Sunday, May 15, 2016

RC SIMIYU AMPA SIKU TANO MTAALAM MSHAURI MRADI WA BARABARA BARIADI MJINI KUWASILISHA MAPITIO YA GHARAMA ZA MRADI(BOQ)



Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka,  ametoa siku tano kwa Mtaalam Mshauri wa Mradi wa Ujenzi wa Barabara za Halmashauri ya Mji wa Bariadi (NOR PLAN) kuwasilisha mapitio ya Mchanganuo wa Gharama (BOQ) ya Ujenzi wa barabara hizo katika Ofisi yake.

Mtaka alitoa agizo hilo jana wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa miradi ya ujenzi wa barabara aliyoifanya katika Halmashauri ya Mji Bariadi, akiambatana na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Bariadi.

 Mtaka alisema ipo haja kwa Uongozi wa Mkoa kuona mapitio hayo ili Ofisi ya Mkoa na watendaji wengine wayapitie na kuona kama kuna vitu ambavyo si vya msingi au vyenye gharama kubwa wamshauri Mtaalam mshauri na Mkandarasi kuviondoa ili kupunguza gharama ya mradi huo uliopangwa kutekelezwa kwa shilingi bilioni 9.1 kwa kilomita 6.

“Katibu Mkuu TAMISEMI alipokuja alikuagiza ufanye review ya BOQ na akataka uanishe kiasi gani cha fedha kitaokolewa . Nakala hiyo tunapaswa tuipate sisi kama viongozi wa mkoa, naagiza uilete hiyo review Ijumaa saa 4:00 asubuhi, halafu  Katibu Tawala Mkoa atakaa na Wataalam wa Sekretarieti  na wadau wengine ambao kwa pamoja watashauri nini kifanyike”alisema Mtaka.

Aidha, baada ya Mhandisi wa Mkandari wa Mradi, Jassie And Company Ltd (JASCO), Ndg. Daniel Nila kueleza kuwa gharama za ujenzi wa barabara hizo zilipangwa kuwa shilingi bilioni 1.3 kwa kilomita moja,  kutokana na barabara hiyo kupangwa kujengwa kwa hadhi ya barabara ya uwanja wa ndege; Mkuu wa mkoa aliwashauri kuangalia mazingira ya Mji wa Bariadi na kujenga barabara inayoendana na mazingira ili kupunguza gharama zisizo za lazima.

Sanjari na hilo Mkuu wa mkoa alitoa wito kwa Wakandarasi wazawa wanaopewa dhamana ya kutekeleza miradi ya Serikali, kuweka uzalendo mbele na kutekeleza miradi kwa kiwango.

Kwa upande wake Mhandisi Victor Malya kutoka Kampuni ya NOR PLAN (Mtaalam Mshauri wa Mradi), alisema tangu Mradi wa ujenzi wa barabara za Mji Bariadi uanze kutekelezwa mwezi Agosti, 2015 hadi sasa umetekelezwa kwa asilimia 50, ulitarajiwa kukamilishwa mwezi Agosti 2016  lakini kutokana na sababu mbalimbali ikiwepo mvua kubwa iliyonyesha mwezi Novemba na Desemba mradi huo hautaweza kukamilika ndani ya muda uliopangwa katika mkataba.

Pamoja na maelezo hayo kutoka kwa Mhandisi Malya, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu alimtaka Mkandarasi wa mradi huo  (JASCO) kuongeza kasi ya utekelezaji  kufikia mwezi Oktoba mradi uwe umetekelezwa kwa asilimia kubwa ili barabara hizo zikatumiwe na viongozi na wananchi wakati wa maadhimisho ya Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2016, kwa sababu kama zitakuwa  zimefungwa kama ilivyo sasa  zitasababisha usumbufu.
Mkuu wa mkoa wa Simiyu Mhe. Anhony J. Mtaka (wa kwanza kulia) akimsikiliza Mhandisi wa Ujenzi wa Sekretarieti ya Mkoa, Deusdedit Mshuga akitoa maelezo na kuonesha mapungufu aliyoyaona katika barabara ya Muungano-Malambo iliyojengwa na Mkandarasi Mzawa GAT Engineering, wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya Barabara mjini Bariadi.




