Saturday, October 14, 2017

TIZEBA:GINNER ATAKAYEGOMA KUPELEKA PAMBA MBEGU KWENYE KIWANDA CHA QUTON HATANUNUA PAMBA MWAKANI

Waziri wa Kilimo Mhe.Dkt. Charles Tizeba amewataka wamiliki wa viwanda vya kuchambua pamba(ginners) kupeleka pamba mbegu kwenye kiwanda cha kuchakata(kutoa manyoya) mbegu za pamba cha Quton na akasema watakaogoma kupeleka hawatanunua pamba msimu ujao.

Waziri Tizeba ameyasema hayo jana alipotembelea kiwanda hicho katika Kata ya Kasoli wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu kwa lengo la kujionea hali ya uzalishaji wa mbegu ya pamba inavyoendelea.

Amesema suala la wenye viwanda vya kuchambua pamba(ginners) kupeleka pamba mbegu katika kiwanda cha kuchakata mbegu za pamba(kuondoa manyoya) siyo la hiari na walishapewa maelekezo, hivyo wanapaswa kupeleka pamba mbegu katika kiwanda cha Quton ili zitolewe manyoya na baadaye zipelekwe kwa wananchi.

“ Nimeambiwa watu wa Quton wanashindwa kufanya kazi kwa shift tatu kwa siku kwa sababu walio na mbegu kwenye viwanda vyao vya kuchambua pamba hawataki kuleta pamba hapa, wakati wanayo maelekezo na hii siyo hiari mbegu ikishatengwa na Bodi ya Pamba si yao” alisema Tizeba.

“Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba nakuagiza wapelekee ujumbe huu kwamba ginner atakayegoma kuleta pamba mbegu hapa Quton hanunui pamba mwaka kesho, wanapaswa walete mbegu zitolewe manyoya ziende kwa wananchi ili wapate mbegu bora, katika hili sitabembelezana na mtu” alisisitiza Tizeba.

Aidha, Mhe.Waziri amesema mahitaji ya mbegu ya pamba iliyotolewa manyoya kwa nchi nzima ni takribani tani 8000, hivyo ili kufikia kiwango hicho katika siku zilizobaki kuelekea msimu wa kilimo cha pamba, kiwanda cha Quton kinapaswa kufanya kazi saa 24 kwa kuwa uzalishaji wa sasa wa tani 60 hadi 65 kwa saa 16 kwa siku hautaweza kufikia lengo hilo.

Wakati huo huo Waziri Tizeba ametoa wito kwa wananchi Mkoani Simiyu kutopanda pamba sasa kwa kuhofia mvua kukatika mapema, badala yake wasubiri taarifa rasmi ya Mamlaka ya Hali ya Hewa juu ya hali ya mvua katika ukanda huo itakayotolewa muda mfupi ujao,ambayo baadaye itatumika kuwashauri wakati muafaka wa kupanda, japo alieleza kuwa taarifa ya jumla ya utabiri wa hali ya hewa inaonesha mvua itanyesha juu ya wastani.

Pia Mhe.Waziri amewahakikishia wananchi kuwa bei ya mbolea imeshuka, hivyo akawataka wataalam wa Kilimo kuwaelimisha wananchi juu ya bei elekezi ya mbolea kwa kila wilaya, ili wasiuziwe kwa bei kubwa na akasisitiza kuwa bei ya mbolea na mbegu mwaka 2018 itapungua zaidi kwa kuwa Serikali imefuta takribani kodi 80 katika kilimo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe.Festo Kiswaga amesema Mkoa wa Simiyu unazalisha pamba kwa wingi, ambapo katika msimu wa mwaka 2016/2017 umezalisha takribani asilimia  65 ya pamba ya nchi nzima, hivyo akaomba wananchi wa mkoa huo wasaidiwe kupewa mikopo ya zana bora za kilimo na pembejeo nyingine kupitia mfuko wa pembejeo ili kuongeza uzalishaji zaidi.

Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Quton Tanzania Limited Ndg. Pradyumansinh Chauhan amemuomba Waziri wa Kilimo kuhamasisha wananchi kutumia mbegu za pamba zilizotolewa manyoya ili kuongeza uzalishaji kwa kuwa hazishambuliwi kwa urahisi na magonjwa na zinapunguza kiasi cha mbegu kinachotumika shambani ambapo kilogramu sita tu hutumika kwa hekali wakati zenye manyoya hutumika hadi kilogramu 15.


