Friday, December 8, 2017

WANAFUNZI 19,242 WACHAGULIWA KUJIUNGA KIDATO CHA KWANZA MWAKA 2018 SIMIYU

Jumla ya wanafunzi 19,242 mkoani Simiyu sawa na asilimia 92.5 wamechaguliwa kujiunga na shule za sekondari katika awamu ya kwanza kwa mwaka 2018.

Hayo yamesemwa na Katibu Tawala wa Mkoa huo, Ndg.Jumanne Sagini katika kikao cha kutangaza matokeo ya uchaguzi wa wanafunzi wa kidato cha  kwanza mwaka 2018 kilichofanyika leo Mjini Bariadi.

Sagini amesema jumla ya wanafunzi 20,818 sawa na asilimia 67.73 ya wanafunzi waliofanya mtihani wa darasa la saba walifaulu, ambapo kati yao 1576 sawa na asilimia 7.5 ya waliofaulu hawakupata nafasi ya kuanza kidato cha kwanza kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa na madawati katika baadhi ya Halmashauri.

“Wanafunzi waliokosa nafasi Halmashauri ya Mji wa Bariadi ni wale waliopaswa kwenda Shule ya Sekondari Kidinda(207) na Biashara(162), Halmashauri ya Wilaya ya Busega walipaswa kwenda shule za Lamadi (486), Nasa (358) na Sogesca (363). Ni wajibu wa Halmashauri hizi kushirikiana na wananchi kuhakikisha miundombinu pungufu imekamilishwa haraka ili ifikapo Februari 15, 2018  wanafunzi hao waripoti kwenye shule walizopaswa kwenda” amefafanua Sagini.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega na Halmashauri ya Mji Bariadi wamesema Halmashauri zao zinaendelea na ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule hizo na wataendelea kufanya jitihada mbalimbali kwa kushirikiana na wananchi kuhakikisha kuwa miundombinu hiyo pungufu inakamilika haraka, ili kufikia Februari 05 mwakani wanafunzi wote waliokosa nafasi awamu ya kwanza waweze kwenda shule.

Wakati huo huo Sagini amezitaka Halmashauri kuendelea kushirikiana na wadau wote wa elimu kukamilisha majengo na kuandaa mazingira ya kuwapokea wanafunzi wote waliochaguliwa kuanza kidato cha kwanza mwaka 2018 bila vikwazo vya aina yoyote.

Ameongeza kuwa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla washirikiane na uongozi wa wilaya, halmashauri na shule  kuhakikisha kwamba wanafunzi wote waliochaguliwa wanaandikishwa, wanaripoti shuleni na kuendelea na masomo yao kwa bidii hadi watakapomaliza elimu yao ya sekondari mwaka 2021.

Akielezea hali ya ufaulu kwa wanafunzi wa darasa la saba  kwa mwaka 2017, Afisa Elimu Mkoa, Mwl. Julius Nestory amesema kwa mara ya kwanza mwanafunzi aliyeongoza katika Mkoa ambaye ni (msichana) Hoka Lyaganda Saguda ametoka katika Shule ya Serikali ambayo ni Shule ya Msingi Sima B iliyopo Mjini Bariadi.

Amesema ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa elimu na kuinua kiwango cha ufaulu mkoani humo Mikakati ya kuinua ufaulu ya kila wilaya isimamiwe kikamilifu,  Ofisi za Wilaya, Halmashauri, Kata na Wakuu wa Shule zifanye ufuatiliaji kuhusu ufundishaji na ujifunzaji na  Ukaguzi wa shule ufanyike kwa kiwango kisichopungua asilimia 50 kwa mwaka na Wakurugenzi watenge fedha kwa ajili ya ukaguzi wa shule.

Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Itilima, Mhe.Mahamoud Mabula ameshauri kuwa ili kuinua ufaulu suala la maendeleo ya Elimu liwe agenda ya kudumu katika vikao vyote muhimu vya Halmashauri mkoani humo, ili kutoa nafasi ya kujadili changamoto mbalimbali za sekta ya elimu na kuzitafutia ufumbuzi.