Tuesday, May 10, 2016

RC SIMIYU APIGA MARUFUKU DAGA SHIDA



Mkuu wa Simiyu Mhe. Anthony J. Mtaka amepiga marufuku tabia ya viongozi wa kimila kuwaadhibu wananchi  wanaobanika kuwa kuwa na makosa kupita mabaraza ya kimila maaarufu  kama DAGA SHIDA na badala yake amewataka  watumie vyombo vya Serikali vinavyotambulika kisheria.

Mtaka alitoa agizo hilo alipozungumza na wananchi wa kijiji cha Ikindilo kata ya Ikindilo tarafa ya Bumela wilayani Itilima, ambapo ameitaka Kamati ya Ulinzi na Usalama wilayani Itilima, kulisimamia suala hilo kwa kuwa limekuwa likiwadharirisha wananchi na wale watakaobainika kukaidi agizo hilo, wafikishwe kwenye vyombo vya sheria na kuchukuliwa hatua.

“Mkuu wa Wilaya na wajumbe wako kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya, simamieni suala hili na mhakikishe linakomeshwa kabisa. Naagiza  hili kwa mkoa mzima sitaki kusikia kitu kinachoitwa daga shida. Hatuwezi kuacha wananchi wanateseka, watumishi wetu tunaowaleta kuwatumikia wananchi nao wanateseka na mifumo kandamizi kama hii wakati vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vipo”alisema Mtaka 

Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa aliwataka wananchi watakaoitwa kwa ajili ya kwenda kuadhibiwa na viongozi wa mabaraza ya kimila maarufu kama Sumbantale wasikubali na wawatake viongozi hao wa kimila kuwashtaki  katika ofisi za Serikali au katika Vituo vya polisi ikiwa watajiridhisha kuwa wana makosa.
Mfumo wa daga shida umekuwa ukitumwa katika maeneo mengi mkoani Simiyu, ambapo wananchi  hususani watumishi wa umma wamekuwa wakiadhibiwa na viongozi wa kimila kwa kuwataka kulipa faini ya fedha , mazao, wanyama  na kupigwa pale wanapoonekana kwenda kinyume na matakwa yao ya kimila na wakati mwingine wamekuwa wakizushiwa .

Wakati huo huo Mtaka amewataka  wazazi na walezi kuacha mara moja tabia ya  kuwakatisha masomo watoto wao wa kike na kuwaozesha kwa kuwa wakiendelea kufanya hivyo watachukuliwa hatua kali za kisheria.

“Ole wake mzazi au mlezi atakayemtoa mtoto shule  na akaenda kumuozesha,ajue ameamua kuhamishia maisha yake toka nyumbani kwenda jela, hilo halina mjadala. Mtoto wa shule ni wako kwa kuwa umemzaa lakini akiwa shule toka darasa la kwanza  mpaka kidato cha sita ni mali ya serikali” alisema Mtaka.

WAKAZI WA ITILIMA WAISHUKURU LIFE MINISTRY KUWACHIMBIA KISIMA



Wakazi wa kijiji cha Ikindilo wilayani Itilima wamelishukuru Shirika la dini la Life Minisry kwa kuwatoa katika adha ya maji iliyokuwa ikiwakabili kwa kuwachimbia kisima kirefu chenye thamani ya shilingi milioni 50.

Akizungumza mara baada ya uzinduzi wa kisima hicho uliofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony . J. Mtaka , mkazi wa kijiji cha Ikindilo bibi . Monica Malugu alisema kisima hicho kimewasadia kuondokana na ashida ya kufuata maji kwa mwendo mrefu.

“Nawashukuru sana wafadhili kwa kutukumbuka wana Ikindilo kwa kutuchimbia kisima hiki, tulikuwa tunafuata mbali yaani tulikuwa tunatembea zaidi ya masaa matatu. Tulikuwa tunaamka usiku kwenda kufuata maji  na wakati mwingine tukichelewa kurudi tunapigwa na waume zetu” alisema Bibi Monica.

Akitoa shukrani kwa niaba ya Serikali, Mkuu wa mkoa wa Simiyu amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango wa mashirika ya dini katika maendeleo ya nchi ya Tanzania na watu wake na akaahidi kuulinda mradi huo na miradi mingine ya Life Ministry inayotekelezwa katika mkoa wa Simiyu.

