Tuesday, April 24, 2018

SIMIYU KUANZA KUWAANDAA WANAFUNZI WA DARASA LA VII, KIDATO CHA NNE WA MWAKA 2019 SASAMkoa wa Simiyu umejipanga kuanza kuwaandaa Wanafunzi wa Darasa la Saba na Kidato cha Nne wa mwaka 2019 kuanzia mwezi Agosti, mwaka huu 2018 ili kufikia malengo ya kuongeza ufaulu katika mitihani yote ya Taifa.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Anthony Mtaka katika Hafla fupi ya kuwapongeza walimu wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi kwa kuongeza ufaulu  kwa Shule za Msingi na Sekondari kipindi cha miaka miwili mfululizo, iliyofanyika Ukumbi wa Bariadi Alliance Mjini hapa.

Mtaka amesema kutakuwa na mitihani kwa wanafunzi wa darasa la sita na kidato cha tatu mwezi Agosti 2018  ili kupata wanafunzi wenye ufaulu mzuri watakaounda darasa maalumu la darasa la saba na kidato cha nne mwaka 2019 ( special class).

"Tunaanza maandalizi ya darasa la saba na kidato cha nne wa mwakani kuanzia mwezi Agosti mwaka huu, ili tuchuje bila kupendelea mtihani ni chujio zuri, matokeo hayo yatabandikwa na wazazi wote wataona" alisema Mtaka.

Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amesema baada ya kumaliza kambi ya kitaaluma kwa kidato cha sita mwezi huu, Mkoa umepanga kufanya kambi za kitaaluma kwa kidato cha nne na darasa la saba ambazo zitafunguliwa rasmi tarehe 06 Juni, 2018.

Wakati huo huo amesema Serikali inaendelea kuwajengea uwezo walimu mahiri na makini ili waweze kuwasaidia wanafunzi wa madarasa maalumu kufanya vizuri lengo likiwa ni kuongeza ufaulu kwa shule za msingi na kufuta daraja la nne na sifuri  kwa shule za sekondari.

Kuhusu ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Mkoa, Mtaka amesema Mkoa utajenga shule ya Mkoa Mjini Bariadi (Makao Makuu ya mkoa) ambayo itatambulika kama Shule ya Sekondari Simiyu na itakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 1000 huku ikiwa na miundombinu mingine muhimu kama maabara, vyumba vya kompyuta na mkongo wa Taifa.

Pia amesema pamoja na kujenga Shule hiyo ya Mkoa, Serikali imedhamiria kwa kushirikiana na wananchi kujenga shule mbili maalumu kwa ajili ya wasichana na wavulana (Simiyu Girls na Simiyu Boy's) ambazo zitabeba taswira ya Mkoa na kutambulisha Mkoa huo tofauti na ilivyo sasa ambapo shule nyingi zilizopo katika Makao makuu ya Mkoa ni zile za Kata.

Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa amewaruhusu walimu mkoani humo kufundisha masomo ya ziada (tuition) hususani wakati wa likizo na mapumziko ili wanafunzi waendelee kujifunza badala ya kusubiri kufundishwa darasani pekee.

Akizungumza kwa niaba ya walimu wa Halmashauri ya Mji, Mwl. Travel Ndimangwa kutoka Shule ya Msingi Somanda A amepongeza utaratibu wa kuwaandaa wanafunzi wa madarasa ya mitihani pamoja na kuruhusiwa kuwafundisha wanafunzi masomo ya ziada  mambo ambayo amesema yatachangia kuongeza ufaulu kwa wanafunzi.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Mhe. Robert Lweyo ametoa wito kwa walimu wa Halmashauri hiyo kufanya kazi kwa bidii na weledi ili kupandisha ufaulu ambapo mwaka 2017  ilishika nafasi ya 22 Kitaifa katika mtihani wa Kidato cha Nne kutoka nafasi ya 44 mwaka 2016.


Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akizungumza na walimu wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi katika Hafla fupi ya kuwapongeza walimu hao kwa kuongeza ufaulu, iliyofanyika Mjini Bariadi.


Baadhi  ya Walimu wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka (hayupo pichani) katika Hafla fupi ya kuwapongeza walimu hao kwa kuongeza ufaulu, iliyofanyika Mjini Bariadi.


Baadhi  ya Walimu wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka (hayupo pichani) katika Hafla fupi ya kuwapongeza walimu hao kwa kuongeza ufaulu, iliyofanyika Mjini Bariadi.Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Mhe.Robert Lweyo akizungumza na walimu wa Halmashauri hiyo katika Hafla fupi ya kuwapongeza kwa kuongeza ufaulu, iliyofanyika Mjini Bariadi.Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe.Festo Kiswaga akimkabidhi cheti mmoja wa walimu ambao wanafunzi wao walifanya vizuri katika Mtihani wa Darasa la Saba mwaka 2017, katika Hafla fupi ya kuwapongeza walimu hao kwa kuongeza ufaulu, iliyofanyika Mjini Bariadi.


Mwalimu Aron Kihunsi kutoka Shule ya Sekondari Bariadi, akipokea cheti  cha pongezi kwa kufanya vizuri katika somo la Kiingereza katika Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2017, kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe.Festo Kiswaga, katika Hafla fupi ya kuwapongeza walimu hao kwa kuongeza ufaulu, iliyofanyika Mjini Bariadi.

0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!