Mkuu wa
Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) nchini Brigedia Jenerali Charles Mbuge
amesema kuwa baadhi ya wazabuni wanaouza vifaa vya ujenzi wamekuwa wakiuza
vifaa kwa bei ya juu na kuchelewesha vifaa hivyo pale vinapohitajika, jambo
linalopelekea baadhi ya miradi inayotekelezwa na Shirika la Uzalishaji Mali la
Jeshi hilo (SUMA JKT) kutokamilika kwa wakati.
Brigedia
Jenerali Mbuge ameyasema hayo Februari 13, 2020 mjini Bariadi wakati akiwa
katika ziara ya kukagua miradi ya ujenzi inayotekelezwa na SUMA JKT mkoani
Simiyu.
Ameongeza
kuwa katika kukabiliana na changamoto hiyo, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limejipanga
kuanzisha maduka ya vifaa vya Ujenzi vitakavyouzwa kwa bei ya jumla ili kuwezesha upatikanaji wa vifaa kwa
urahisi, haraka na kwa bei nafuu ikilinganishwa na wazabuni wengine.
“Tatizo
moja ninaloliona kwenye utekelezaji wa miradi ni vifaa kuuzwa kwa bei ya juu
sana na kucheleweshwa, tumeamua kuwa na maduka
ya vifaa ya jumla; tutatoa maelekezo kwa wakuu wa kanda za ujenzi watatupatia
mahitaji yao, ili kuwawezesha kufanya kazi kwa wakati kama tunavyokubaliana na
washitiri wetu,” alisema Brigedia Jenerali Mbuge.
Katika
hatua nyingine Brigedia Jenerali Mbuge amesema jeshi hilo litaendelea kuwatumia
vijana watakaomaliza mafunzo ya JKT katika shughuli zilizopo kwenye miradi
inayotekelezwa na Jeshi hilo lengo likiwa kuwawezesha vijana hao kupata kipato na
baadaye waweze kujiajiri badala ya kutegemea kuajiriwa pekee.
Vile vile ameahidi
kuongeza nguvu kazi ya vijana katika mradi inayotekelezwa na SUMA JKT mkoani
Simiyu kuongeza kasi na miradi hiyo iweze kukamilika kwa muda uliopangwa, huku
akitoa wito kwa Taasisi mbalimbali kuipa kazi SUMA JKT, ili iendelee kuwa kutoa gawio kubwa kwa
Serikali, ambapo amesema mwaka 2018/2019 ilitoa zaidi ya shilingi bilioni moja
na mwaka 2019/2020 linatarajia kupanda zaidi kutokana na uwepo wa vyanzo vya
kutosha.
Awali
akitoa taarifa, Katibu Tawala Msaidizi Seksheni ya miundombinu katika ofisi ya
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, mhandisi Mashaka Luhamba amesema JKT wanatekeleza
miradi minne mkoani Simiyu ukiwemo wa ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa,
wodi ya wazazi Hospitali ya Rufaa ya mkoa, ujenzi jengo la wizara ya
kilimo linalojengwa kwenye viwanja vya maonesho ya Nane nane pamoja na
kiwanda cha Chaki Maswa ( Maswa chalk) .
Aidha
mhandisi huyo amebainisha kuwa ujenzi wa jengo la Mkuu wa Mkoa unatekelezwa kwa
kipindi cha miezi 18 kwa gharama ya shilingi bilioni 5.7 ambapo ujenzi
rasmi ulianza mwezi Mei, 2019 na endapo fedha zitapatikana kwa wakati unatarajiwa
kukamilika Novemba, 2020.
Kwa upande
wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema ni vema SUMA JKT
ikahuisha uharaka wa kutekeleza miradi kama jamii inavyoutarajia kwa kuwa jamii
na Serikali imejenga imani kubwa kwa JKT kutekeleza miradi kwa wakati ikilinganishwa
na wakandarasi wengine.
Mtaka
ameongeza kuwa miradi inayotekelezwa na SUMA JKT iwe fursa kwa vijana waliopata
mafunzo ya JKT na kumaliza mikataba yao ili waweze kupata kipato kitakachowasaidia
kwenda kujitegemea na kujiajiri endapo hawataajiriwa.
MWISHO
Katibu Tawala Msaidizi seksheni ya Miundombinu katika Ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhandisi Mashaka Luhamba akitoa maelezo ya hali ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi inayotekelezwa na SUMA JKT Mkoani Simiyu kwa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa nchini Brigedia Jenerali Charles Mbuge , wakati wa ziara ya Mkuu huyo wa JKT Mkoani humo Februari 13, 2020 yenye lengo la kukagua miradi mbalimbali ya ujenzi inayotekelezwa na SUMA JKT.
Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa nchini (JKT), Brigedia Jenerali Charles Mbuge(wa nne kulia) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa Mkoa wa Simiyu wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Anthony Mtaka (wa nne kushoto), wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa na baadhi ya Maafisa wa jeshi hilo waliofuatana naye katika ziara ya kukagua miradi ya ujenzi inayotekelezwa na SUMA JKT Mkoani Simiyu Februari 13, 2020.
Meneja wa SUMA JKT Kanda ya Ziwa Kapteni Fabian Buberwa(kulia) akitoa maelezo ya hali ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa jengo la Wizara ya Kilimo katika Uwanja wa Nanenane Mjini Bariadi mkoani Simiyu kwa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa nchini(JKT), Brigedia Jenerali Charles Mbuge(wa pili kushoto), wakati wa ziara yake Februari 13, 2020 ya kukagua miradi inayotekelezwa na SUMA JKT Mkoani Simiyu
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka (kulia) akiwa na Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa(JKT), Brigedia Jenerali Charles Mbuge alipompokea mara baada ya kuwasili Mjini Bariadi kwa lengo la kufanya ziara ya kukagua miradi ya ujenzi inayotekelezwa na SUMA JKT Mkoani humo, iliyofanyika Februari 13, 2020.
Mkuu wa Jeshi la
Kujenga Taifa nchini (JKT), Brigedia
Jenerali Charles Mbuge akizungumza na baadhi ya viongozi wa Mkoa wa Simiyu na
watendaji wa Jeshi mara baada ya kukagua
mradi wa Ujenzi wa Jengo la wodi ya wazazi unaoendela katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa
wa Simiyu Mjini Bariadi, wakati wa ziara yake Mkoani humo Februari 13,
2020 yenye lengo la kukagua miradi
mbalimbali ya ujenzi inayotekelezwa na Shirika la Uzalishaji mali la JKT(SUMA
JKT).
0 comments:
Post a Comment