Aidha, Mtaka alisema wafadhili kama hao wamekuwa wadau wakubwa wa maendeleo tangu uhuru hivyo  aliwahakikishia kuwa watapata ushirikiano wa kotosha kutoka kwa Viongozi wa Serikali ngazi ya kijiji hadi Mkoa pale watakapohitaji  kutekeleza miradi mingine ya maendeleo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Life Ministry Tanzania Bw.Dismas Shekalaghe aliwataka wakazi wa Ikindilo kukilinda na kukitunza kisima hicho na miundombinu yake ili kiwanufaishe kwa kuwapa huduma  ya maji safi iliyo endelevu, ambapo walaihidi kukifanyia ukarabati kila baada ya mwaka mmoja.
Shirika la Life Ministry linafanya kazi katika nchi zaidi ya 198 duniani, Pamoja na kuchimba visima vitatu katika mkoa wa Simiyu wanatarajia  kuwasaidia wananchi  katika maeneo mengine,  hususani kilimo cha mboga mboga ili kuwakwamua katika umasikini.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka  (katikati) akikata utepe wakati wa uzinduzi wa kisima kilichochimbwa na shirika la dini la Life Ministry kwa ajili ya wakazi wa Ikindilo wilayani Itilima, kushoto kwake ni Mkurugenzi wa Shirika la Life Ministry Bw. Dismas Shekalaghe na kulia kwake ni Diwani wa kata ya Ikindilo, Mhe.Joseph Kulwa. Picha na Stella Kalinga


 Mkurugenzi wa Shirika la Life Ministry Bw. Dismas Shekalaghe (kulia) akizungumza na wananchi wa Ikindilo (hawapo pichani) kabla ya uzinduzi wa kisima cha maji, wa pili kulia Mkuu wa mkoa wa Simiyu akifatiwa na Mkuu waWilaya ya Itilima Mhe. Georgiina Bundala.



Thursday, May 5, 2016

RC SIMIYU AAGIZA KAMATI YA ULINZI NA USALAMA YA WILAYA BARIADI KUMPA TAARIFA YA MIRADI YA MAJI




Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka ameiagiza  Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Bariadi kumpelekea taarifa ya miradi ya maji inayotiliwa shaka ya kujengwa chini ya kiwango, ndani ya siku tano kuanzia tarehe 04.05.2016.

Mtaka alitoa agizo hilo jana alipokuwa akizungumza na viongozi na watendaji  katika kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, katika Ukumbi wa Kanisa Katoliki Bariadi.

 “Siwezi kuvumilia na kuendelea kuona fedha za Serikali zinazotolewa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji na miradi mingine kwa ajili ya maendeleo ya wananchi zinatumika vibaya au miradi ya maendeleo kutekelezwa chini ya kiwango. DC na Kamati yako ya Ulinzi na Usalama nataka uniletee taarifa ya miradi yote ya maji katika wilaya ya Bariadi inayotiliwa shaka ya kutekelezwa chini ya kiwango,Jumatatu asubuhi, ili tuchukue hatua” alisema Mtaka.

Mtaka aliwataka  viongozi na watendaji kila mmoja kutimiza wajibu wake katika kusimamia na kuhakikisha miradi yote ya Serikali inatekelezwa kwa kiwango,  kulingana na thamani ya fedha ili iweze kuleta manufaa kwa wananchi.

Aidha, Mkuu wa Mkoa alisema hatasita kumchukulia hatua mtu yeyote atakayebainika kuhusika kwa namna moja ama nyingine katika utekelezaji wa miradi hiyo chini ya kiwango hata kama ni kada wa Chama Tawala, kwa sababu amedhamiria kutekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi ambacho kimeaminiwa na kupewa ridhaa ya kuongoza nchi na wananchi wenyewe, ambapo aliahidi atasimamia ipasavyo ili wananchi waendelee kukiamini Chama cha Mapinduzi na Serikali yake.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony J.Mtaka (wa pili kulia) akizungumza na madiwani na watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi (hawapo pichani) katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika katika Ukumbi wa Kanisa Katoliki Bariadi

Sunday, May 1, 2016

MPINA ATAKA VIONGOZI WANAOSHINDWA KUSIMAMIA USAFI WAWAJIBISHWE



Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira, Mhe. Luhaga Mpina amewataka Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa wilaya kuwachukulia hatua viongozi wanaoshindwa kusimamia utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Magufuli la kufanya usafi wa Mazingira kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi.

