Wananchi wa Kata ya Lamadi Wilayani Busega mkoani
Simiyu wamepiga kura za siri kwa lengo la kubaini watuhumiwa wa mauaji ya
watoto yaliyotokea hivi karibuni wilayani humo.
Wakizungumza
katika zoezi hilo lililofanyika Februari 14, 2019 katika Kitongoji cha Kisesa Kijiji cha Lamadi
wananchi hao wamesema kuwa wamelipokea vizuri
zoezi hilo na kubainisha kuwa kura hizo zitasaidia Vyombo vya Dola katika
kufanya uchunguzi na kuwabaini wauaji wa watoto wilayani humo
“Zoezi hili nimelipokea vizuri na nina imani
litatusaidia kuwapata wauaji wa watoto wetu na naishukuru Serikali kuona haja
ya kuwashirikisha wananchi maana mauaji haya ya watoto yametusikitisha sana
wakazi wa Lamadi” alisema Modesta Andrea mkazi wa Lamadi
“ Tukio hili la kupiga kura za siri mimi naona ni
zuri kwa sababu naamini kuna baadhi ya wananchi wanaweza wakawa wanafahamu watu
waliofanya mauaji ya watoto na kama ikitokea kuna watu wakaandikwa labda kwa
sababu ya fitina tunaamini vyombo vyetu vya dola vitachuja na kuchunguza na
mwishowe wauaji watabainika tu; tunaomba wakibainika sheria ifuate mkondo wake”
alisema Elisha Daniel mkazi wa Lamadi.
Akizungumza na wananchi wa Lamadi mara baada ya zoezi
hilo kukamilika, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka amesema kufanyika
kwa zoezi hilo hatua ya kwanza ya uchunguzi wa mauaji ya watoto wilayani humo,
huku akiwahakikishia wananchi kura walizopiga zitahesabiwa na vyombo vya dola
mkoani humo.
“Kupiga kura za siri si kwamba tumeshindwa kufanya
upelelezi, hii ni hatua ya kwanza ya sisi kufanya uchunguzi wetu, kura hizi
zitahesabiwa na vyombo vya dola mkoani Simiyu ambavyo ni Usalama wa Taifa,
Uhamiaji, Jeshi la Magereza, Jeshi la Wananchi JWTZ (Mkoa wa Simiyu), Jeshi la
Zimamoto, Jeshi la Polisi na TAKUKURU na baadaye taarifa itatolewa.
Aidha, Mtaka amesema wajibu wa kwanza wa Serikali ni
kulinda watu wake kuhakikisha wananchi wanaishi kwa amani ili waweze kufanya
vema shughuli za maendeleo.
Sambamba na hilo Mtaka amesema Serikali Mkoani
Simiyu itahakikisha inayafanyia kazi masuala mbalimbali yaliyosemwa na wananchi
katika mkutano huo ikiwa ni pamoja na malalamiko dhidi ya utendaji wa baadhi ya
viongozi na watendaji wa Serikali na
kubainisha kuwa hatua stahiki
zitachukuliwa dhidi ya wale wote watakaobainika kwenda kinyume katika
kuwatumikia wananchi.
“Niwahakikishie kuwa Serikali itayafanyia kazi yote
yaliyosemwa na wananchi katika Mkutano wa hadhara uliofanyika hapa Lamadi, kama
kuna wakubadilishwa watabadilishwa, wa kuwajibishwa watawajibishwa,
wakuhamishwa watahamishwa naomba mniamini” alisisitiza Mtaka.
Kwa upande wake Mbunge wa Busega, Dkt. Raphael
Chegeni ametoa pole kwa wazazi wote waliopoteza watoto wao katika mauaji ya
watoto na kuahidi kutoa rambirambi shilingi 500,000/= kwa kila familia ilikutwa
na msiba huku akilaani vikali vitendo vya mauaji ya kinyama ambayo yamekatisha
ndoto za watoto hao.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Busega, Mhe. Tano Mwera
amewashukuru wananchi wa Lamadi kwa namna
walivyojitokeza katika zoezi la kupiga kura za siri na kwa namna walvyolifanya
kwa amani na utulivu.
