Thursday, May 5, 2016

RC SIMIYU AAGIZA KAMATI YA ULINZI NA USALAMA YA WILAYA BARIADI KUMPA TAARIFA YA MIRADI YA MAJI




Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka ameiagiza  Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Bariadi kumpelekea taarifa ya miradi ya maji inayotiliwa shaka ya kujengwa chini ya kiwango, ndani ya siku tano kuanzia tarehe 04.05.2016.

Mtaka alitoa agizo hilo jana alipokuwa akizungumza na viongozi na watendaji  katika kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, katika Ukumbi wa Kanisa Katoliki Bariadi.

 “Siwezi kuvumilia na kuendelea kuona fedha za Serikali zinazotolewa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji na miradi mingine kwa ajili ya maendeleo ya wananchi zinatumika vibaya au miradi ya maendeleo kutekelezwa chini ya kiwango. DC na Kamati yako ya Ulinzi na Usalama nataka uniletee taarifa ya miradi yote ya maji katika wilaya ya Bariadi inayotiliwa shaka ya kutekelezwa chini ya kiwango,Jumatatu asubuhi, ili tuchukue hatua” alisema Mtaka.

Mtaka aliwataka  viongozi na watendaji kila mmoja kutimiza wajibu wake katika kusimamia na kuhakikisha miradi yote ya Serikali inatekelezwa kwa kiwango,  kulingana na thamani ya fedha ili iweze kuleta manufaa kwa wananchi.

Aidha, Mkuu wa Mkoa alisema hatasita kumchukulia hatua mtu yeyote atakayebainika kuhusika kwa namna moja ama nyingine katika utekelezaji wa miradi hiyo chini ya kiwango hata kama ni kada wa Chama Tawala, kwa sababu amedhamiria kutekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi ambacho kimeaminiwa na kupewa ridhaa ya kuongoza nchi na wananchi wenyewe, ambapo aliahidi atasimamia ipasavyo ili wananchi waendelee kukiamini Chama cha Mapinduzi na Serikali yake.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony J.Mtaka (wa pili kulia) akizungumza na madiwani na watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi (hawapo pichani) katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika katika Ukumbi wa Kanisa Katoliki Bariadi

Sunday, May 1, 2016

MPINA ATAKA VIONGOZI WANAOSHINDWA KUSIMAMIA USAFI WAWAJIBISHWE



Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira, Mhe. Luhaga Mpina amewataka Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa wilaya kuwachukulia hatua viongozi wanaoshindwa kusimamia utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Magufuli la kufanya usafi wa Mazingira kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi.

Mhe. Mpina aliyasema hayo alipozungumza na viongozi na wananchi mara baada ya kushiriki kufanya usafi katika kituo cha Afya cha Mwandoya wilayani Meatu, zoezi ambalo lilienda sambamba na uzinduzi wa upandaji wa miti ya matunda katika mkoa wa Simiyu, ambapo Mkoa wa Simiyu umepokea jumla ya miche 18, 400 ya miembe na michungwa kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais.

Mpina alisema viongozi kuanzia ngazi ya Vijiji hadi Mkoa wanao wajibu wa kusimamia usafi wa mazingira katika maeneo yao, kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi kwa kuhakikisha wananchi wanafanya usafi kuanzia saa 12:00 hadi saa 3:00 asubuhi, ikiwa kuna wananchi watakaobainika kushindwa kutekeleza agizo hilo wachukuliwe hatua.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Mhe. Pius Machungwa alisema viongozi wa Wilaya ya Meatu na mkoa wa Simiyu kwa ujumla wataendelea kuunga mkono juhudi za serikali katika kuhakikisha shughuli za usafi na utunzaji wa mazingira zinaendelezwa.

Wakati huo huo Mhe. Mpina amewahimiza wananchi kupanda miti yenye manufaa , hususani miti ya mbao na matunda kwa sababu itawasidia kupata fedha, chakula na malighafi kwa ajili ya viwanda mbalimbali nchini na hivyo kuinua uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu , Bw. Joseph S. Nandrie alikiri mkoa kupokea jumla ya miche ya miembe na machungwa 18,400 ambayo imeshasambazwa katika Halmashauri zote sita na akaahidi kuifuatilia miti hiyo na kuhakikisha inatunzwa.

