na Halmashauri ya Wilaya ya Meatu kwa ajili ya kuwekea taka ikiwa ni njia mojawapo ya kuweka safi mji wa Mwanhuzi na mkakati wa usafi na utunzaji wa mazingira Wilyani humo (wa kwanza kushoto) ni Katibu Tawala Wilaya ya Meatu, Chele Ndaki. Picha Na Stella A. Kalinga

 
Katibu Tawala Mkoa, Jumanne A. Sagini akizungumza na mafundi wanaotengeneza madawati katika moja ya karakana kwa ajili ya shule za msingi na Sekondari wilayani Meatu, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais, John Pombe Magufuli la kuhakikisha kuwa hakuna mwanafunzi anayekaa chini ifikapo Juni 30, 2016. Picha Na Stella A. Kalinga









0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!