Wednesday, August 10, 2016

NAIBU WAZIRI AMEMSIMAMISHA KAZI MKUU WA CHUO CHA MAENDELEO YA JAMII MKOANI SIMIYU



Na Stella Kalinga
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi,Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi Mhandisi Stella Manyanya amemsimamisha kazi aliyekuwa Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Bunamhala kilichopo Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu Bw. Ramadhani Said, kutokana na utendaji usioridhisha na kumteua Bi. Levina Mrema kushikilia wadhifa huo kwa muda, wakati taratibu zingine zikiendelea.

Mhandisi Manyanya amechukua uamuzi huo alipopokea taarifa baada ya kutembelea chuo hicho alipokuwa katika ziara yake Mkoani Simiyu, ambapo amesema hajaridhishwa  na utendaji kazi katika chuo hicho kikongwe kilichofunguliwa rasmi mwaka 1978  ambacho kwa sasa kina watumishi 10 wanaolipwa mshahara na Serikali kwa kuwahudumia wanafunzi 8 tu.

 “Nimepata taarifa kuwa kuna wakati chuo hiki hakina wanafunzi kabisa lakini watumishi mpo na mnaendelea kulipwa mshahara na Serikali, kwa nini vyuo vingine vina wanafunzi hiki  cha kwenu hakina wanafunzi?Wewe kama Mkuu wa Chuo umefanya jitihada gani kuhakikisha chuo kinakuwa na wanafunzi wa kutosha? Maana chuo siyo majengo tu”, alisema Manyanya.  

Manyanya amesema amemteua Levina Mrema kuwa Kaimu Mkuu wa Chuo hiki, kwa kipindi cha matazamio kwa miezi sita ili atumie uzoefu wake kuja na mawazo mapya akishirikiana na uongozi wa Mkoa na wilaya kukifanya chuo kinarudi katika hadhi yake.

Akitoa taarifa kwa Naibu Waziri, aliyekuwa Mkuu wa Chuo hicho Ramadhani Said amesema amefanya jitihada za kukitangaza chuo lakini wanafunzi wanapofika chuoni wanaondoka baada ya kukutana na changamoto ya miundombinu chakavu ya majengo,ukosefu wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia na ukosefu wa umeme.

Katika kukabiliana na changamoto ya miundombinu ya chuo, Naibu Waziri amemuagiza Mkurugenzi wa VETA Taifa kutenga fedha kwa ajili ya ukarabati wa bweni , vitanda na kuweka umeme katika chuo hicho, ambapo aliahidi kutoa shilingi milioni tano za kuanzia kufanya ukarabati ili wanafunzi wasome katika mazingira mazuri. 

Mhandisi Manyanya amemtaka Mkuu wa Chuo aliyeteuliwa kuweka mikakati ya kukitangaza chuo ili kitambulike ndani ya Mkoa na nje ya mkoa wa Simiyu ili vijana wapate ujuzi utakaowasaidia kujikwamua kutoka katika umaskini.

Pamoja na jitihada alizozionesha Naibu Waziri, Bi. Mrema ameomba Serikali itenge fedha  za kutosha katika bajeti ya mwaka wa fedha ujao ili kufanya ukarabati wa majengo yote, kununua vifaa vya kujifunzia na kufundishia, kutengeneza barabara ili kuweka mazingira yatakayowashawishi wanafunzi kujiunga katika chuo hicho.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka ameahidi kusimamia na kuhakikisha chuo hicho kinakuwa na manufaa kwa Mkoa wa Simiyu na Taifa kwa ujumla ili kiwasaidie Watanzania hususani vijana kupata elimu na ujuzi wa masuala mbalimbali ukiwemo ujasiriamali, ushonaji, ufundi uashi, ufundi seremara na mafunzo mengine.

Kabla ya kuteuliwa kuwa Kaimu Mkuu wa Chuo, Bi. Levina Mrema alikuwa Mhasibu katika chuo hicho.
 

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Mhandisi Stella Manyanya (kushoto) akitoa maelekezo kwa Kaimu Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Bi. Levina Mrema (kulia) aliyemteua wakati alipokuwa katika ziara yake ya siku moja  Mkoani Simiyu, (katikati) Mkurugenzi wa VETA Kitengo cha Masoko, Ajira  na Mipango Enock Kibendera  (Picha na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu)
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Mhandisi Stella Manyanya (katikati) akizungumza jambo na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka (kushoto) wakati alipokuwa akikagua miundombinu ya Chuo cha Maendeleo ya Jamii Bunamhala Mjini Bariadi, wakati wa ziara yake Mkoani humo, (kulia) ni Mkurugenzi wa VETA Kitengo cha Masoko, Ajira  na Mipango Enock Kibendera. (Picha Na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Mhandisi Stella Manyanya (kushoto) akizungumza na watumishi wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Bunamhala Mjini Bariadi(hawapo pichani) wakati wa ziara yake Mkoani humo. (Picha Na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu.

Watumishi wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Bunamhala Mjini Bariadi wakimsikiliza Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Mhandisi Stella Manyanya (hayupo pichani) wakati wa zira yake ya siku moja mkoani humo. (Picha Na Ofisi ya mkuu wa mkoa wa Simiyu)


Aliyekuwa Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii, Bunamhala Ramadhani Saidi (wa pili kushoto) akitoa maelezo juu ya chuo hicho kwa Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Mhandisi Stella Manyanya (hayupo pichani) wakati wa ziara yake Mkoani Simiyu. (Picha Na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu)







0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!