Idadi ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza mwaka 2018 Mkoani Simiyu imeongezeka kutoka wanafunzi 16,620 mwaka 2017 hadi wanafunzi 19,242.
Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Ndg. Jumanne Sagini akifungua kikao cha kutangaza matokeo ya Uchaguzi wa Wanafunzi wa Kujiunga Kidato cha Kwanza mwaka 2018 Mkoani humo, kilichofanyika leo Mjini Bariadi.
Afisa Elimu Mkoa, Mwl. Julius Nestory akiwasilisha taarifa ya hali ya ufaulu wa wanafunzi wa darasa la saba kwa mwaka 2017, katika  kikao cha kutangaza matokeo ya Uchaguzi wa Wanafunzi wa Kujiunga Kidato cha Kwanza mwaka 2018 Mkoani Simiyu, kilichofanyika leo Mjini Bariadi.
Mkuu wa Wiayaya Bariadi, Mhe.Festo Kiswaga akichangia hoja katika katika  kikao cha kutangaza matokeo ya Uchaguzi wa Wanafunzi wa Kujiunga Kidato cha Kwanza mwaka 2018 Mkoani Simiyu, kilichofanyika Mjini Bariadi.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Meatu, Mhe.Juma Mwiburi akichangia hoja katika  kikao cha kutangaza matokeo ya Uchaguzi wa Wanafunzi wa Kujiunga Kidato cha Kwanza mwaka 2018 Mkoani Simiyu, kilichofanyika leo Mjini Bariadi.
Mkuu wa Wilaya ya Busega, Mhe.Tano Mwera akichangia hoja katika  kikao cha kutangaza matokeo ya Uchaguzi wa Wanafunzi wa Kujiunga Kidato cha Kwanza mwaka 2018 Mkoani Simiyu, kilichofanyika leo  Mjini Bariadi.
Katibu Tawala Wilaya ya Meatu, Veronica Kinyemi akichangia hoja katika  kikao cha kutangaza matokeo ya Uchaguzi wa Wanafunzi wa Kujiunga Kidato cha Kwanza mwaka 2018 Mkoani Simiyu, kilichofanyika leo  Mjini Bariadi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega, Ndg.Anderson Njiginya, akichangia hoja katika  kikao cha kutangaza matokeo ya Uchaguzi wa Wanafunzi wa Kujiunga Kidato cha Kwanza mwaka 2018 Mkoani Simiyu, kilichofanyika leo Mjini Bariadi.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Maswa, Mhandisi Paul Jidayi akichangia hoja katika  kikao cha kutangaza matokeo ya Uchaguzi wa Wanafunzi wa Kujiunga Kidato cha Kwanza mwaka 2018 Mkoani Simiyu, kilichofanyika leo Mjini Bariadi.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Itilima, Mahamoud Mabula akichangia hoja katika  kikao cha kutangaza matokeo ya Uchaguzi wa Wanafunzi wa Kujiunga Kidato cha Kwanza mwaka 2018 Mkoaani Simiyu, kilichofanyika leo Mjini Bariadi.
Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Mhe.Benson Kilangi akichangia hoja katika  kikao cha kutangaza matokeo ya Uchaguzi wa Wanafunzi wa Kujiunga Kidato cha Kwanza mwaka 2018 Mkoani Simiyu, kilichofanyika leo Mjini Bariadi.
Mkurugenzi wa Mji wa Bariadi, Ndg.Melkezedeck Humbe akichangia hoja katika  kikao cha kutangaza matokeo ya Uchaguzi wa Wanafunzi wa Kujiunga Kidato cha Kwanza mwaka 2018, Mkoani Simiyu kilichofanyika leo Mjini Bariadi.
Baadhi ya Wajumbe wa Kikao cha Kamati ya kutangaza matokeo ya Uchaguzi wa wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2018 mkoani Simiyu, kilichofanyika leo Mjini Bariadi

Wednesday, December 6, 2017

SIMIYU YAJIPANGA KUVUNA TANI 490,000 ZA PAMBA MWAKA 2018

Mkoa wa Simiyu unatarajia kuvuna takribani tani 264,000 sawa na kilo milioni 264 hadi tani 490,000  sawa na kilo milioni 490 za zao la pamba, katika msimu wa mwaka 2017/2018 kutoka kilo milioni 70 za mwaka 2016/2017.

Hayo yamesemwa  na Afisa Kilimo Ofisi Mkuu  wa Mkoa wa Simiyu, Ndg.Elias Kasuka  katika Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa(RCC) kilichofanyika Mjini Bariadi.

Kasuka  amesema  mkoa wa Simiyu una jumla ya wakulima wa pamba 301, 000 watakaolima pamba katika msimu huu, katika eneo la zaidi ya ekari 700,000 huku matarajio ya mavuno yakiwa ni zaidi ya kilo 700 kwa ekari moja.

Mkuu wa Mkoa huo, Mhe.Anthony Mtaka amesema Watalaam wa Kilimo wa Mkoa na Wilaya waandae mipango kazi yao itakayoonesha ratiba ya kuwatembelea wakulima wa pamba katika kipindi chote cha msimu tangu kupanda mpaka watakapovuna, ili malengo hayo ya kuongeza mavuno yaweze kutimia.

Mtaka ameongeza kuwa Zao la pamba linachangia kwa kiasi kikubwa mapato kwa Halmashauri za Mkoa huo, hivyo Wakurugenzi wanapaswa kuhakikisha Maafisa Kilimo wanawezeshwa muda wote wanaohitaji kuwafikia wakulima katika kipindi cha msimu wa kilimo badala ya kusubiri wakati wa ukusanyaji ushuru baada ya mavuno.

