Thursday, April 12, 2018

MKURUGENZI TANTRADE ATOA WITO KWA MAKAMPUNI, WAKULIMA, WAFANYABIASHARA KUJIANDAA NA NANENANE MWAKA 2018 KANDA YA ZIWA MASHARIKI


Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (TanTrade ) Edwin Rutageruka ametoa wito kwa wakulima,wafanyabiashara  na makampuni madogo Nchini kujiandaa  na kushiriki  maonesho ya Kilimo na Sikukuu ya Wakulima NaneNane ya Kanda ya Ziwa Mashariki  ili kujifunza teknolojia mpya  kutoka katika makampuni ya nje.

Maonesho hayo ambayo mwaka 2018 yanatarajia kufanyika kitaifa Mkoani Simiyu yameelezwa kuwa yatakuwa ya kipekee ikilinganishwa na miaka mingine   huku yakitoa fursa zaidi kwa wafanyabiashara na  makampuni  madogo kujitokeza kwa wingi kushiriki.

 Akizungumza  leo Aprili 12  katika kikao cha maandalizi  ya Nane Nane Kitaifa yanayotarajiwa kufanyika  Mkoani Simiyu, Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade Edwin Rutageruka amesema kuwa taasisi yake iko tayari kutoa ushirikiano wa dhati  kwa uongozi wa Mkoa wa Simiyu ili kuhakikisha wanayafanya maonesho hayo kuwa ya kipekee.

 Amesema ni vema makampuni madogo, wakulima na wafanyabiashara wakajitokeza kushiriki maonesho hayo kwani watapata fursa ya kujifunza Teknolojia  mpya kutoka nchi za nje ambazo zitashiriki maonesho hayo.

“Ni vema Wafanyabiashara, wakulima na makampuni madogo yakajitokeza kushiriki maonesho hayo kwani tumejipanga vizuri, tumetenga maeneo mazuri na tutapanga kulingana na sekta mbalimbali ”alisema

Ameongeza kuwa katika kuyatangaza maonesho hayo ya Nane Nane ya mwaka huu 2018 , TanTrade itaandaa dawati maalum la kuutangaza rasmi Mkoa wa Simiyu na fursa zilizopo ili Watanzania na Wawekezaji wajitokeze kwa wingi kuwekeza.

Aidha,  Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka amesema uwepo wa Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Ziwa Mashariki  yatakayofanyika Mkoani humo, kwa kushirikiana na  Mikoa ya Mara na Shinyanga ambayo kwa pamoja inaunda Kanda hiyo, yatasaidia wakulima kujifunza kwa washiriki kutoka maeneo mbalimbali na hatimaye kuongeza thamani ya mazao yao.

Mtaka ameeleza kuwa mbali na Uwanja wa Maonesho kutumika kwa ajili ya Maonesho ya Sikukuu ya Wakulima Nane Nane, Uwanja huo utatumika katika shughuli mbalimbali  za kiuchumi ambazo zitawanufaisha kiuchumi wananchi na Taifa kwa ujumla.

Akizungumza kwa niaba ya Wafanyabiashara wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Bahini Masunga amesema  kuwepo kwa Maonesho ya Nane Nane kutawasaidia Wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla  kutambua fursa mbalimbali pamoja na kujiongezea ujuzi wa namna ya kuongeza thamani katika bidhaa zao.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (TanTrade ) Edwin Rutageruka (katikati) akizungumza na baadhi ya viongozi wa Mkoa wa Simiyu katika kikao kilichofanyika Mjini Bariadi kujadili juu ya maandalizi ya Maonesho ya Kilimo na Sikukuu ya Wakulima Nane Nane Kitaifa mwaka 2018 ambayo itafanyika Kanda ya Ziwa Mashariki Mkoani Simiyu.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akisisitiza jambo  katika kikao kilichofanyika Mjini Bariadi kati ya Viongozi wa Mkoa huo  na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (TanTrade ) Bw. Edwin Rutageruka kujadili juu ya maandalizi ya Maonesho ya Kilimo na Sikukuu ya Wakulima Nane Nane Kitaifa mwaka 2018 , ambayo itafanyika Kanda ya Ziwa Mashariki Mkoani humo.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (TanTrade ) Bw. Edwin Rutageruka(wa nne kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi na watalam wa Mkoa wa Simiyu, baada ya kikao kilichofanyika Mjini Bariadi kujadili maandalizi ya Maonesho ya Kilimo na Sikukuu ya Wakulima Nane Nane Kitaifa mwaka 2018,  ambayo itafanyika Kanda ya Ziwa Mashariki Mkoani Simiyu.

0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!