Aidha Mpina alieleza azma ya Serikali katika kuhakikisha miti inapandwa nchi nzima ili kurejesha uoto wa asili uliopotea, kuongeza uwezo wa kunyonya hewa ya ukaa ambayo imeongezeka duniani kote kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.
“Tumeandaa Mpango wa kitaifa wa upandaji wa miti, na kwa kuanzia tumetenga shilingi bilioni 20 kwa mwaka kwa ajili ya upandaji miti nchi nzima, kwa kupanga huko tunataka kila wilaya iwe na kitalu kikubwa cha miti inayoandaliwa kwenda kwa wananchi kwa urahisi. Tunataka kufikia mwaka 2020 watu wakose mahali pa kupanda miti kwa kuwa kila mahali patakuwa na miti” alisema Mpina.

Mhe. Mpina alitoa miche hiyo 18,400 kwa Mkoa wa Simiyu ikiwa ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa wakati wa ziara ya Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa , aliyoifanya Mkoani Simiyu mapema mwezi Machi, 2016 na ameahidi kuongeza miche hadi kufikia 30,000. 
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mhe. Luhaga J. Mpina akishiriki kufanya usafi pamoja viongozi na wanachi katika eneo la Kituo cha Afya cha Mwandoya, wilaya ya Meatu mkoani Simiyu Aprili 30 mwaka huu, ikiwa ni utekelezaji wa Agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, la kufanya usafi wa mazingira kila Jumamosi ya Mwisho wa mwezi. Picha Na Stella A. Kalinga

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mhe. Luhaga J. Mpina akipanda mti wa mwembe katika kijiji cha Mwandoya wilayani Meatu, wakati wa uzinduzi wa zoezi la upandaji miti 18,400 ya michungwa na miembe iliyotolewa na Ofisi Makamu wa Rais kwa Mkoa wa Simiyu, zoezi hili lilifanyika baada ya kukamilisha usafi wa mazingira katika Kitua cha Afya cha Mwandoya, Meatu. Picha na Stella A. Kalinga


Sunday, April 24, 2016

RC SIMIYU: WATENDAJI MWIBA HOLDINGS LIMITED, MARUFUKU KUWAHOJI WANANCHI KATIKA OFISI ZAO





Mkuu  wa mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony J. Mtaka amepiga marufuku tabia ya askari na watendaji  wengine wa  mwekezaji MWIBA Holdings  Limited wa Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori (WMA) Makao wilayani Meatu, ya kuwakamata wananchi na kuwafanyia mahojiano katika Ofisi zao , na kuwataka kufuata sheria na kukitumia kituo cha polisi cha Makao kufanya mahojiano.

Mwenyekiti wa kijiji cha Makao na Diwani wa kata ya Mwangudo Mhe. .Anthony Philipo (kushoto) akiwasilisha malalamiko yake dhidi ya Mwekezaji MWIBA Holdings kwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony J. Mtaka (kulia) katika mkutano wa hadhara ambao ulifanyika katika kijiji cha Makao  hivi karibuni. Picha na Stella Kalinga
Mkuu wa Mkoa aliyasema hayo jana alipozungumza na wananchi wa kijiji cha Makao kata ya Mwangudo wilayani Meatu katika mkutano wa hadhara, mara baada ya kusikiliza malalamiko ya wananchi hao dhidi ya Mwekezaji MWIBA Holdings Limited, ikiwemo unyanyasaji wa wananchi, kukiukwa kwa makubaliano ya mikataba ya utwaaji ardhi na mkataba wa uanzishwaji wa Lanchi.