Mhe. Mpina aliyasema hayo alipozungumza na viongozi na wananchi mara baada ya kushiriki kufanya usafi katika kituo cha Afya cha Mwandoya wilayani Meatu, zoezi ambalo lilienda sambamba na uzinduzi wa upandaji wa miti ya matunda katika mkoa wa Simiyu, ambapo Mkoa wa Simiyu umepokea jumla ya miche 18, 400 ya miembe na michungwa kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais.

Mpina alisema viongozi kuanzia ngazi ya Vijiji hadi Mkoa wanao wajibu wa kusimamia usafi wa mazingira katika maeneo yao, kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi kwa kuhakikisha wananchi wanafanya usafi kuanzia saa 12:00 hadi saa 3:00 asubuhi, ikiwa kuna wananchi watakaobainika kushindwa kutekeleza agizo hilo wachukuliwe hatua.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Mhe. Pius Machungwa alisema viongozi wa Wilaya ya Meatu na mkoa wa Simiyu kwa ujumla wataendelea kuunga mkono juhudi za serikali katika kuhakikisha shughuli za usafi na utunzaji wa mazingira zinaendelezwa.

Wakati huo huo Mhe. Mpina amewahimiza wananchi kupanda miti yenye manufaa , hususani miti ya mbao na matunda kwa sababu itawasidia kupata fedha, chakula na malighafi kwa ajili ya viwanda mbalimbali nchini na hivyo kuinua uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu , Bw. Joseph S. Nandrie alikiri mkoa kupokea jumla ya miche ya miembe na machungwa 18,400 ambayo imeshasambazwa katika Halmashauri zote sita na akaahidi kuifuatilia miti hiyo na kuhakikisha inatunzwa.

Aidha Mpina alieleza azma ya Serikali katika kuhakikisha miti inapandwa nchi nzima ili kurejesha uoto wa asili uliopotea, kuongeza uwezo wa kunyonya hewa ya ukaa ambayo imeongezeka duniani kote kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.
“Tumeandaa Mpango wa kitaifa wa upandaji wa miti, na kwa kuanzia tumetenga shilingi bilioni 20 kwa mwaka kwa ajili ya upandaji miti nchi nzima, kwa kupanga huko tunataka kila wilaya iwe na kitalu kikubwa cha miti inayoandaliwa kwenda kwa wananchi kwa urahisi. Tunataka kufikia mwaka 2020 watu wakose mahali pa kupanda miti kwa kuwa kila mahali patakuwa na miti” alisema Mpina.

Mhe. Mpina alitoa miche hiyo 18,400 kwa Mkoa wa Simiyu ikiwa ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa wakati wa ziara ya Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa , aliyoifanya Mkoani Simiyu mapema mwezi Machi, 2016 na ameahidi kuongeza miche hadi kufikia 30,000. 
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mhe. Luhaga J. Mpina akishiriki kufanya usafi pamoja viongozi na wanachi katika eneo la Kituo cha Afya cha Mwandoya, wilaya ya Meatu mkoani Simiyu Aprili 30 mwaka huu, ikiwa ni utekelezaji wa Agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, la kufanya usafi wa mazingira kila Jumamosi ya Mwisho wa mwezi. Picha Na Stella A. Kalinga

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mhe. Luhaga J. Mpina akipanda mti wa mwembe katika kijiji cha Mwandoya wilayani Meatu, wakati wa uzinduzi wa zoezi la upandaji miti 18,400 ya michungwa na miembe iliyotolewa na Ofisi Makamu wa Rais kwa Mkoa wa Simiyu, zoezi hili lilifanyika baada ya kukamilisha usafi wa mazingira katika Kitua cha Afya cha Mwandoya, Meatu. Picha na Stella A. Kalinga


Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!