Thursday, April 7, 2016

BARAZA LA USHAURI LA WATUMIA HUDUMA ZA EWURA LAZINDULIWA RASMI MKOANI SIMIYU


Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony J.  Mtaka  jana amezindua  Kamati ya Mkoa ya Baraza la  Ushauri  la Watumiaji wa Huduma zinazodhibitiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishati (EWURA) ya mkoa huo.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony John Mtaka (wa pili kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Wadau wa Huduma za Nishati , Viongozi wa Serikali na Wajumbe wa Kamati ya Baraza la Ushauri la Watumia huduma za Nishati na Maji la Mkoa wa Simiyu iliyozinduliwa Aprili 06,2016. ( wa kwanza kulia ) ni Katibu Tawala Mkoa, Bibi Mwamvua A. Jilumbi. Picha na Stella Kalinga

Akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Baraza hilo na wadau walioshiriki katika hafla ya uzinduzi , iliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mtaka alisema kamati ya baraza hilo inapaswa kuhakikisha inakuwa mstari wa mbele katika kutetea maslahi ya watumiaji wa huduma za nishati na maji, hasa upatikanaji  na uboreshaji  ili huduma hizo ziendane na thamani ya fedha wanazotoa watumiaji.

Mtaka alisema wajumbe wa kamati ya baraza la ushauri la watumia huduma za EWURA, wanao wajibu wa kuelimisha na kusambaza taarifa sahihi kwa watumiaji wa huduma za nishati na maji ili wajue masuala yanayowahusu hususani haki na wajibu wao.
“Mwenyekiti kamati yako itoe taarifa za mara kwa mara kwa watumiaji wa huduma za nishati na maji hasa yanapotokea mabadiliko kama kupanda au kushuka kwa bei ya maji , mafuta na umeme, kukatika kwa maji au umeme na taarifa nyingine muhimu kwa watumiaji wa huduma hizi ili wawe na ufahamu wa kutosha”, alisema Mtaka.

 Aliahidi kuwa Serikali ya Mkoa na vyombo vyake itashirikiana na Kamati ya baraza hili la Mkoa katika kuwajengea mazingira mazuri ya kufanya kazi ikiwa ni pamoja na kutoa ushirikiano na kuhakikisha malengo ya kuanzishwa kwake yanafanikiwa.

Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa aliwataka wafanyabiashara wa mafuta kuwashushia bei wananchi pale inapotokea bei za bidhaa hiyo kupungua katika soko badala ya kuendelea kuwaumiza kwa kisingizio cha kutopunguza bei kwa kuwa walichukua mzigo wakati bei ikiwa juu.


Kamati ya Mkoa ya Baraza la Ushauri la Watumia huduma zinazodhibitiwa na EWURA Mkoa wa Simiyu inaundwa na wajumbe watano: Suzan Sabuni (Mwenyekiti), Kubagwa Madabila(Katibu), Kulwa Mtebe (Mtunza Hazina), Magreth Kayanda (Mjumbe) na Martha Zongo (Mjumbe).

0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!