Akiwasilisha malalamiko yake kwa Mkuu wa Mkoa mmoja wa wananchi wanaodaiwa  kupigwa na kufanyiwa vitendo vya unyanyasaji  katika ofisi za MWIBA Holdings Limited, Bibi. Asteria Godson mkazi wa kijiji cha Makao alisema, alichukuliwa nyumbani kwake na kupelekwa katika moja ya ofisi za mwekezaji huyo ambako alipigwa na kusababishiwa maumivu makali na kuvunjika mkono wa kulia ambao hadi sasa hata baada ya kupata matibabu, bado hauwezi kufanya kazi sawasawa.

“Mimi nilikuwa nimelala ndani kwangu wakaingia watu ambao sikuweza kuwatambua wakitaka niwaeleze mahali alipo mume wangu, nikawaambia mume wangu hayupo wakaanza kunipiga, walinipiga baadae wakanichukua mpaka ofisi za MWIBA huko nako walinipiga na kunifanyia vitendo vingi vya unyanyasaji. Kutokana na kile kipigo sasa hivi mkono wangu mmoja haufanyi kazi”alisema Asteria.

 Akipokea maelekezo ya Mkuu wa Mkoa, Afisa  Uhusiano wa MWIBA Holdings Limited Bwana Msafiri Clarenes alisema wamekubali na watatekeleza kama ilivyoelekezwa, ambapo alimuomba Mkuu wa Mkoa atoe maelekezo kwa wananchi wa Mako kuacha kuchungia mifugo katika eneo la uwekezaji.

Katika kukabiliana na tatizo la eneo la malisho ya mifugo, Mtaka alisema Serikali iliweka mpango wa matumizi bora ya ardhi ambao unaeleza kuwa litatengwa eneo maalum kwa ajili ya machungo ambalo litatumika kipindi ambacho majani yatakuwa yamepungua kuanzia mwezi Julai hadi mvua zitakapoanza kunyesha.

Akitoa ufafanuzi juu ya eneo la kulishia mifugo Afisa Ardhi wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu Bwana Emmanuel Lugamila alisema, eneo hilo lipo ndani ya Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori (WMA) Makao na linatarajiwa kuwekewa alama za kudumu mwezi Juni,2016 ili wananchi waweze kulitambua.

Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa amewaasa wananchi kuachana na tabia ya kupangisha mifugo ambayo ni maarufu katika Maeneo hayo kama LUBAGA, kwa kuwa ni chanzo cha migogoro kati ya wafugaji, badala yake viongozi wa vijiji wawatambue watu wenye mifugo katika maeneo yao na kuepuka kwenda katika maeneo ambayo hawaruhusiwi kuchungia.

Wananchi wa kijiji cha Makao wamekuwa na Mgogoro wa kimkataba na Mwekezaji MWIBA Holdings Limited ambao  unaendelea kutafutiwa suluhu kwa mujibu wa sheria.   

Tuesday, April 12, 2016

ASKARI POLISI WANAOKIUKA MAADILI YA JESHI WAWAJIBISHWE




Viongozi wa jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu wameaswa kuwawajibisha askari polisi watakaokiuka maadili ya kazi yao ikiwemo kutoa siri za jeshi la polisi kwa wahalifu.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony John Mtaka alipozungumza na Viongozi na Askari wa Jeshi la Polisi Mkoani Simiyu jana,  katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari Bariadi Mjini Bariadi, katika kikao cha kujitambulisha na kutoa maelekezo ya Serikali kwa Jeshi la polisi.

Mtaka amesema viongozi hao wasisite kuwawajibisha askari watakaoonekana kuvujisha siri za jeshi hilo kwa kuwa kufanya hivyo kunalifedhehesha Jeshi la Polisi.

“Hatuwezi kukukubali kudhalilisha taaluma ya jeshi la polisi, hivi askari anayetoa siri za jeshi OCD unamwangalia wa nini, hii ni fedheha. Jeshi la Polisi linaonekana la ovyo kwa sababu ya askari wachache wasiotaka kutii  na kufuata maadili; raia anashindwa kutoa taarifa katika chombo cha dola kwa sababu anaogopa chombo cha dola kitamuuza, aibu hii haivumiliki wachukulieni hatua” alisema Mtaka.

Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa  amewataka viongozi wa Jeshi la Polisi kufanya kazi kwa bidii na kusimamia haki ili askari watekeleze majukumu yao  sawa sawa.

Pamoja na kuwaasa Mtaka alitoa pongezi kwa jeshi la polisi kwa kazi nzuri inayoendelea kufanyika katika maeneo tofauti ya mkoa wa Simiyu ikiwa ni pamoja na kufanikiwa kuwakamata majangili waliotungua helikopta wilayani Meatu ,kufanya oparesheni za kuteketeza mashamba ya bangi na kazi nyingine za ulinzi na usalama wa raia na mali zao.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, ASP. Onesmo Lyanga, alisema hatasita kuwachukulia hatua viongozi  na askari wa jeshi la polisi wababaishaji, hivyo akawataka wafanye kazi zao kwa bidii.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mh. Anthony J. Mtaka (wa pili Kushoto) akizungumza na viongozi na Askari wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu (hawapo pichani) jana mjini Bariadi, kulia kwake (wa kwanza) ni Kamanda wa Polisi Mkoa. Onesmo Lyanga.




Thursday, April 7, 2016

BARAZA LA USHAURI LA WATUMIA HUDUMA ZA EWURA LAZINDULIWA RASMI MKOANI SIMIYU


Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony J.  Mtaka  jana amezindua  Kamati ya Mkoa ya Baraza la  Ushauri  la Watumiaji wa Huduma zinazodhibitiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishati (EWURA) ya mkoa huo.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony John Mtaka (wa pili kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Wadau wa Huduma za Nishati , Viongozi wa Serikali na Wajumbe wa Kamati ya Baraza la Ushauri la Watumia huduma za Nishati na Maji la Mkoa wa Simiyu iliyozinduliwa Aprili 06,2016. ( wa kwanza kulia ) ni Katibu Tawala Mkoa, Bibi Mwamvua A. Jilumbi. Picha na Stella Kalinga

Akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Baraza hilo na wadau walioshiriki katika hafla ya uzinduzi , iliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mtaka alisema kamati ya baraza hilo inapaswa kuhakikisha inakuwa mstari wa mbele katika kutetea maslahi ya watumiaji wa huduma za nishati na maji, hasa upatikanaji  na uboreshaji  ili huduma hizo ziendane na thamani ya fedha wanazotoa watumiaji.

Mtaka alisema wajumbe wa kamati ya baraza la ushauri la watumia huduma za EWURA, wanao wajibu wa kuelimisha na kusambaza taarifa sahihi kwa watumiaji wa huduma za nishati na maji ili wajue masuala yanayowahusu hususani haki na wajibu wao.
“Mwenyekiti kamati yako itoe taarifa za mara kwa mara kwa watumiaji wa huduma za nishati na maji hasa yanapotokea mabadiliko kama kupanda au kushuka kwa bei ya maji , mafuta na umeme, kukatika kwa maji au umeme na taarifa nyingine muhimu kwa watumiaji wa huduma hizi ili wawe na ufahamu wa kutosha”, alisema Mtaka.

 Aliahidi kuwa Serikali ya Mkoa na vyombo vyake itashirikiana na Kamati ya baraza hili la Mkoa katika kuwajengea mazingira mazuri ya kufanya kazi ikiwa ni pamoja na kutoa ushirikiano na kuhakikisha malengo ya kuanzishwa kwake yanafanikiwa.

Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa aliwataka wafanyabiashara wa mafuta kuwashushia bei wananchi pale inapotokea bei za bidhaa hiyo kupungua katika soko badala ya kuendelea kuwaumiza kwa kisingizio cha kutopunguza bei kwa kuwa walichukua mzigo wakati bei ikiwa juu.


Kamati ya Mkoa ya Baraza la Ushauri la Watumia huduma zinazodhibitiwa na EWURA Mkoa wa Simiyu inaundwa na wajumbe watano: Suzan Sabuni (Mwenyekiti), Kubagwa Madabila(Katibu), Kulwa Mtebe (Mtunza Hazina), Magreth Kayanda (Mjumbe) na Martha Zongo (Mjumbe).
Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!