“Wakurugenzi nilishawaambia Uhai wa Halmashauri zenu uko kwenye ushuru wa pamba hakikisheni Maafisa Kilimo wanawezeshwa kuwafikia wakulima; Wakuu wa Wilaya pia  kagueni mashamba ya pamba kwenye maeneo yenu. Wenyeviti wa Halmashauri niwaombe tusichangamkie pamba wakati inapovunwa tu, tuichangamkie hata pale inapokuwa shambani, tuwaone wananchi wanapolalamika kuwa mbegu hazijaoota au dawa hii haiuwi wadudu”alisisitiza Mtaka.

Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Mhe.Dkt.Seif Shekalaghe ameomba Uongozi wa Mkoa kuwasiliana na Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba ili wakulima ambao hawajapata mbegu za pamba katika baadhi ya maeneo wapate haraka kabla ya msimu wa upandaji kuisha.

Akiwasilisha taarifa ya  Maendeleo ya Sekta ya Kilimo , Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dkt.Gamitwe Mahaza amesema hadi kufikia Oktoba 30 mwaka huu jumla ya tani 3,628.727 za mbegu za pamba zilikuwa zimeshasambazwa sawa na wastani wa asilimia 48.0 ya lengo la kusambaza tani 7,485.400.

Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka amesema  Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji imetenga fedha kwa ajili ya Ujenzi wa Majengo ya Ofisi na Karakana za Shirika la Maendeleo ya Viwanda VidogoVidogo (SIDO) Mkoani humo, ambayo yanatarajiwa kuanza kujengwa mwishoni mwa mwaka huu katika eneo la Isanga Bariadi Mjini na Mkandarasi ambaye ni SUMA JKT ameshafika kuona eneo husika.

Amesema Serikali inakusudia kujenga SIDO ya kisasa itakayokidhi mahitaji yanayoendana na wakati ikiwa ni pamoja na  kuwa mahali sahihi pa makundi muhimu hususani vijana na wanawake kupata mafunzo ya kuendesha shughuli zao za uzalishaji na viwanda vidogo.

“ Kila DC , Diwani tunapoenda kujenga SIDO kwenye Mkoa wetu,changamkia fursa, wananchi katika maeneo yenu waje na miradi ya viwanda vidogo vidogo, Tumeongea na Baraza la Taifa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na wadau wengine kuhusu miradi hii  midogo midogo; tuna uzalishaji wa viatu vya ngozi Busega, Bariadi na Maswa, tunataka kila kikundi kiende kwenye uzalishaji wa eneo lake la umahiri katika bidhaa za ngozi “ alisema.  

Mkoa wa Simiyu unatekeleza Sera ya Viwanda chini ya Kauli Mbiu ya Mkoa huo ya Wilaya moja Bidhaa Moja Kiwanda Kimoja(One District One Product-ODOP) na umedhamiria kuanza kutekeleza mpango wa Bidhaa Moja Kijiji Kimoja(One Village One Product-OVOP)
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akifungua kikao cha Kamati yaUshauri ya Mkoa huo(RCC), kilichofanyika jana Mjini Bariadi, (kushoto)Mbunge wa Bariadi Mhe. Andrew Chenge,(wa pili kushoto) Katibu Tawala mkoa Simiyu, Ndg.Jumanne Sagini na ( kulia) Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe.Festo Kiswaga.
Baadhi ya wajumbe wakifuatilia masuala mbalimbali yaliyokuwa yakiwasilishwa katika Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) wa Simiyu kilichofanyia jana Mjini Bariadi.
Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Dkt.Gamitwe Mahazaakiwasilisha Taarifa ya Mkoa ya Maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, katika Kikao Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kilichofanyia jana Mjini Bariadi.
Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Mhe.Dkt.Seif Shekalaghe akichangia hoja katika Kikao Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC)  Simiyu kilichofanyia jana Mjini Bariadi.

WADAU WA MAENDELEO SIMIYU WAKUBALIANA NA UCHANGIAJI KATIKA UJENZI WA MIUNDOMBINU YA SHULE KUELEKEA MWAKA 2018

Wadau wa Maendeleo Mkoani Simiyu wamekubaliana na Uchangiaji wa Ujenzi wa Miundombinu ya shule Mkoani humo hususani vyumba vya madarasa katika shule za Msingi na Sekondari ili kukabiliana na upungufu uliopo, kutokana na ongezeko la wanafunzi watakaoanza darasa la kwanza na kidato cha kwanza mwaka 2018.

Makubaliano hayo yamefikiwa katika Kikao cha Ushauri wa Mkoa(RCC) kilichofanyika jana Mjini Bariadi.

Akifungua kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka amesema Mkoa huo unahitaji zaidi ya shilingi bilioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya shule hususani Vyumba vya madarasa , hivyo wananchi pamoja na wadau wengine wanaombwa kuchangia ujenzi huo.

Mtaka amesema hadi sasa wapo wadau kadhaa walioonesha nia ya kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo na nyumba za walimu kwa kutoa ahadi za vifaa vya ujenzi vikiwemo saruji na mabati.