Waziri wa Kilimo, Mhe.Dkt.Charles Tizeba (wa tatu kushoto) akisikiliza maelezo kutoka wa Meneja Uzalishaji wa Mbegu,Pheneas Chikaura(kulia) katika Kiwanda cha Kuzalisha mbegu za pamba cha Quton wakati wa ziara yake kiwandani hapo Wilayani Bariadi Mkoani Simiyu.
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe Festo Kiswaga(kulia) akiwasilisha taarifa ya Wilaya yake kwa Waziri wa Kilimo, Dkt.Charles Tizeba (wa tatu kushoto) wakati alipofanya ziara katika Wilaya hiyo Mkoani Simiyu.
Waziri wa Kilimo, Mhe.Charles Tizeba akikaribishwa na Mkurugenzi wa Quton Tanzania Limited Ndg.Pradyumansinh Chauhan, alipotembea Kiwanda cha kuzalisha Mbegu za Pamba cha Quton kilichopo kata ya kasoli Wilayani Bariadi Mkoani Simiyu.
Waziri wa Kilimo, Mhe.Dkt.Charles Tizeba(kushoto) akisalimiana na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Ndg.Donatus Weginah mara baada ya kuwasili Mjini Bariadi kwa ajili ya ziara ya siku moja Mkoani humo.
Waziri wa Kilimo, Mhe.Dkt.Charles Tizeba(kushoto) akisalimiana na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bariadi, Mhe.Juliana Mahongo mara baada ya kuwasili Mjini Bariadi kwa ajili ya ziara ya siku moja Mkoani Simiyu.
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Ndg.Donatus Weginah akitoa taarifa ya Mkoa kwa Waziri wa Kilimo, Dkt.Charles Tizeba (kulia) wakati alipofanya ziara katika Wilaya ya Bariadi Mkoani humo.
Baadhi ya Viongozi na Wataalam wa Kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi na Mkoa wa Simiyu wakimsikiliza Waziri wa Kilimo, Dkt.Charles Tizeba(hayupo pichani) wakati alipozungumza nao kabla ya kutembelea Kiwanda cha Kuchakata mbegu za pamba(zilizotolewa manyoya) cha Quton katika Kata ya Kasoli Mkoani Simiyu kujionea uzalishaji wa mbegu za pamba.
Mkurugenzi wa Kiwanda cha Kuchambua pamba cha Alliance Ginnery, Ndg. Boazi Ogola(wa pili kushoto) akimuongoza Waziri wa Kilimo, Dkt.Charles Tizeba (aliyeweka mkono kifuani) na baadhi ya Viongozi wa Wilaya ya Bariadi na Mkoa wa Simiyu kuelekea kuona kiwanda hicho wakati wa ziara ya Waziri huyo Mkoani Simiyu.
Waziri wa Kilimo, Mhe. Dkt.Charles Tizeba akionesha moja ya mashine iliyopo katika Kiwanda cha kuchambua pamba cha Alliance Ginnery na akataka maelezo juu ya mashine hiyo wakati ziara yake Wilayani Bariadi Mkoani Simiyu.
Waziri wa Kilimo, Mhe.Dkt.Charles Tizeba(wa pili kulia) na baadhi ya viongozi na wataalam wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi na Mkoa wa Simiyu wakielekea katika kiwanda cha kuzalisha mbegu za pamba zilizotolewa manyoya cha Quton wakati wa ziara yake katika kiwanda hicho Mkoani Simiyu.
Waziri wa Kilimo, Mhe.Dkt. Charles Tizeba(kulia) akizungumza na baadhi ya Viongozi na Wataalam wa Kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi na Mkoa wa Simiyu (hawapo pichani) kabla ya kutembelea Kampuni ya Quton katika Kata ya Kasoli Mkoani Simiyu kujionea uzalishaji wa mbegu za pamba.
Waziri wa Kilimo, Mhe.Dkt. Charles Tizeba(kushoto) akipokea maelezo kutoka kwa Meneja Uzalishaji wa Mbegu,Pheneas Chikaura(kulia) juu ya mbegu zilizozalishwa katika Kiwanda cha Kuzalisha mbegu za pamba cha Qutoni wakati wa ziara yake kiwandani hapo Wilayani Bariadi Mkoani Simiyu.
Baadhi ya Viongozi, wataalam wa Mkoa wa Simiyu, Wataalam wa Kampuni ya Quton na Alliance Ginnery wakimsikiliza Waziri wa Kilimo, Mhe.Dkt. Charles Tizeba(wa pili kushoto) mara baada ya kutembelea moja ya kitalu kilichopandwa mbegu za pamba zilizotolewa manyoya wakati wa ziara yake Mkoani humo.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Quton Tanzania Limited, Ndg.Pradyumansinh Chauhan akitoa taarifa ya uzalishaji wa mbegu za pamba zilizotolewa manyoya katika kiwanda cha kampuni hiyo kwa Waziri wa Kilimo, Mhe.Dkt.Charles Tizeba alipotembelea kiwanda hicho kilichopo Kata ya Kasoli wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Quton Tanzania Limited, Ndg.Pradyumansinh Chauhan akitoa taarifa ya uzalishaji wa mbegu za pamba zilizotolewa manyoya katika kiwanda cha kampuni hiyo kwa Waziri wa Kilimo, Mhe.Dkt.Charles Tizeba alipotembelea kiwanda hicho kilichopo Kata ya Kasoli wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu.
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe.Festo Kiswaga akizungumza na baadhi ya wananchi wa Kata ya Kasoli (hawapo pichani)wakati wa Ziara ya Waziri wa Kilimo, Mhe.Charles Tizeba, ambapo alitembelea kiwanda cha kuzalisha mbegu za pamba zilizoondolewa manyoya cha Quton Mkoani Simiyu ili kujionea uzalishaji wa mbegu hizo.

0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!