Thursday, February 28, 2019

NAIBU WAZIRI IKUPA AWAOMBA WADAU KUWASAIDIA WALEMAVU VIFAA SAIDIZI


Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu nayeshughulikia watu wenye ulemavu, Mhe. Stella Ikupa ametoa wito kwa wadau kuendelea kutoa msaada wa vifaa saidizi kwa watu wenye ulemavu kwa kuwa hili ni hitaji endelevu kwa watu hao.

Mhe. Ikupa ameyasema hayo jana Februari 27, 2019 wakati akizungumza na viongozi na watendaji wa Serikali wilayani Busega mkoani Simiyu wakati akiwa katika ziara yake ya kikazi wilayani humo.

Amewashukuru viongozi wa Wilaya ya Busega kwa namna inavyowasaidia watu wenye ulemavu katika kuwapatia vifaa saidizi huku akibainisha kuwa Serikali inaendelea kufanya jitihada za kuwatafutia na kuwapatia watu wenye ulemavu vifaa hivyo kwa kadri vitakavyopatikana.

“Napenda kuwashukuru viongozi wa Busega kwa namna wanavyowasaidia watu wenye ulemavu kupata vifaa saidizi kama fimbo nyeupe kwa wasioona, baiskeli na viungo bandia kwa walemavu wa viungo, mafuta kwa wenye ualbino, lakini niwaombe wadau waendelee kuwasaidia kwa kuwa hili ni hitaji endelevu katika kuishi kwao.” alisema Mhe. Ikupa.

Katika hatua nyingine Mhe. Naibu Waziri amesisitiza Kamati za watu wenye ulemavu kupewa miongozo ya namna ya kuziendesha kamati hizo, ili ziweze kutimiza majukumu yake ipasavyo na kuzitaka kutoa taarifa kuhusu fursa na masuala mbalimbali yanayowahusu walemavu katika maeneo yao.

Vile vile Mhe. Ikupa amesema Serikali inatarajia kuanzisha mfuko wa watu wenye ulemavu ambao utakuwa ukishughulikia masuala mbalimbali ya watu wenye ulemavu ikiwa ni pamoja na kutoa ruzuku kwa vyama vya walemavu.

Akitoa taarifa Mkuu wa Wilaya ya Busega, Mhe. Tano Mwera, amesema Serikali wilayani imetoa baiskeli 17 kwa watu wenye ulemavu wa viungo, zaidi ya fimbo nyeupe 50 kwa wasioona, mafuta kwa watu wenye ualbino na Halmashauri imeandaa mpango maalum wa Mfuko wa Bima ya Afya(CHF) iliyoboreshwa kwa ajili ya huduma za afya kwa walemavu.

Kwa upande wao watu wenye ulemavu wameiomba Serikali na wadau kuendelea kuwapa msaada wa vifaa saidizi , kupewa elimu ya kuunda vikundi na kuandaa maandiko ya miradi na kutoa semina elekezi kwa kamati za watu wenye ulemavu.

“Mahitaji ya walemavu bado ni makubwa tunaomba wadau mbalimbali waendelee kutukumbuka kutupa msaada wa vifaa saidizi kama fimbo nyeupe kwa wasioona, viungo bandia na baiskeli kwa walemavu wa viungo lakini na mafuta kwa wenzetu wenye ualbino” alisema Katibu wa  SHIVYAWATA Wilaya ya Busega, Makasi Egonjo.

“Tunaishukuru Serikali kwa kutusaidia kwenye mahitaji yetu mengi lakini tunaendelea kuomba wasichoke kutusaidia, tunaomba maafisa ustawi wa jamii wawafikie watu wenye ulemavu mpaka waliopo vijijini ili tuwe na elimu kuhusu mambo yanayotuhusu na fursa za mikopo na ujasiriamali” alisema Mwenyekiti wa Chama cha Wasioona, John Daniel

Naye Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga amemhakikishia Naiba waziri Ikupa kuwa Mkoa wa Simiyu utaendelea kufanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa katika ziara yake na kuhakikisha walemavu wanashirikishwa na kufikiwa katika fursa mbalimbali.

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia walemavu, Mhe. Stella Ikupa amehitimisha ziara yake ya siku tatu mkoani Simiyu Febrauari 27, 2019 ambapo alipata nafasi ya kuzungumza na  viongozi wa serikali, watu wenye ulemavu na kukagua mradi wa kitalu nyumba katika Halmashauri zote sita za Mkoa wa Simiyu.
MWISHO
Katibu wa  Shirikisho la Vyama vya Watu wenye ulemavu (SHIVYAWTA) Wilaya ya Busega, Makasi Egonjo akiwasilisha taarifa ya watu wenye ulemavu kwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia walemavu, Mhe. Stella Ikupa, wakati wa ziara yake Wilayani humo Februari 27, 2019
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia walemavu, Mhe. Stella Ikupa, akizungumza na viongozi wa Serikali na watu wenye ulemavu  wilayani Busega, wakati wa ziara yake Wilayani humo Februari 27, 2019.
 Mwenyekiti wa Chama cha Wasioona, John Daniel akiwasilisha hoja kwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia walemavu, Mhe. Stella Ikupa, wakati wa ziara yake Wilayani humo Februari 27, 2019. 
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia walemavu, Mhe. Stella Ikupa, akizungumza jambo na viongozi wa Serikali na watu wenye ulemavu  wilayani Busega, wakati wa ziara yake Wilayani humo Februari 27, 2019.
 Mwakilishi wa Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mhe. Athony Mtaka ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga akizungumza na viongozi na watu wenye ulemavu wilayani Busega, wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia walemavu, Mhe. Stella Ikupa, Wilayani humo Februari 27, 2019.
Mkuu wa Wilaya ya Busega, Mhe. Tano Mwera akiwasilisha taarifa ya wilaya kwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia walemavu, Mhe. Stella Ikupa, wakati wa ziara yake Wilayani humo Februari 27, 2019.
 Baadhi ya Wakuu wa Idara wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega wakifuatilia kati ya viongozi wa watendaji wa wilaya hiyo, watu wenye ulemavu na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia walemavu, Mhe. Stella Ikupa, wakati wa ziara yake Wilayani humo Februari 27, 2019.




Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia walemavu, Mhe. Stella Ikupa akiwaaga baadhi ya viongozi na watendaji wa serikali pamoja na watu wenye ulemavu wilayani Busega(baadhi hawapo pichani) mara baada ya kukamilisha ziara yake wilayani humo,  Februari 27, 2019




Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia walemavu, Mhe. Stella Ikupa(wa pili kushoto) alipotembelea Ofisi za CCM Wilaya, wakati wa ziara yake ya kikazi wilayani humo, Februari 27, 2019.
Baadhi ya viongozi na watendaji wa serikali pamoja na watu wenye ulemavu wilayani Busega wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia walemavu, Mhe. Stella Ikupa, wakati alipotembelea Kitalu nyumba katika ziara yake wilayani humo Februari 27, 2019.

0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!