Wizara
ya Katiba na Sheria, imeandaa utaratibu wa kutumia wasuluhishi na watatuzi wa
migogoro ngazi ya vijiji na mitaa kote nchini kabla ya
wananchi kufikisha mashauri yao mahakamani.
Hayo
yamesemwa jana na Naibu Katibu Mkuu Wzara ya Katiba na Sheria Bw. Amon Mpanju
wakati akihitimisha mafunzo ya msaada wa kisheria kwa viongozi wanawake
,watumishi wanawake wasio viongozi na makundi mbalimbali ya wanawake wakiwemo
wajasiriamali ambayo yamelenga kuwajengea uelewa mpana wa masuala ya
kisheria.
"Hawa
watu tutawasajili rasmi tutawatambua ili watusaidie kutatua migogoro kwenye
familia, migogoro ya ardhi, ugomvi na kadhalika, lengo hasa ni kuwa na mfumo
unaoweza kumfikia mwananchi kutatua migogoro pasipo na ulazima wa kwenda
mahakamani ambako kimsingi wananchi wamekuwa wakipoteza muda na rasilimali
nyingi," alisema Mpanju.
Aidha,
Mpanju amesema lengo la Serikali ya awamu ya tano ni kuhakikisha wananchi
hususani wale wa pembezoni na wasio na uwezo wa kumudu gharama za kutafuta
mawakili wa kusimamia mashauri yao wanapata huduma za kisheria, ambapo amesema
kupitia Sheria namba 1 ya Huduma za msaada wa kisheria ya mwaka 2017 Wizara ya
Katiba na Sheria imesajili Taasisi na watoa huduma za kisheria kupitia kwa
wasaidizi wa kisheria.
Awali
akizungumza kabla ya kumkaribisha Naibu Katibu Mkuu, Mkuu wa mkoa wa Simiyu,
Mhe. Anthony Mtaka amesema wizara ya katiba na sheria imekuwa
msaada kwa utoaji elimu ya sheria mkoani Simiyu na kuabinisha kuwa
mafunzo hayo yatawasaidia washiriki kujua namba ya kushughulikia masuala na
changamoto mbalimbali katika jamii.
Katika
hatua nyingine Mtaka ameeleza kuwa mkoa wa Simiyu umepanga kutumia mabweni ya
Shule za sekondari za Serikali kuwahifadhi washukiwa wa maambukizi ya Virusi
vya Corona ambapo amewatoa hofu wakazi wa Simiyu kuwa kabla ya shule
kufunguliwa mabweni yatakayotumika kwa kazi hiyo yatapuliziwa dawa endapo
itabainika yalihifadhi watu wenye maambukizi.
Sambamba
na hilo Mtaka ametoa ofa kwa walimu wa Mkoa wa Simiyu watakaokuja na ubunifu
ambao utawasaidia wanafunzi kujisomea wakiwa nyumbani katika kipindi hiki
ambacho shule zimefungwa kwa ajili ya tahadhari ya maambukizi ya virusi vya
Corona.
Wawezeshaji
wa mafunzo ya msaada wa kisheria wamesema, "mafunzo haya yamewasaidia sana
watumishi na viongozi mbalimbali wanawake walioshiriki,walikuwa hawajui vitu
vingi mfano, wengine walikuwa hawajui masuala ya sheria zandoa,mirathi na
wengine walikuwa hawajui wanapata wapi huduma za msaada wa kisheria; tunaomba
mafunzo kama haya yawe yanatolewa mara kwa mara kuwasaidia wananchi kujua
sheria na haki zao” mwezeshaji wa. mafunzo Bibi. Eddah Maliki.
"Tumekutana
na makundi mbalimbali ya wanawake katika mada za haki za binadamu, ukatili wa kijinsia, sheria
ya ndoa, mirathi, sheria ya huduma za msaada wa kisheria; tumebainia kuna
uhitaji wa elimuya masuala ya kisheria na ukatili wa kijinsia ni changamoto
kubwa katika jamii, washiriki wameomba wanaume pia wapewe mafunzo haya ili washirikiane
kuondoa ukatili wa kijinsia katika jamii," alisema George Mollel Wakili
kutoka Wizaraya Katiba na Sheria.
Naye
mmojawa washiriki wa mafunzo haya, Angelina Daudi kutoka Ofisi ya. Dawati la
Jinsia, Jeshi la Polisi wilaya ya Itilima amesema mafunzo haya yamemuongezea
uelewa katika masuala yanayohusu haki za wanawake,mirathi na sheria ya ndoa na
elimu aliyoipata itamsaidia kuboresha kazi yake na kuomba mafunzo haya yawe
yanatolewa mara kwa mara..
MWISHO
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akizungumza na baadhi ya viongozi wanawake na makundi mbalimbali ya wanawake jana mkoani Simiyu wakati wa kuhitimisha mafunzo ya huduma za msaada wa kisheria yaliyofanyika Mjini Bariadi kwa muda wa siku tano.
Mkuu wa Shule ya Msingi Ibulyu, Mwl. Adela Mkusi akizungumzia manufaa ya mafunzo ya humdma za kisheria yaliyotolewa kwa baadhi ya wanawake viongozi, watumishi wanawake na wajasiriamali mkoani Simiyu, wakati wa kuhitimisha mafunzo hayo yaliyofanyika kwa muda wa siku tano Mjini Bariadi.
Baadhi ya wanawake
viongozi na wanawake wa makundi mbalimbali wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu
Wizara ya Katiba na Sheria, Bw. Amon Mpanju (hayupo pichani) wakati
akihitimisha mafunzo ya huduma za msaada
wa kisheria kwa kundi hilo, yaliyofanyika Mjini Bariadi kwa muda wa siku tano.
Wakili kutoka Wizara ya Katiba na Sheria. George
Mollel akitoa mafunzo kwa baadhi ya viongozi wanawake na
makundi mbalimbali ya wanawake jana mkoani Simiyu wakati wa kuhitimisha mafunzo
ya huduma za msaada wa kisheria yaliyofanyika Mjini Bariadi kwa muda wa siku
tano.
Baadhi ya wanawake
viongozi na wanawake wa makundi mbalimbali wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu
Wizara ya Katiba na Sheria, Bw. Amon Mpanju (hayupo pichani) wakati
akihitimisha mafunzo ya huduma za msaada
wa kisheria kwa kundi hilo, yaliyofanyika Mjini Bariadi kwa muda wa siku tano.
0 comments:
Post a Comment