MWISHO
Baadhi ya wananchi wa
Lamadi wakiweka karatasi zao za kura za siri zilizopigwa katika zoezi maalum la
wananchi wa Lamadi kupiga kura za siri
lililofanyika katika Kitongoji cha Kisesa,
kwa ajili ya kubaini watuhumiwa
wa mauaji ya watoto yaliyotokea hivi karibuni wilayani humo.
Bi.Modesta Andrea
kutoka kijiji cha Itongo Kata ya Lamadi wilayani Busega mkoani Simiyu akipiga kura ya siri katika zoezi maalum la kupiga
kura za siri lililowahusisha wananchi wa
Lamadi lililofanyika katika Kitongoji
cha Kisesa Februari 14, 2019 kwa ajili
ya kubaini watuhumiwa wa mauaji ya watoto yaliyotokea hivi karibuni wilayani
humo.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,
Mhe. Anthony Mtaka akizungumza na wananchi wa Lamadi wilayani Busega mara baada
ya kukamilika kwa zoaezi la wananchi kupiga kura za siri kubaini watuhumiwa wa
mauaji ya watoto yaliyotokea hivi karibuni wilayani humo, ambalo limefanyika
katika Kitongoji cha Kisesa Kijiji cha Lamadi Februari 14,2019.
Baadhi ya wananchi wa
Lamadi wilayani Busega wakiendelea kupiga kura za siri na wengine wakisubiri
kauli ya Serikali mara baada ya kupiga kura hizo zilizokuwa na lengo la kubaini
watuhumiwa wa maujai ya watoto yaliyotokea hivi karibuni wilayani Busega, zoezi
la kupiga kura limefanyika katika Kitongoji cha Kijiji cha Lamadi Februari
14,2019.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa
wa Simiyu, Mhe. Enock Yakobo akizungumza na wananchi wa Lamadi wilayani Busega
mara baada ya kukamilika kwa zoezi la
wananchi kupiga kura za siri kubaini watuhumiwa wa mauaji ya watoto yaliyotokea
hivi karibuni wilayani humo, ambalo limefanyika katika Kitongoji cha Kisesa
Kijiji cha Lamadi Februari 14,2019.
Kutoka kulia ni Mkuu wa
Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka, Mkuu wa Wilaya ya Busega, Mhe. Tano Mwera,
Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Dkt. Joseph Chilongani na Mbunge wa Busega, Dkt.
Raphael Chegeni wakiteta jambo katika mkutano maalum ambao wananchi wa Lamadi
wilayani Busega, wamepiga kura za siri kubaini watuhumiwa wa mauaji ya watoto
yaliyotokea hivi karibuni, zoezi ambalo limefanyika katika Kitongoji cha Kisesa
Kijiji cha Lamadi Februari 14,2019.
Mzee Fulile Msikule
akichangia hoja katika mkutano maalum ambao wananchi wa Lamadi wilayani Busega,
wamepiga kura za siri kubaini watuhumiwa wa mauaji ya watoto yaliyotokea hivi
karibuni, zoezi ambalo limefanyika katika Kitongoji cha Kisesa Kijiji cha
Lamadi Februari 14,2019.
Mzee Alfred Nanai
akichangia hoja katika mkutano maalum ambao wananchi wa Lamadi wilayani Busega,
wamepiga kura za siri kubaini watuhumiwa wa mauaji ya watoto yaliyotokea hivi
karibuni, zoezi ambalo limefanyika katika Kitongoji cha Kisesa Kijiji cha
Lamadi Februari 14,2019.
Mbunge wa Busega, Dkt.
Raphael Chegeni akizungumza na wananchi wa Lamadi wilayani Busega mara baada ya
kukamilika kwa zoezi la wananchi kupiga
kura za siri kubaini watuhumiwa wa mauaji ya watoto yaliyotokea hivi karibuni
wilayani humo, ambalo limefanyika katika Kitongoji cha Kisesa Kijiji cha Lamadi
Februari 14,2019.
0 comments:
Post a Comment