Mkuu wa
Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka amewataka Maafisa Michezo na Walimu wa
Michezo mkoani humo kuwasaidia Vijana wa Kitanzania kutoka kwenye nadharia ya
kufikiri kuwa michezo ni afya, urafiki na burudani tu ili waanze kufikiri michezo katika
mtazamo wa biashara na ajira.
Mtaka
ameyasema hayo wakati alipokuwa akifunga semina ya kuwajengea uwezo Maafisa Michezo, Viongozi wa
Vyama na Vilabu vya Michezo, makocha na walimu wa michezo shuleni, kwa lengo la kuchochea maendeleo ya Michezo Mkoani
Simiyu, ambayo yametolewa na Dkt. Angela Daalmann na Anja Henke
ambao ni Wataalam wa Michezo kutoka
Jimbo la Hannover Nchini Ujerumani.
“Tumeleta mafunzo haya tukiamini
kuwa Maafisa Michezo wote ndani ya Mkoa wa Simiyu watakuwa na msaada mkubwa
kwenye kuwaandaa vijana wa Kitanzania kutoka kwenye nadharia ya kusema michezo
ni afya, michezo ni upendo, michezo ni burudani ; nataka Afisa Michezo akienda
kwenye implementation(utekelezaji) vijana wa mkoa wa Simiyu waanze kujenga vichwani
mwao kuwa michezo ni ajira, michezo ni biashara” alisema Mtaka.
“Katika Dunia ya leo michezo ni
biashara kubwa na ni ajira kubwa ya dunia ndiyo maana hapa mmefundishwa kuhusu miradi,
hili suala la michezo ni burudani, michezo ni afya, michezo ni urafiki na upendo libaki kama
jambo la pili” alisisitiza
Ameongeza kuwa Maafisa Michezo
pamoja na walimu wa michezo Mkoani Simiyu kupitia michezo ya UMITASHUMTA na UMISETA wanapaswa kuwatambua watoto/vijana
wenye vipaji na kuwaandaa kibiashara ili wajue kuwa vipaji vyao ni ajira zao za
baadaye.
Aidha, amesema Serikali mkoani
humo imedhamiria kutangaza utalii na kukuza uchumi kupitia sanaa, michezo na
utamaduni na akabainisha kuwa Mkoa umeanza kutekeleza hilo kupitia uanzishwaji wa Tamasha kubwa la michezo na
utamaduni maarufu kama “Simiyu Festival” ambalo linafanyika kila mwaka na kwa
mwaka 2018 litafanyika mapema mwezi Julai.
Naye Mtalaam wa Michezo kutoka Jimbo la Hannover Dkt. Angela
Daalmann amesema kwamba wamehamasika kutoa mafunzo kwa maafisa, viongozi na
walimu wa michezo mkoani Simiyu ikiwa ni mara ya pili sasa, kutokana na utayari
wa viongozi na watalaam mkoani humo katika kuleta mapinduzi kwenye sekta ya michezo.
Afisa Michezo wa Mkoa wa Simiyu,
Bw.Emmanuel Athanas amesema mafunzo hayo yataamsha ari na hamasa ya michezo kwa
Maafisa Michezo na Walimu wa Michezo mkoani humo na kuwasaidia katika kuibua
miradi mbalimbali itakayohusianishwa na michezo (sports projects) sambamba na kuwatafuta wadau mbalimbali kuwezesha
miradi hiyo.
Naye Afisa Michezo wilaya ya
Meatu, Bw. Hassan Sengulo amesema mafunzo hayo yamewasaidia kutambua namna
sahihi ya kupata fedha kwa ajili ya uendeshaji wa michezo, hivyo watayatumia kuwaelimisha Walimu wa
Michezo na Viongozi wa Vyama na Vilabu vya Michezo namna ya kutatua changamoto ya ukosefu
wa fedha za kuendeshea michezo.
Semina hii ilijumuisha jumla ya
washiriki 27 kutoka Halmashauri zote sita za Mkoa wa Simiyu na baadaye
ikafuatiwa na Bonanza la michezo kwa wanafunzi wa baadhi ya shule za msingi
kushiriki mchezo wa riadha, ambapo
wanafunzi walipata nafasi ya kukimbia mbio za mita 100, mita 400 na mita 1500
katika Uwanja wa Shule ya Msingi Somanda Mjini Bariadi.
