Saturday, July 16, 2016

WAZIRI TIZEBA:WANUNUZI WA PAMBA WATAKAOCHEZEA MIZANI WAKAMATWE


Serikali imesema itawachukulia hatua kali Wafanyabiashara wa pamba watakaochezea mizani kwa lengo la kuwaibia wananchi pale wanaponunua pamba.

 Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mhe. Charles Tizeba wakati wa ziara yake ya siku moja Mkoani Simiyu ,alipotembelea kituo cha kununulia pamba cha N.G.S ,katika kijiji cha Luguru wilayani Itilima.

Waziri Tizeba alisema Serikali haitavumilia vitendo vya unyonyaji dhidi ya mkulima kwa kuwa inafanya kila jitihada   kuwasaidia wakulima wa pamba ili waone umuhimu wa zao hilo na kuhakikisha wanazalisha pamba bora.

Aidha, Waziri Tizeba ameitaka Bodi ya Pamba kuwachukulia wakulima wote watakaobainika kuuza pamba iliyochafuliwa kwa kuwekwa maji, mchanga na mafuta kwa kuwa wanaharibu ubora wa pamba na hivyo kuchangia kushusha thamani ya pamba ya Tanzania katika soko la dunia.

“Sheria ni msumeno unakata kote, Serikali itawachukulia hatua wafanyabiashara wa pamba wanaochezea mizani na ninyi wananchi mnaoweka maji,mafuta na mchanga kwenye pamba muache, mkiendelea mtachukuliwa hatua kwa sababu mnasababisha pamba yetu inashuka thamani katika soko la Dunia”, alisema Tizeba

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Simyu, Anthony J. Mtaka amesema Serikali imekusudia kutatua kero za wakulima wa pamba  na kuwakikishia mazingira mazuri ya uzalishaji ikiwa ni pamoja na wakulima kupata mbegu bora, dawa na kuhakikisha wanauza pamba kwa bei nzuri.

“Kwa muda mrefu mmekuwa mkilima pamba na kupata mavuno yasiyoridhisha mpaka mkakata tamaa na kuanza kulima mazao mengine, tunataka pamba kama zao kuu la biashara mkoani Simiyu lizalishwe kwa wingi na katika ubora”, alisema Mtaka wakati alipozungumza na wananchi wa Luguru.

Sanjari na hilo Waziri, Tizeba ametoa wito wa wakulima kuwatumia Maafisa ugani waliopo katika maeneo yao ili wapate ushauri wa kitaalam juu ya kanuni bora za kilimo katika zao la pamba na mazao mengine wanayolima.

Akiwasilisha taarifa ya Mkoa kwa Waziri wa Kilimo,Mifugo na Uvuvi, Katibu Tawala Mkoa, Bw. Jumanne A. Sagini alisema Mkoa wa Simiyu una jumla ya Maafisa Ugani 261 waliopangwa kwenye kata na vijiji na wasimamiwa kikamilifu katika kutimiza majukumu yao ikiwa ni pamoja na kutoa ushauri  wa kitaalam kwa wakulima.

 Waziri Tizeba pia aliwahamasisha wananchi wa Mkoa wa Simiyu kulima kwa wingi dengu, choroko na mbaazi kwa sababu Serikali ya India kupitia kwa Waziri Mkuu wake imesema inahitaji kati ya tani milioni sita hadi nane za choroko, dengu na mbaazi.

Mkoa wa Simiyu unategemea Kilimo kwa asilimia kubwa ambapo sekta ya kilimo inachangia takribani asilimia 75 ya pato la Mkoa na zao kuu la biashara  ni pamba.

Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mhe. Charles Tizeba (kulia) akikagua mzani wa kupimia pamba katika kituo cha kununulia pamba cha N.G.S kilichopo Luguru, wilayani Itilima wakati wa ziara yake Mkoani Simiyu. (Picha Stella A. Kalinga)

Baadhi ya viongozi na wadau wa pamba wa Mkoa wa Simiyu wakimsikiliza Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mhe Charles Tizeba (hayupo pichani) wakati akizungumza na wakazi wa Luguru, wilayani Itilima, (wa kwanza kulia) Katibu Tawala Mkoa, Bw.Jumanne A. Sagini (wa pili) Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony J. Mtaka. (Picha Stella A. Kalinga)

Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mhe. Charles Tizeba (kulia) akizungumza na wakazi wa Luguru Wilayani Itilima mara baada ya kukagua mzani wa kupimia pamba katika kituo cha kununulia pamba cha N.G.S kilichopo Luguru, wilayani Itilima wakati wa ziara yake ya siku moja Mkoani Simiyu. (Picha Stella A. Kalinga)


Wednesday, July 13, 2016

SERIKALI YA CHINA YAMUUNGA MKONO JPM KUELEKEA TANZANIA YA VIWANDA



Serikali ya CHINA imeahidi kushirikiana na Mkoa wa Simiyu katika uwekezaji  hususani katika maeneo ya viwanda. Kilimo na uvuvi ili kutimiza azma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Magufuli ya kuwa na Tanzania ya Viwanda.

Hayo yamesemwa na Balozi Mshauri wa China nchini, Bw.Zhang Biao wakati alipofanya ziara yake mkoani Simiyu na kufanya mazungumzo na Uongozi wa Mkoa wa Simiyu na wadau wa maendeleo mkoani humo.

Balozi Zhang amesema endapo  Serikali itatengeneza mazingira wezeshi kwa kujenga miundombinu kwa ajili ya uwekezaji, Makampuni kutoka China yatakuwa tayari kuwekeza mkoani Simiyu.

“ Mkoa wa Simiyu una maliasili nyingi na kwa kuwa mmeonyesha utayari Makampuni ya China yatakuja kuwekeza kwa kasi, Serikali isaidie kuwezesha huduma za maji na umeme zinapatikana na miundombibu ya kusafirisha malighafi kupelekeka viwandani na kupeleka bidhaa zetu zitakazozalishwa sokoni”, alisema Balozi Zhang.

Akitoa shukrani kwa niaba ya Serikali Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony. J. Mtaka amesema Serikali iko tayari kutenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji  na kuhakikisha miundombinu muhimu kama maji na umeme inapatikana kwa ajili ya kuwezesha uwekezaji na akamuomba  Balozi Zhang kuunganisha Mkoa wa Simiyu na Makampuni ya China yaliyo tayari kuwekeza.  

“ Mkoa wa Simiyu una fursa nyingi sana za uwekezaji katika eneo la viwanda vya nguo na nyuzi kwa kuwa unazalisha karibu asilimia 60 ya pamba ya nchini, lakini pia mkoa wetu ni wa tatu kwa kuwa na ng’ombe wengi kwa hiyo bado kuna fursa ya uwekezaji katika mazao ya ufugaji wa ng’ombe kama nyama, ngozi na maziwa” , alisema Mtaka.

Aidha, Mtaka alisema kupitia sehemu ya Ziwa Viktoria mkoa una fursa ya uwekezaji katika kilimo cha umwagiliaji ambacho alieleza kinaweza kusaidia kuinua uchumi wa wakazi wa wilaya ya Busega na Mkoa wa Simiyu kwa ujumla, ambapo Serikali inaandaa mpango wa kuwa na zao moja kwa wilaya moja (one product one district)  ili kila wilaya iwe na zao au shughuli moja inayowaingizia watu wake kipato.

Hii ni mara ya kwanza kwa Balozi Mshauri wa China nchini kufika mkoani Simiyu ambapo Balozi Zhang ameahidi kuendeleza urafiki wa nchi ya Tanzania na China ambao ulianza tangu enzi za Rais wa awamu ya kwanza Hayati Julius K. Nyerere na kuhakikisha uhusiano kati ya nchi hizi mbili unawanufaisha wananchi wa pande zote mbili.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony J. Mtaka  akimshukuru Balozi Mshauri wa China nchini Tanzania Bw.Zhang Biao mara baada ya kuzungumza na Viongozi na wadau wa maendeleo  (hawapo pichani) wakati wa ziara yake mkoani Simiyu. (Picha na Stella A. Kalinga 
Katibu Tawala mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne A. Sagini (kulia) akizungumza jambo na Balozi Mshauri wa China nchini, Bw.Zhang Biao (katikati) mara baada ya kumaliza mazungumzo  na Viongozi na wadau wa maendeleo (hawapo pichani) wakati wa ziara yake mkoani Simiyu,  (kushoto) Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony J. Mtaka. (Picha na Stella A. Kalinga)
Balozi Mshauri wa China nchini, Bw.Zhang Biao (wa nne kulia) akiwa katika picha ya pamoja na  Viongozi na wadau wa maendeleo wakati wa ziara yake mkoani Simiyu, (kushoto kwake) Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga, (kulia kwake) Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony J. Mtaka, anayefuata Katibu Tawala Mkoa, Bw. Jumanne A. Sagini (Picha na Stella A. Kalinga)

