Monday, July 24, 2017

RC MTAKA: SIMIYU INAHITAJI USHIRIKA IMARA, WA KISASA KUELEKEA UCHUMI WA KATI

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka  amesema Mkoa huo unahitaji ushirika imara na wa kisasa unaolenga kuwafikisha wananchi katika Uchumi wa kati.

Mtaka amesema  hayo wakati wa uzinduzi wa Jukwaa la Ushirika la Mkoa wa Simiyu uliofanyika katika Ukumbi wa kanisa Katoliki Mjini Bariadi, tukio ambalo limeshirikisha viongozi Serikali na watalaam mbalimbali ngazi ya Mkoa na Wilaya, viongozi wa vyama vya ushirika, Tume ya maendeleo ya Ushirika  na wadau  mbalimbali wa ushirika.

" Sisi kama mkoa tuko tayari  kwa yale ambayo  ninyi wenzetu wa Tume ya Ushirika mnadhani kupitia hayo tutakuwa na ushirika imara na utakaoendeshwa kisasa, tuko tayari hata kwa kuwatoa watu wetu kujifunza katika vyama  vya ushirika vilivyofanikiwa;ushirika wa Tanzania ukiamua Uchumi wa kati inawezekana"

Aidha, Mtaka amesema  wananchi wakielimishwa na kukubali kuungana katika vyama ushirika wanaweza kuondokana na Umaskini,  hivyo amesisitiza uwepo wa ushirika imara wenye matokeo chanya katika maeneo muhimu ya uzalishaji, ili hata mikoa mingine ijifunze Simiyu

"Mwalimu Nyerere amewahi kusema namna pekee ya watu maskini kujikomboa ni kuungana, niwasihi wanaushirika kuunganisha nguvu katika ushirika, matajiri wanaungana kuunda makampuni yanayoweza kukopa, yakashtaki na kushtakiwa ninyi unganeni kwenye vyama vya ushirika kujenga uchumi " amesema Mtaka.

Aidha, Mtaka amesema  Benki ya Maendeleo ya Kilimo(TADB) imekubali kufanya kazi na Mkoa wa Simiyu kwa kuviwezesha vyama vya ushirika na  vikundi vilivyosajiliwa kisheria kwa kuwajengea uwezo wanachama na kuwapa mikopo kwa ajili ya kuendesha miradi mbalimbali, hivyo vyama vya ushirika vinapaswa kuchangamkia fursa hiyo.

Akizungumzia mchango wa ushirika katika utekelezaji wa Kauli Mbiu ya Mkoa"Wilaya Moja Bidhaa Moja Kiwanda Kimoja" Mkuu huyo wa Mkoa amesema vyama vya ushirika ndivyo vyenye wazalishaji wa malighafi ya viwanda, hivyo jukwaa la ushirika litumiwe vizuri katika kuweka mikakati ya kuimarisha vyama vya ushirika na Viongozi wa Serikali wako tayari kuonesha ushirikiano.

Katika hatua nyingine Mtaka amesema mkoa unaandaa andiko linalolenga kuwakusanya wakulima na wanaushirika wote pamoja, ambapo watatumia vyumba vya madarasa katika Shule za Serikali wanafunzi watakapokuwa likizo kupewa mafunzo ya ushirika na kilimo na Wataalam wa Halmashauri, Mkoa na Chuo Kikuu cha Ushirika, ili kuimarisha ushirika na kuongeza tija katika kilimo na mifugo.

Sanjali na hilo Mtaka amesisitiza kuwa mkoa wa Simiyu ndio unaoongoza kwa kulima pamba hapa nchini, hivyo ni vema kukawa na ushirika wenye kuleta majawabu kwa changamoto zinazowakabili wakulima wa pamba kuondoa kero kwa wakulima na kuongeza ubora katika uzalishaji.

Kwa Upande wake Kaimu Naibu Mrajis kutoka Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Ndg.Collins Nyakunga amemshukuru Mkuu  wa Mkoa wa Simiyu kwa kuonesha nia ya kuimarisha ushirika katika mkoa huo na kuona kuwa kupitia ushirika wananchi wanyonge wanaweza kutatua matatizo yao ya kiuchumi na Kijamii.

Nyakunga amesema Tume ya Maendeleo ya Ushirika itaandaa namna ambayo itautoa ushirika katika uendeshaji wa kizamani uendeshwe kisasa, tafiti zitafanyika kupitia Chuo Kikuu cha Ushirika kuona namna ya kuongeza bei, thamani ya zao la pamba na ushirika mkoani Simiyu kuimarika.

Naye Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Simiyu, Ndg Mathias Shineneko amesema Mkoa huo umejiwekea mkakati wa kuakikisha vyama vya ushirika vinajielekeza katika kuweka taratibu za kuongeza  na kuimarisha mitaji, hisa na akiba ili kujiimarisha kiuchumi.

Wakati huo huo Ezekiel Ganji kutoka Chama cha Msingi Sola wilayani  Maswa ameiomba Serikali kuwashirikisha wakulima wa pamba katika maamuzi ya kupanga bei badala ya kupangwa na makampuni yanayonunua pamba na kusisitiza kuwa katika ukaguzi wa vyama vya ushirika Serikali  iangalie uwezo wa vyama hivyo na kupunguza tozo za ukaguzi  kwa kuwa vyama vingi havina uwezo mzuri kifedha
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na wadau wa Ushirika wa Mkoa huo(hawapo pichani) wakati wa Uzinduzi wa Jukwaa la Ushirika la Mkoa huo Mjini Bariadi, (kushoto) ni Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe.Festo Kiswaga

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka(kushoto) akiteta jambo na Kaimu Naibu Mrajis kutoka Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Ndg.Collins Nyakunga wakati wa Uzinduzi wa Jukwaa la Ushirika la mkoa wa Simiyu, Mjini Bariadi

Baadhi ya Wadau wa Ushirika Mkoa wa Simiyu wakifuatilia mada mbalimbali zilizowasilishwa mara baada ya uzinduzi wa Jukwaa la Ushirika la Mkoa huo Mjini Bariadi.
Baadhi ya Wadau wa Ushirika Mkoa wa Simiyu wakifuatilia mada mbalimbali zilizowasilishwa mara baada ya uzinduzi wa Jukwaa la Ushirika la Mkoa huo Mjini Bariadi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na wadau wa Ushirika  wa mkoa huo (hawapo pichani) wakati wa Uzinduzi wa Jukwaa la Ushirika la Mkoa huo Mjini Bariadi.
Afisa Ushirika Mkuu kutoka Tume ya Maendeleo ya Ushirika Sehemu ya Uhamasishaji na utaratibu, Veneranda Mgoba akiwasilisha mada ya Usimamizi na Udhibiti Vyama vya Ushirika kwa wadau wa Ushirika wa Mkoa huo(hawapo pichani) wakati wa Uzinduzi wa Jukwaa la Ushirika la Mkoa huo Mjini Bariadi.
Mwanasheria kutoka Tume ya Maendeleo ya ushirika Kitengo cha Sheria, Donald Deogratius  akiwasilisha mada ya Sheria ya Ushirika kwa wadau wa Ushirika wa Mkoa huo(hawapo pichani) wakati wa Uzinduzi wa Jukwaa la Ushirika la Mkoa huo Mjini Bariadi.

0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!