MWISHO
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,
Mhe.Anthony Mtaka akizungumza katika semina ya Maafisa Michezo, Baadhi ya walimu wa michezo
na Viongozi wa Vyama vya Michezo mkoani humo iliyofanyika Machi
06, 2018 Mjini Bariadi.
Mtalaam wa Michezo kutoka Jimbo la Hannover nchini Ujerumani Dkt.
Angela Daalmann akizungumza na Maafisa Michezo, Viongozi wa Vyama na Vilabu
vya Michezo, makocha na walimu wa michezo shuleni (hawapo pichani) mkoani Simiyu katika Semina
iliyofanyika Machi 06, 2018 Mjini Bariadi.
Baadhi ya Maafisa Michezo, Viongozi wa Vyama na
Vilabu vya Michezo, makocha na walimu wa michezo shuleni mkoani Simiyu
wakimsikiliza Mtalaam
wa Michezo kutoka Jimbo la Hannover nchini Ujerumani Dkt. Angela Daalmann
katika Semina iliyofanyika Machi 06, 2018 Mjini Bariadi.
Baadhi ya Maafisa
Michezo, Viongozi wa Vyama na Vilabu vya Michezo, makocha na walimu wa michezo
shuleni mkoani Simiyu wakimsikiliza Mtalaam wa Michezo kutoka Jimbo la Hannover nchini
Ujerumani Dkt. Angela Daalmann katika Semina iliyofanyika Machi
06, 2018 Mjini Bariadi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,
Mhe.Anthony Mtaka (kushoto) akiteta jambo na Mtalaam
wa Michezo kutoka Jimbo la Hannover nchini Ujerumani Dkt. Angela Daalmann
katika Semina ya Maafisa Michezo, Viongozi wa Vyama na Vilabu vya Michezo, makocha
na walimu wa michezo shuleni mkoani Simiyu iliyofanyika Machi 06, 2018 Mjini
Bariadi.
Baadhi ya Wanafunzi wa
kike kutoka Shule ya Msingi Somanda A na Somanda B wakishiriki mbio za mita 100 katika Bonanza la Michezo
lililofanyika katika viwanja vya shule hiyo Machi 06, 2018 Mjini Bariadi.
Baadhi ya Wanafunzi wa
kiume kutoka Shule ya Msingi Somanda A na Somanda B wakishiriki mbio za mita
400 katika Bonanza la Michezo lililofanyika katika viwanja vya shule hiyo Machi
06, 2018 Mjini Bariadi.
Baadhi ya wanafunzi wa
Shule ya Msingi Somanda B wakitoa burudani ya ngoma ya asili ya kabila la
Wasukuma katika Bonanza la Michezo lililofanyika katika viwanja vya shule hiyo
Machi 06, 2018 Mjini Bariadi.
Mkuu
wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka(wa tatu kulia mbele) akiwa katika picha ya
pamoja washiriki wa Semina kuwajengea uwezo Maafisa Michezo, Viongozi wa Vyama
na Vilabu vya Michezo, makocha na walimu wa michezo shuleni mkoani humo pamoja
na Dkt. Angela Daalmann na Anja Henke ambao ni Wataalam wa Michezo kutoka Jimbo la Hannover
Nchini Ujerumani.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,
Mhe.Anthony Mtaka(wa pili kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Wataalam wa
Michezo kutoka Jimbo la Hannover nchini Ujerumani Dkt. Angela Daalmann(wa
pili kushoto) na Anja Henke(kulia) mara baada ya kukamilika kwa semina kwa
Viongozi, Maafisa na walimu wa Michezo mkoani humo (kushoto ) Mkuu wa Wilaya ya
Busega, Mhe.Tano Mwera.
Afisa Michezo wa Mkoa wa Simiyu, Bw.Emmanuel Athanas akifafanua jambo katika semina
ya kuwajengea uwezo Maafisa Michezo,
Viongozi wa Vyama na Vilabu vya Michezo, makocha na walimu wa michezo mkoani
humo iliyofanyika Machi 06, 2018 Mjini Bariadi.
0 comments:
Post a Comment