Mkoa wa Simiyu na Mamlaka ya Maendeleo
ya Biashara Tanzania(TanTrade) wamesema watashirikiana kwa pamoja kuandaa Maonesho
ya Kilimo NaneNane mwaka 2018 ambayo Kitaifa yatafanyika Mkoa wa Simiyu.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa
Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya
Biashara Tanzania (TanTrade) Bw. Edwin Rutageruka katika Mkutano wao na
Waandishi wa Habari uliofanyika katika makao makuu ya Mamlaka hiyo Jijini Dar es
Salaam.
Akiongea na waandishi wa habari Mkuu wa
Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema kuwa Mkoa utatoa dira ya kuyafanya
Maonesho ya Kilimo NaneNane kuwa ni Maonesho ya Kilimo Biashara ili Watanzania
wapate fursa ya kuona teknolojia mbalimbali kwenye eneo la kilimo, mifugo na
uvuvi.
“Sisi kama Mkoa tungehitaji tutoe dira
ya kuyafanya maonesho ya Wakulima NaneNane yawe ni maonesho ya Kilimo Biashara,
mahali ambapo Watanzania watapata Fursa ya kuona teknolojia mbalimbali kwenye
eneo la Kilimo, eneo la mifugo, eneo la uvuvi na yote haya yabebebwe na dhana
ya Kilimo Biashara” alisema Mtaka
“Matarajio yetu kama mkoa kwa
kushirikiana na TanTrade ni kuona kwamba tunaingiza Maonesho ya Kilimo NaneNane
kuwa tukio ambalo litawakaribisha watu wenye teknolojia mbalimbali Kitaifa na
Kimataifa kwenye kuwezesha mageuzi ya kilimo,uvuvi na ufugaji wa nchi kwa
kuonesha ni kwa namna gani wanaweza kumfikia mkulima, mvuvi na mfugaji kwenye
teknolojia ya kisasa ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi ili Maonesho ya Kilimo
NaneNane yawekwe kwenye ramani ya dunia” alisisitiza Mtaka
Aidha, Mtaka ameziomba Balozi za
Tanzania katika nchi mbalimbali kuyatangaza Maonesho haya kwa kuyatumia kukaribisha
makampuni yenye teknolojia kuja kuonesha mkoani Simiyu na akatumia fursa hiyo
kuwakaribisha wawekezaji kwa makundi yote kutoka ndani na nje ya nchi kuja
kuwekeza katika eneo litakalofanyika Maonesho ya Kilimo Biashara ili uwekezaji
huo uendane na viwango vya Kimataifa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa
Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) Bw. Edwin Rutageruka ameeleza
kuwa Mkoa wa Simiyu na TanTrade wamekubaliana kuwa na maonesho endelevu ya
Kisekta katika Mkoa wa Simiyu
Rutageruka ameongeza kuwa TanTrade ni
taasisi pekee iliyopewa jukumu la kusimamia masuala ya Maonesho ndani na nje ya
nchi kisheria, hivyo kutokana na uzoefu wa uandaaji wa Maonesho mbalimbali, kwa mwaka 2018 Maonesho ya Kilimo Biashara
yatakuwa ni Maonesho bora kwasababu watawaandaa washiriki wote Kisekta, kuweka miundo mbinu ya kisasa na kuyafanya
Maonesho haya kuwa ya Kimataifa.
“Mkoa wa Simiyu una kiu ya kuona Maonesho
ya Kilimo Biashara yanakuwa ya
kisasa kama ilivyo Maonesho ya Biashara
ya Kimataifa ya Dar es Salaam ambayo kwa Afrika Mashariki ndiyo Maonesho
yanayoongoza kwa ubora na Maonesho haya ya Kilimo tutayafikisha huko” aliongeza
Bw Rutageruka.
Hivi karibu Serikali imetangaza Kanda
Mpya ya Maonesho ya Kilimo na Sherehe za Wakulima NaneNane inayojumuisha mikoa ya Simiyu, Mara na
Shinyanga ambayo inatambulika kama Kanda ya Ziwa Mashariki na Maonesho hayo kwa
kanda hiyo yatakuwa yanafanyika Mkoani
Simiyu.
0 comments:
Post a Comment