Thursday, September 22, 2016

SIMIYU YARIDHIA CHAKULA KITOLEWE KWA WANAFUNZI WA SHULE ZA MSINGI NA SEKONDARI ZA KUTWA

Na Stella Kalinga
Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Simiyu (RCC) kimeridhia wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari za Kutwa katika mkoa huo kupata chakula cha mchana shuleni ili kuwatengenezea mazingira mazuri ya kujifunza.

Uamuzi huo umefikiwa kufuatia hoja iliyowasilishwa na Mbunge wa Viti Maalum wa Mkoa wa Simiyu kupitia Chama cha Mapinduzi , Mhe. Leah Komanya juu ya taarifa iliyotolewa na Afisa Elimu Mkoa Mwl. Julius Nestory kuwa takribani asilimia 38 ya wanafunzi katika Mkoa wa Simiyu hawahudhurii masomo kikamilifu.

Mhe. Komanya alisema moja ya sababu inayopelekea wanafunzi kutokwenda shule ni kukosa chakula, hivyo endapo watapata chakula shuleni watashawishika kusoma na muda waliokuwa wanakwenda kutafuta chakula watautumia kwa ajili ya masomo.

Komanya alisema kwa mujibu wa taarifa ya shirika moja la Kimataifa lililofanya utafiti wa athari za mabadiliko ya tabia nchi katika Wilaya ya Meatu,  ilibanishwa kuwa watoto kutoka familia za wanawake wajane zimeathiriwa na uwezo duni, hivyo watoto hawaendi shuleni kwa sababu ya kukosa chakula, hli inayopelekea watoto hao kwenda kujitafutia chakula, jukumu ambalo lingepaswa kufanywa na baba zao .

“Matokeo ya darasa la saba Wilaya ya Meatu mwaka 2015, shule iliyokuwa ya mwisho katika Wilaya ya Meatu ilitoka kata ya Mwamanimba na Kata ya Mwamanimba nilivyofuatilia ni kata iliyofanyiwa tathmini ya athari za mabadiliko ya tabia nchi, kwa hiyo ni wazi kwamba chakula kikipatikana uwezo wa wanafunzi wa kuhudhuria na kuchangia shuleni utakuwa mkubwa” alisema Komanya.

  Mhe.Komanya alisema wazazi kwa umoja wao washirikiane na Serikali katika kuchangia chakula ili kusaidia familia ambazo hazina uwezo wa kuchangia fedha ziweze kutoa mazao ya chakula kwa kuwa wakazi wa Mkoa wa Simiyu walio wengi ni wakulima.

Aidha, Mhe. Komanya ametoa wito kwa mashirika na taasisi mbalimbali kuunga mkono Mkoa wa Simiyu kwa kusaidia kutoa vitu mbalimbali ikiwa ni pamoja na majiko banifu katika shule, nishati itakayotumika kupikia, vyakula na vyombo vya kupikia, ambapo yeye ameahidi kutoa vyombo vya kupikia katika Wilaya zote na akaombaWabunge wote wa Mkoa wa Simiyu wamuunge mkono.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema suala la wazazi kuchangia chakula kwa ajili ya wanafunzi ni la hiari,  hivyo akatoa maelekezo kwa Viongozi Ngazi ya Wilaya kuwafafanulia wananchi ili wawe na uelewa wa pamoja na wafuate taratibu zinazotakiwa kupata vibali vya kuanza kwa zoezi hilo.

Aidha, Mtaka amewatakahadharisha watendajiwa ngazi zote kuhakikisha wanapotoa vibali hivyo kwa Kamati za Shule na Wazazi kuzingatia taratibu ili wanafunzi wapate chakula badala ya kutafuta mianya ya kujinufaisha kwa namna moja au nyingine.


Naye Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega, Mhe. Mickness Mahela amesema anaunga mkono utaratibu wa chakula mashuleni na katika kata yake ya Nyashimo vikao vya Maendeleo ya Kata vimeshakaa na kukubaliana kuanza kutoa chakula kwa wanafunzi, ambapo Shule ya Sekondari Nasa inatarajia kuanza kutoa chakula kwa wanafunzi Novemba Mosi, 2016.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) katika kikao kilichafanyika leo, mjini Bariadi

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka (katikati) akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) katika kikao kilichafanyika leo, mjini Bariadi, (Kushoto )Mwenyekiti wa CCM (M), Dkt. Titus Kamani, (kulia) Katibu Tawala Mkoa Simiyu, Jumanne Sagini
Mbunge waViti Maalum mkoa wa Simiyu (CCM), Mhe. Leah Komanya akizungumza na wandishi wa habari hawapo pichani) mara baada ya kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa kilichofanyika leo Mjini Bariadi.


Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Ushauri wa Mkoa (RCC) wa Simiyu wakifuatilia mijadala mbalimbali katika kikao cha kamati hiyo kilichofanyika leo Mjini Bariadi.

Afisa Elimu wa Mkoa, Julius Nestory akiwasilisha taarifa ya Maendeleo ya Elimu ,  katika  kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa kilichofanyika leo Mjini Bariadi.

Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Ushauri wa Mkoa (RCC) wa Simiyu wakifuatilia mijadala mbalimbali katika kikao cha kamati hiyo kilichofanyika leo Mjini Bariadi.

0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!