Mbunge wa Jimbo la Bariadi, Mhe.John Chenge amesema suala la Elimu ni si la Serikali Kuu pekee bali ni pamoja na wananchi, Serikali za Mitaa pamoja na wadau wengine, hivyo wananchi wahamasishwe kuchangia ujenzi wa miundombinu hiyo kwa ajili ya maendeleo ya Elimu mkoani humo.

Akichangia hoja hiyo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Mhe.Enock Yakobo ameshauri kuwa hamasa ya ujenzi wa  miundombinu ya shule ifanywe na viongozi wote Mkoani humo,  ikiwezekana kwa kubadilishana maeneo ya kwenda kutoa hamasa ambayo ni tofauti na maeneo wanayofahamika zaidi.

“ Wakati  tunaanza ujenzi wa Shule za Kata tulikubaliana kuwa viongozi tubadilishane uzoefu kwa kila mmoja kwenda kuhamasisha maeneo ambayo wananchi hawawafahamu na hawajawazoea;  viongozi wa Wilaya ya Bariadi walienda Meatu, wa Meatu wakaenda Maswa, wa Maswa walienda Bariadi , lile jambo lilifanikiwa sana wananchi walihamasika wakachangia nashauri tutumie pia mfumo huu tutafanikiwa”alisema.

Kaimu Afisa Elimu Mkoa wa Simiyu, Ndg.Charles Maganga amesema Wanafunzi wanaotarajia kuingia darasa la kwanza mwaka 2018 ni 109,899 wakati waliomaliza darasa la saba ni 30,898 hali inayosababisha mahitaji mapya ya vyumba vya madarasa 1757 na madawati 26,334; wanaotarajia kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2018 ni 20,818 waliohitimu kidato cha nne 6195 mahitaji mapya ya vyumba vya madarasa ni 367 na madawati 14,623.

Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Maswa,Mhe.Dkt. Shekalaghe ametoa wito kwa viongozi wenzake kuwahamasiha wazazi kuchangia chakula kwa ajili ya watoto wao ili waweze kupatiwa chakula cha mchana kwa shule ambazo bado hazijaanza kufanya hivyo, jambo na  ambalo liliungwa mkono na viongozi wengi

Kuhusu suala la mimba shuleni Mkuu wa Mkoa  wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka amesema Serikali Mkoani humo itaendelea kuwachukulia hatua kali za kisheria wale wote watakaobainika kuwapa mimba wanafunzi wa kike.

Mtaka amesema Serikali Mkoani humo imedhamiria  na kuweka mikakati madhubuti ya kuwalinda watoto wa kike ikiwa ni pamoja na  kujenga mabweni kwa ajili ya wasichana katika shule zote za kata, ili kuwasaidia kuondokana na vishawishi wanavyoweza kuvipata kutokana na kutembea mwendo mrefu.


Mtaka pia alitumia kikao hicho kuwajulisha viongozi na wadau wa Maendeleo Mkoani Simiyu kuwa Mkoa huo umepewa heshima ya kuwa mwenyeji wa Mahafali ya 34 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania mwaka 2018, hivyo akawataka kujiandaa kwa ajili ya tukio hilo ambalo litaleta watu zaidi ya 1500 kutoka maeneo mbalimbali hapa nchini.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akifungua kikao cha Kamati yaUshauri ya Mkoa huo(RCC), kilichofanyika jana Mjini Bariadi, (kushoto)Mbunge wa Bariadi Mhe. Andrew Chenge,(wa pili kushoto) Katibu Tawala mkoa Simiyu, Ndg.Jumanne Sagini na ( kulia) Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe.Festo Kiswaga.
Baadhi ya wajumbe wakifuatilia masuala mbalimbali yaliyokuwa yakiwasilishwa katika Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) wa Simiyu kilichofanyia jana Mjini Bariadi.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Mhe. Enock Yakobo akichangia hoja katika Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kilichofanyia jana Mjini Bariadi.
Mbunge wa Jimbo la Itilima, Mhe.Njalu Silanga akichangia hoja katika Kikao Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC)  Mkoani Simiyu kilichofanyia jana Mjini Bariadi.
Baadhi ya wajumbe wakifuatilia masuala mbalimbali yaliyokuwa yakiwasilishwa katika Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) wa Simiyu kilichofanyia jana Mjini Bariadi.
Kaimu Afisa Elimu Mkoa wa Simiyu, Ndg Charles Maganga akiwasilisha taarifa ya Mkoa ya  Maendeleo ya Elimu katika Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa(RCC), kilchofanyika jana Mjini Bariadi.
Meneja wa AGPAHI Kanda ya Ziwa, Dkt.Nkingwa Mabelele akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi wa Shirika hilo ambao wadau wa Afya Mkoani Simiyu, katika Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa(RCC), kilchofanyika jana Mjini Bariadi.
Mbunge wa Jimbo la Bariadi, Mhe.Andrew Chenge akichangia hoja katika Kikao Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC)  Simiyu kilichofanyia jana Mjini Bariadi.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Maswa, Mhe.Paul Jidayi akichangia hoja katika Kikao Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC)  Simiyu kilichofanyia jana Mjini Bariadi.
Katibu Tawala Msaidizi wa Huduma zaMaji kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhandisi.Hatari Kapufi akiwasilisha Taarifa ya Huduma za Maji Mkoa, katika Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa(RCC), kilchofanyika jana Mjini Bariadi.
Mchungaji wa Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA) Bariadi, Mashauri Bahini akichangia hoja katika Kikao Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC)  Simiyu kilichofanyia jana Mjini Bariadi.
Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Mhe.Dkt.Seif Shekalaghe akichangia hoja katika Kikao Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC)  Simiyu kilichofanyia jana Mjini Bariadi.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Itilima, Ndg.Mariano Mwanyigu akichangia hoja katika Kikao Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC)  Simiyu kilichofanyia jana Mjini Bariadi.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Bariadi, Mhe.Robert Lweyo akichangia hoja katika Kikao Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC)  Simiyu kilichofanyia jana Mjini Bariadi.
Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Dkt.Gamitwe Mahaza akiwasilisha Taarifa ya Mkoa ya Maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, katika Kikao Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kilichofanyia jana Mjini Bariadi.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dkt. Mageda Kihulya akiwasilisha Taarifa ya Afya ya Mkoa, katika Kikao Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kilichofanyia jana Mjini Bariadi.