Monday, July 11, 2016

WAKULIMA WA PAMBA WAASWA KUTOWEKA MAJI, MCHANGA, MAFUTA KULINDA UBORA WA PAMBA



Wakulima wa pamba mkoani Simiyu wameaswa kuacha tabia ya kuweka maji ,mchanga, na mafuta katika pamba kwa kisingizio cha kuongeza uzito na wale watakaokaidi watachukuliwa hatua kali 

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony J. Mtaka wakati alipozungumza na Wafanyabiashara wa Pamba pamoja na Wenyeviti  na Wakurugenzi wa Halmashauri zote za Mkoa wa Simiyu wakati wa mjadala wa suala la ununuzi wa pamba katika msimu wa mwaka 2016.

Mtaka amesema wakulima wanaoweka maji , mchanga na mafuta katika pamba wanachangia katika kushusha thamani  pamba ya Tanzania na hivyo kufanya  thamani yake kuwa chini katika soko la dunia.
“Mkoa wa Simiyu unazalisha zaidi ya asilimia 60 ya pamba ya Tanzania kwa hiyo kama pamba hii ikiharibiwa ni wazi kwamba ni pamba ya Tanzania inaharibiwa,mwaka jana tumeuza zaidi ya kilo milioni 70; kama mkoa unaozalisha pamba kwa wingi   tumejipanga kurejesha heshima ya zao la pamba” alisema Mtaka.

Aidha, Mtaka amekemea tabia ya wafanyabiashara kuwaibia wakulima kwa kuchezea mizani na akaagiza atakayebainika achukuliwe hatua kali.

“Hatutavumlia kuona wafanyabiashara wanaowaibia wakulima kwa kufanya ujanja ujanja katika mizani tukiwabaini tutawachukulia hatua kali, na hili limeshaanza kufanyiwa kazi, katika wilaya ya Meatu baadhi ya wafanyabiashara wameshtakiwa , naupongeza sana uongozi wa wilaya ya Meatu” , alisema Mtaka.

Kwa upande wao Wakurugenzi na Wenyeviti wa Halmashauri wameahidi kutoa ushirikiano kwa wanunuzi na kuwaomba watoe malipo ya awali (advanced payment) ili kupunguza madeni yasiyoya lazima na kuzifanya Halmashauri kuendesha baadhi ya shughuli muhimu kupitia ushuru wa pamba.

 Wakati huo huo Mtaka amewataka mawakala wa makampuni yanayojihusisha na ununuzi wa pamba kuwa waaminifu kwa kuacha tabia ya kukimbia na fedha wanazopewa kwa ajili ya kununua pamba na kuwadanganya wakulima kwa kuchezea mizani (kuchakachua) pale wanapopima pamba.

“ Mawakala wa makampuni wafanye kazi yao kwa uaminifu kwa kuwa hiyo ni sehemu ya ajiria kwao, wasilazimishe wafanyabiashara kwenda kutafuta mawakala Kenya, Uganda au nchi nyingine kwa sababu ya kukosa sifa ya uaminifu.Wawe waaminifu kwa fedha wanazopewa na kupima kwa mizani ambazo hazijachakachuliwa” alisema Mtaka. 

Msimu wa ununuzi wa pamba mkoani Simiyu umeanza na Serikali imeagiza wafanyabiashara  kununua kilo moja kwa shilingi 1000 na kuendelea.














Wednesday, June 1, 2016

MASWA WATEKELEZA AGIZO LA RAIS LA KUTENGENEZA MADAWATI KWA ASILIMIA 75



Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu imetekeleza agizo la Rais John Pombe Magufuli la kutengeneza madawati kwa asilimia 75, ambapo hadi kufikia Mei 31mwaka huu, imetengeneza madawati 19,655 kati ya  26,261 yanayohitajika kwa shule za msingi na meza 10,943 kati ya 9,359 zinazohitajika na viti 10,810 kati ya 9,359 vinavyohitajika na kufanya kuwa na ziada ya meza 1,432 na viti 1,277 kwa shule za sekondari. 

