Wednesday, August 5, 2020

WAKULIMA CHAGUENI VIONGOZI WA VYAMA VYA USHIRIKA WAADILIFU: WAZIRI KAIRUKI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu uwekezaji, Mhe. Angela Kairuki ametoa wito kwa wakulima (wanaushirika) kuchagua viongozi waadilifu wanaojali maslahi ya wote badala ya kuangalia maslahi binafsi. 

Mhe. Kairuki amesema hayo Agosti 03, 2020 wakati akitoa ujumbe maalum wa ushirika kwa katika Maonesho ya Nanenane Kitaifa 2020 yanayoendelea katika Viwanja vya Nyakabindi Bariadi mkoani Simiyu akimwakilisha Waziri Mkuu wa Jmahuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa.

 

Aidha, Waziri Kairuki ameipongeza wizara ya kilimo kwa uamuzi wa kuvifuta vyama vya ushirika 2,539 ambavyo vilikuwa na utendaji mbovu uliosababisha kero kwa wanaushirika nchini hatua itakayowawezesha  wanaushirika ambao ni wakulima, wavuvi na wafugaji kunufaika na kazi zao ndani ya ushirika .

“Ninawapongeza sana Wizara kwa hatua mliyochukua yakuvifuta vyama vya ushirika 2,539 kwasababu ya  kutofanya kazi iliyokusudiwa.” Alisema Waziri Kairuki.

Waziri Kairuki alisema katika kipindi cha 2018/2019 jumla ya viwanda 75 vimeanzishwa na vyama vya ushirika vinavyochakata alizeti, chikichi, kutengeneza samani za majumbani, kuchakata pamba na mazao ya nafaka pamoja na usindikaji wa  maziwa.

“ Viwanda vinavyomilikiwa na vyama vya ushirika vimeongezeka kutoka viwanda 133 mwaka 2018 hadi kufikia viwanda 208 mwaka 2019” alisema Waziri Kairuki.

Katika hatua nyingine Waziri Kairuki ameiagiza Tume ya Maendeleo ya Ushirika kushirikiana na Wakala wa Serikali Mtandao (EGA) kuangalia namna bora ya kuweka mfumo shirikishi wa TEHAMA utakaoweza kuongeza uwazi katika usimamizi wa vyama vya ushirika hususan AMCOS.

Naye Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga amesema wizara yake itaendelea kuhakikisha wakulima, wavuvi na wafugaji nchini wananjiunga na vyama vya ushirika ambavyo vitawasaidia kupata nguvu ya kuweza kupata mitaji, masoko, pembejeo na huduma za ugani ili wakuze uzalishaji.

Maonesho ya Kilimo ya Nane nane Kitaifa yameingia siku ya tatu leo ambapo wananchi na wakulima toka mikoa ya Mara, Simiyu na Shinyanga wanaendelea kupata elimu kwenye mabanda na vipando vilivyoandaliwa.

Kauli mbiu ya Nane nane mwaka huu inasema“ Kwa Maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Chagua Viongozi Bora 2020”

MWISHO.

 Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu uwekezaji, Mhe. Angela Kairuki akiangalia mchele uliokobolew na kupangwa madaraja kutoka wilayani Maswa  wakati alipotembelea mabanda ya maonesho ya nanenane  Kitaifa Agosti 03, 2020 yanayofanyika Uwanja wa Nyakabindi wilayani Bariadi mkoani Simiyu

TAZAMA PICHA MBALIMBALI WAZIRI KAIRUKI ALIPOTEMBELA MABANDA MABALIMBALI YA MAONESHO YA NANENANE NYAKABIDHI BARIADI SIMIYU






0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!