Monday, December 4, 2017

TARURA WATAKIWA KUSIMAMIA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA BARABARA KWA WELEDI

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka ametoa wito kwa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini(TARURA) Mkoani humo kusimamia utekelezaji wa Miradi ya  ujenzi wa barabara na madaraja kwa kuzingatia weledi.

Mtaka ametoa wito huo wakati akifungua kikao cha Bodi ya Barabara ya Mkoa huo, kichofanyika leo Mjini Bariadi  Mkoani humo.

" Nawaomba TARURA mfanye kazi kwa kuzingatia weledi, siyo madaraja yanajengwa mnapeleka karavati zinavunjika kabla daraja halijajengwa, mahali pa kuweka kokoto mnaweka udongo, mtaidhalilisha taaluma; ningeomba mzingatie weledi kwa sababu mkifanya vibaya wananchi watatushtaki watasema tumeanzisha wakala ambaye hana maana kwao" amesema Mtaka.

Ameongeza kuwa Uongozi wa Mkoa wa Simiyu haujapata shida juu ya miradi ya barabara inayosimamiwa na Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), hivyo ipo haja pia kwa TARURA kusimamia utekelezaji wa miradi yake katika ubora,  kwa kuwa Miradi hiyo imeondolewa katika Halmashauri (Mabaraza ya Madiwani) na kupelekwa TARURA, ili ipangiwe mipango  na kusimamiwa na wataalam pekee kwa lengo la kuonesha utofauti kiutendaji  na umuhimu wa Wakala huo katika kuwapa huduma bora wananchi.

Wakati huo huo Mtaka amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutoa shilingi Bilioni 86.1 kwa ajili ya Ujenzi wa Barabara ya Bariadi -Maswa yenye urefu wa Kilomita 49.7 kwa kiwango cha lami, ambayo amesema ikikamilika itaifanya Bariadi na Maeneo mengine ya Mkoa huo kama Malampaka(Maswa) kuwa  maeneo ya kibiashara.

Aidha, amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri ya Mji Bariadi na Halmashauri ya Wilaya Maswa kutumia fursa hiyo kujenga vituo vya mabasi vya kimkakati vitakavyoendana na kasi ya uingiaji wa magari mengi baada ya kukamilika kwa barabara ya Maswa-Bariadi na Ujenzi wa Reli ya “Standard Gauge” na  Bandari kavu itakayojengwa Malampaka wilayani Maswa.

Akiwasilisha taarifa ya barabara zinazosimamiwa na TANROADS, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Simiyu, Mhandisi Albert Kent  amesema Barabara ya Bariadi-Maswa itajengwa kwa kutumia fedha za Serikali ya Tanzania na itachukua muda wa miezi 24 mpaka kukamilika kwake, ambapo amebainisha kuwa Mkandarasi Kampuni ya M/s CHICO ameshawasili eneo la kazi(site).

Kwa upande wake  Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Ndg. Jumanne Sagini ameomba wazo la marekebisho ya Viwango vya fedha zinazotakiwa kwenda TANROADS na TARURA ambalo lilitolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, lifanyiwe kazi ili TARURA wapate fedha na kufanya kazi kwa weledi pamoja na kusaidia barabara za Halmashauri zisife.

Sagini ameongeza kuwa Halmashauri zishirikiane na TARURA kutafuta namna ya kuzifanyia matengenezo barabara za Vijiji ambazo haziko chini ya usimamizi wa wakala huo (TARURA), lakini  ni za muhimu kwa maendeleo ya wananchi hususani zinazounganisha vijiji ili kurahisisha mawasiliano kati ya kijiji na kijiji.