Hayo  yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Mhe. Rosemary Kirigini wakati akiwasilisha taarifa ya hali ya utekelezaji wa agizo hilo mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony J. Mtaka alipofanya ziara kuona namna agizo hilo linavyotekelezwa wilayani humo.
Mhe. Kirigini alisema wamefikia hatua hiyo kutokana na kuwashirikisha wadau mbalimbali, kunua mbao na  kutumia  mafundi ambao ni wanafunzi wa Chuo cha Ufundi cha Binza, ambao wamekuwa wakitengeneza madawati 500 hadi 1000 kwa siku, kwa gharama ya shilingi 21,625/= kwa dawati moja.

Akipokea taarifa ya wilaya ya Maswa, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu mhe. Anthony J. Mtaka ameupongeza uongozi wa wilaya ya Maswa kwa hatua waliyofikia na ubunifu walioutumia katika kutafuta mbao na kuwatumia mafundi kutoka Chuo cha Ufundi cha Binza, hali iliyosaidia kupunguza gharama na akazitaka wilaya nyingine kutumia uzoefu wa Maswa ili zikamilishe agizo la Mhe. Rais kwa wakati uliopangwa.
“Hiki chuo ni cha Serikali, wakipewa mbao wanatengeneza dawati moja kwa shilingi 21,625 kama alivyotuambia DC,kwa nini wilaya zote za mkoa huu wasione umuhimu wa kuwatumia hawa vijana wa chuo hiki kuwafanyia kazi yao. Watu wanatengeneza dawati moja kwa shilingi 70,000/= sasa si bora tukatumia chuo chetu hiki ili tupunguze gharama na kumuwezesha Mkuu wa chuo akapata fedha zitakazomsaidia kuendesha chuo badala ya kutegemea ruzuku ya serikali?” alisema Mtaka.
  
Aidha, Mtaka amepiga marufuku tabia ya kutumia viti,meza na madawati ya wanafunzi katika shughuli nyingine kama mikutano ya hadhara kwa kuwa kuhamisha madawati au viti kutoka sehemu moja kwenda nyingine kunachangia uharibifu.

Wakati huo huo Mtaka amewataka Maafisa Elimu kuweka mikakati ya kitaaluma ili kuwafanya kuongeza ufaulu kwa wanafunzi ikiwa ni pamoja na kuweka utaratibu wa kufanya mitihani ya majaribio ya mara kwa mara kwa madarasa ya mitihani na kuanzisha na kuzisimamia klabu za masomo mbalimbali mashuleni

Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa, Jumanne A. Sagini amesema Halmashauri ione umuhimu wa kupima maeneo yote ya shule ili yatambuliwe yasivamiwe na wananchi kwa kufanya shughuli nyingine kinyume na utaratibu. 

Halmashauri ya Wilaya ya Maswa ina jumla ya shule za Msingi 121 zenye wanafunzi  78,783 na shule za sekondari 40  kati ya hizo 36 ni za Serikali ambazo zina jumla ya wanafunzi 9359. 
Mkuu wa Wilaya ya MaswaMhe. Rosemary Kirigini (kulia) alitoa maelezo kwa Mkuu wa Mkoa Mhe. Anthony J. Mtaka (wa pili kulia), kuhusu madawati yaliyotengenezwa katika Chuo cha Ufundi cha Binza wakati wa ziara yake wilayani humo. Wengine ni viongozi wa Mkoa na Wilaya walioshiriki katika ziara hiyo.Picha na Stella A. Kalinga.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka (wa tatu kushoto) akizungumza na viongozi wa wilaya ya Maswa (hawapo pichani) kabla ya kufanya ziara ya kukagua utekelezaji wa agizo la Mhe.Rais la utengenezaji wa madawati wilayani humo, (wa pili kushoto) Katibu Tawala Mkoa, Jumanne Sagini na (wa nne kulia) ni Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Mhe. Rosemary Kirigini. Picha Na Stella A. Kalinga.

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!