Meneja wa TARURA Mkoa wa Simiyu,Mhandisi Peter Mosha amesema mwaka 2017/2018 Mkoa huo umeidhinishiwa zaidi ya shilingi bilioni sita kwa ajili ya kufanya matengenezo kwenye mtandao wa barabara wenye jumla ya kilomita 1780.87 , madaraja na makaravati katika Halmashauri zote sita za Mkoa kulingana na mahitaji na mpango wa bajeti wa Halmashauri husika.

Naye Mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki, Mhe. Mashimba Ndaki amesema Wakala wa Barabara (TANROADS) unapaswa kuhakikisha barabara zote zinawekewa  vivuko ili kuwasaidia wananchi kuvuka kwa usalama.


Akipongeza kazi inayofanywa na TANROADS Mkoa wa Simiyu, Mbunge wa Jimbo la Itilima, Mhe. Njalu Silanga ameomba TANROADS kuona namna ya kufanyia kazi kona nyingi zilizopo katika barabara ya Bariadi-Lagangabili-Kisesa  pamoja na kuangalia upanuzi wa barabara mbalimbali zinazosimamiwa na Wakala huo ili zisisababishe uharibifu wa magari.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na wajumbe wa Bodi ya Barabara ya Mkoa huo(hawapo pichani) katika Kikao cha bodi hiyo kilichofanyika jana Mjini Bariadi, (kushoto) Katibu Tawala Mkoa, Ndg.Jumanne Sagini na Mkuu wa Wilaya ya Bariadi,Mhe.Festo Kiswaga(kulia)
Meneja wa Wakala wa Barabara Mijiji na Vijijini(TARURA) Mkoa wa Simiyu, Mhandisi.Peter Mosha akiwasilisha taarifa ya wakala huo(Mkoa) kwa Wajumbe wa Bodi ya Barabara katikakikao cha bodi hiyo kilichofanyika Mjini Bariadi.
Meneja wa Wakala wa Barabara  (TANROADS) Mkoa wa Simiyu, Mhandisi. Albert Kent akiwasilisha taarifa ya miradi inayosimamiwa na wakala huo Mkoani humo, katika Kikao cha Bodi ya Barabara kilichofanyika leo Mjini Bariadi.
Mkuu wa Wilaya ya Maswa Mhe.Dkt. Seif Shekalaghe akichangia hoja katika Kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Simiyu kilichofanyika leo Mjini Bariadi.
Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi, Mhe.Mashimba Ndaki akichangia hoja katika Kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Simiyu kilichofanyika leo Mjini Bariadi.
Baadhi ya Wajumbe wa Bodi ya Barabara Mkoa wa Simiyu wakifuatilia hoja mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa katika Kikao Bodi hiyo kilichofanyika leo Mjini Bariadi

Sunday, December 3, 2017

NAIBU WAZIRI TAMISEMI AAGIZA MIKOA YOTE NCHINI KUUNDA KAMATI ZA KUSHUGHULIKIA WATU WENYE ULEMAVU

Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe.Joseph Kakunda ameiagiza mikoa na Halmashauri zote Nchini kuhakikisha kuwa zinaunda Kamati za kushughulikia mahitaji ya watu wenye Ulemavu katika kila Halmashauri, Kata na Vijiji, kabla ya June 30, 2018.

Mhe. Kakunda ametoa agizo hilo wakati wa Maadhimisho ya Kimataifa ya Watu wenye Ulemavu Duniani, yaliyofanyika Kitaifa katika Uwanja wa Halmashauri ya mji Bariadi Mkoani Simiyu.

Amesema Serikali imetenga shilingi milioni 50 kuliwezesha Baraza la wenye Ulemavu Kitaifa kufanya kazi zake kwa mujibu wa Sheria ikiwa ni pamoja na kuhakikisha Kamati zinaundwa hadi ngazi ya vijiji, ili kufanikisha azma hiyo,  amesema lazima ziundwe kamati za kushughulikia wenye ulemavu katika kila Halmashauri, Kata na Vijiji, ambapo ameipongeza mikoa ya Simiyu,, Tabora na Mbeya kwa kukamilisha zoezi hili.

“Naipongeza mikoa ya Simiyu, Tabora na Mbeya kwa kuanzisha kamati hizo katika Halmashauri zao  zote, naagiza Kamati hizo ziundwe katika mikoa yote na katika Halmashauri zote nchini, wale ambao bado hawajakamilisha wakamilishe; tunataka kuona ifikapo tarehe 30 Juni 2018 mikoa yote iwe na kamati hizo” amesisitiza Kakunda.

Mhe.Kakunda pia ameziagiza Halmashauri zote Nchini kuwapa Kipaumbele Wajasiriamali wenye Ulemavu katika utoaji wa Mikopo inayotokana na asilimia 10 ya Mapato ya ndani ili waweze kujipatia mitaji ya kuendeshea shughuli zao mbalimbali za ujasiriamali na kujikwamua kiuchumi.

Ameongeza kuwa Serikali imeandaa utaratibu wa Bima ya Afya kwa watu wote wakiwemo wenye ulemavu ambao ujumuisha upatikanaji wa huduma tengamavu na vifaa saidizi na itaendelea kuagiza na kutoa vifaa hivyo kwa watu wenye ulemavu.

Aidha, amesema Serikali itahakikisha miundombinu inakuwa rafiki na fikivu kwa wenye ulemavu, itaangalia namna bora ya upatikanaji wa ajira kwao,  itawahimiza wamiliki wa vyombo vya habari kutumia wakalimani wa lugha ya alama, kuendelea kuchukua hatua kadi dhidi ya wanaofanya ukatili kwa wenye ualbino, italifanyia kazi suala la ukosefu wa Ofisi kwa ajili ya SHIVYAWATA kwa kuangalia uwezekano wa kushirikisha Halmashauri kutenga Ofisi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa SHIVYAWATA Bi.Ummy Nderininanga akiwasilisha risala ya watu wenye Ulemavu, ametoa mapendekezo kadhaa kwa Serikali na kuomba yafanyiwe kazi ikiwa ni pamoja na watu wenye ulemavu kupatiwa bima za afya,upatikanaji wa ofisi za SHIVYAWATA,  kuongezwa kwa nafasi za ajira kwa watu wenye ulemavu, kutoa mikopo kwa watu wenye ulemavu,kuongeza ulinzi kwa watu wenye ualbino na wanafunzi wa elimu ya juu wenye ulemavu kupewa ruzuku badala ya mikopo, ambayo yote yalitolewa ufafanuzi na Viongozi wa Serikali.

Naye Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anyeshughulikia wenye Ulemavu, Mhe.Stella Ikupa amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeanza  kutoa kipaumbele  na kujumuisha watu wenye ulemavu katika mpango wa ukuzaji ujuzi unaoendeshwa na Ofisi ya Waziri Mkuu  na pia imeanza  kujadili kuona ni jinsi gani mikopo ya elimu ya Juu itatolewa kama ruzuku kwa watu wenye ulemavu.

Akiwasilisha salamu za Mkoa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu  Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Mhe.Festo Kiswaga amesema Mkoa wa Simiyu umeweka utaratibu maalum wa kuwatambua watu wenye ulemavu kuanzia ngazi za vijiji na kubainisha kuwa hadi kufikia mwaka 2017 jumla ya watu 6305 wenye ulemavu mbalimbali wametambuliwa.

Maadhimisho ya Kimataifa ya Watu wenye Ulemavu Duniani, yaliyofanyika Kitaifa katika Uwanja wa Halmashauri ya mji Bariadi Mkoani Simiyu, Kauli Mbiu isemayo , yenye Kauli Mbiu isemayo “BADILIKA TUNAPOELEKEA JAMII ENDELEVU NA IMARA KWA WOTE”  na ni mara ya kwanza kufanyika Mkoani Simiyu.
 
Baadhi ya watu wenye Ulemavu wakiwa katika Maandamano katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji Bariadi wakati wa Maadhimisho ya Kimataifa ya Watu wenye Ulemavu Duniani , yalifanyika Kitaifa katika Uwanja wa Halmashauri ya mji Bariadi Mkoani Simiyu.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe.Joseph Kakunda akizungumza na watu wenye uLemavu na wananchi wa Bariadi Mkoani Simiyu(hawapo pichani), wakati wa Maadhimisho ya Kimataifa ya Watu wenye Ulemavu Duniani, yaliyofanyika Kitaifa katika Uwanja wa Halmashauri ya mji Bariadi Mkoani Simiyu.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Mhe.Stella Ikupa akizungumza na watu wenye uLemavu na wananchi wa Bariadi Mkoani Simiyu(hawapo pichani), wakati wa Maadhimisho ya Kimataifa ya Watu wenye Ulemavu Duniani, yaliyofanyika Kitaifa katika Uwanja wa Halmashauri ya mji Bariadi Mkoani Simiyu
Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Walemavu Tanzania(SHIVYAWATA), Bi. Ummy Nderininanga akizungumza na watu wenye ulemavu na wananchi wa Bariadi Mkoani Simiyu (hawapo pichani), Maadhimisho ya Kimataifa ya Watu wenye Ulemavu Duniani, yaliyofanyika katika Uwanja wa Halmashauri ya mji Bariadi Mkoani Simiyu.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Anthony Mtaka akitoa ufafanuzi juu ya masuala mbalimbali kwa Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe.Joseph Kakunda(kulia) na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Walemavu, Mhe.Stella Ikupa(katikati) walipofika Ofisini kwake kabla ya Maadhimisho ya Kimataifa ya Watu wenye Ulemavu Duniani, yaliyofanyika Kitaifa katika Uwanja wa Halmashauri ya mji Bariadi Mkoani humo.
 Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Ndg.Jumanne Sagini akiwasilisha taarifa ya Mkoa kwa Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe.Joseph Kakunda(hayupo pichani) na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Walemavu, Mhe.Stella Ikupa(kulia) walipofika Ofisini kwa Mkuu wa Mkoa huo,kabla ya Maadhimisho ya Kimataifa ya Watu wenye Ulemavu Duniani , yaliyofanyika Kitaifa katika Uwanja wa Halmashauri ya mji Bariadi Mkoani humo.
Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Ndg.Jumanne Sagini (kushoto) akiwaongoza Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe.Joseph Kakunda(kulia) na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Walemavu, Mhe.Stella Ikupa(katikati) kwenda Wagonjwa waliopata Ajali na kulazwa katika Hospitali Teule ya Mkoa huo, kabla ya Maadhimisho ya Kimataifa ya Watu wenye Ulemavu Duniani, yaliyofanyika Kitaifa katika Uwanja wa Halmashauri ya mji Bariadi Mkoani humo.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe.Joseph Kakunda(hayupo pichani) na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Walemavu, Mhe.Stella Ikupa(kushoto)akimjulia hali mmoja wa Wagonjwa waliopata Ajali na kulazwa katika Hospitali Teule ya Mkoa huo, kabla ya Maadhimisho ya Kimataifa ya Watu wenye Ulemavu Duniani, yaliyofanyika Kitaifa katika Uwanja wa Halmashauri ya mji Bariadi Mkoani humo

Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe.Joseph Kakunda na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Walemavu, Mhe.Stella Ikupa(kushoto) wakizungumza baada ya kuona bidhaa zinazotengenezwa na walemavu, wakati wa Maadhimisho ya Kimataifa ya Watu wenye Ulemavu Duniani, yaliyofanyika Kitaifa katika Uwanja wa Halmashauri ya mji Bariadi Mkoani Simiyu.
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe.Festo Kiswaga akiwasilisha Salamu za Mkoa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka, wakati wa Maadhimisho ya Kimataifa ya Watu wenye Ulemavu Duniani, yaliyofanyika Kitaifa katika Uwanja wa Halmashauri ya mji Bariadi Mkoani Simiyu.

Mmoja wa watu wenye Ulemavu, Bw.Athumani Rubandame aliyepata ulemavu kutokana na ajali za barabarani akitoa ushuhuda juu ya namna ajali za barabarani zinavyochangia ulemavu, Maadhimisho ya Kimataifa ya Watu wenye Ulemavu Duniani, yaliyofanyika Kitaifa katika Uwanja wa Halmashauri ya mji Bariadi Mkoani Simiyu.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe.Joseph Kakunda na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Walemavu, Mhe.Stella Ikupa wakipata maelezo kutoka kwa Viongozi wa watu wenye Ualbino, Maadhimisho ya Kimataifa ya Watu wenye Ulemavu Duniani, yaliyofanyika Kitaifa katika Uwanja wa Halmashauri ya mji Bariadi Mkoani Simiyu.
Baadhi ya Viongozi na Watu wenye Ulemavu wakimsikiliza Mgeni Rasmi katika, Maadhimisho ya Kimataifa ya Watu wenye Ulemavu Duniani, yaliyofanyika Kitaifa Mkoani Simiyu, Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe.Joseph Kakunda(hayupo pichani).

Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Ndg.Jumanne Sagini(katikati) akiteta jambo na Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe.Festo Kiswaga, Mhe.Festo Kiswaga(kulia), katika Maadhimisho ya Kimataifa ya Watu wenye Ulemavu Duniani, yaliyofanyika Kitaifa katika Uwanja wa Halmashauri ya mji Bariadi Mkoani Simiyu. (kushoto) Katibu wa SHIVYAWATA Ndg.Felician Mkude.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe.Joseph Kakunda(wa pili kushoto) akicheza pamoja na watu wenye ulemavu  na baadhi ya viongozi , baada ya kumaliza shughuli za Maadhimisho ya Kimataifa ya Watu wenye Ulemavu Duniani , yaliyofanyika Kitaifa katika Uwanja wa Halmashauri ya mji Bariadi Mkoani Simiyu.
Baadhi ya Viongozi na Watu wenye Ulemavu wakimsikiliza Mgeni Rasmi Maadhimisho ya Kimataifa ya Watu wenye Ulemavu Duniani, ambayo yamefanyika Kitaifa katika Uwanja wa Halmashauri ya mji Bariadi Mkoani Simiyu.Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe.Joseph Kakunda(hayupo pichani).
Baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu wakimsikiliza Mgeni Rasmi katika Maadhimisho ya Kimataifa ya Watu wenye Ulemavu Duniani, yaliyofanyika Kitaifa katika Uwanja wa Halmashauri ya mji Bariadi Mkoani Simiyu, Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe.Joseph Kakunda(hayupo pichani).

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!