Saturday, December 17, 2016

WILAYA YA MEATU YAANDAA MPANGO MKAKATI KUBORESHA KILIMO CHA PAMBA , MAHINDI NA MTAMA

Na Stella Kalinga
Halmashauri  wilaya ya Meatu Mkoani Simiyu imeandaa mpango mkakati wa kuboresha kilimo cha pamba , mahindi na mtama kwa lengo la kuwawezesha wakulima kuzalisha mazao mengi na yenye ubora kwa kufuata kanuni za kilimo bora.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Ndg.Fabian Manoza alipozungumza na wananchi wa Kata ya Mwanhuzi kwenye Mkutano wa hadhara uliofanyika jana, katika kituo cha mabasi cha mjini Mwanhuzi,, wakati wa Ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka wilayani humo.

Manoza amesema wakulima wengi wamekuwa wakizalisha pamba kwa kutofauata kanuni za kilimo bora hali inayopelekea kupata mavuno hafifu ya kilo 300 kwa heka moja wakati endapo watalima kitaalam wanaweza kupata kuanzia kilo 1000 kwa heka moja.

“Pamba tunayozalisha sasa hivi, mkulima ukijitahidi unavuna kilo 300 kwa heka moja lakini ikitunzwa vizuri, ukatumia mbegu nzuri  unaweza  kupata kilo 1000. Sisi kama viongozi tuliopewa dhamana Lazima tuwapeleke wakulima wetu huko, sasa tumeanza kwa kuanzisha mafunzo ya kilimo bora cha pamba,kata zote vijiji vyote mafunzo ambayo  yataenda sambamba na matumizi ya mbegu bora ya UKM08, tuachane na matumizi ya mbegu za kienyeji.”, alisema Manoza.

Manoza amesema Halmashauri yake imekusudia kufikia mwaka 2019 wakulima wote wilayani humo watumie mbegu bora za pamba na kutumia mbinu za kisasa za kilimo ili wafikie azma ya kuzalisha kilo 1000 kwa heka.

Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa kuanzia tarehe 19 Disemba,2016 yeye pamoja na wakuu wote wa idara wataenda vijijini kwa ajili ya kufungua mashamba darasa ya pamba, mahindi na mtama, hivyo akaagiza Maafisa Watendaji wa kata zote wafike Ofisini kwake kwa ajili ya kuchukua mbegu za mashamba darasa hayo.

Kwa upande wa kilimo cha mahindi Mkurugenzi huyo amesema kwa kuwa Jimbo la Kisesa limekuwa likipata mvua za kutosha ikilinganishwa na jimbo la Meatu, wamekusudia kuwasaidia wananchi wa Kisesa kulima mahindi kwa kufuata mbinu za kisasa ili wapate chakula cha kutosha na ziada, kwa ajili  ya biashara.

Manoza amesema kwa kuwa Jimbo la Meatu limekuwa likipata mvua kidogo Halmashauri imesaini mkataba na Mwekezaji Saimon Group ambaye atafanya kilimo cha mkataba na wakulima, ambapo atatoa mbegu bora  za mtama na kutoa mikopo kwa wakulima kwa asilimia 100 ili kuwawezesha kutekeleza kilimo cha mtama.

Kufuatia kuwepo kwa mkakati huo ifikapo Disemba 2017 Halmashauri imekusudia kuyaongezea thamani mazao ya mahindi na mtama kwa kujenga kiwanda cha  kuchakata unga wa mahindi katika kata ya Mwandoya (Jimbo la Kisesa) na Kiwanda cha kuchakata unga wa mtama katika kata ya Jija (Jimbo la Kisesa) ambao utauzwa ndani na nje ya Simiyu.

Akiunga mkono mkakati huo wa kilimo Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka amewahimiza wananchi kulima pamba kwa kuwa Serikali mkoani humo kwa kushirikiana na wadau wengine imejipanga kuanza kujenga viwanda vya bidhaa za afya zitokanazo na pamba mwaka 2017, ambazo ni pamba za hospitali, bandeji, pamba za masikio, pampasi za watoto  na pedi za wanawake, hali itakayoliongezea thamani zao la pamba, kwa kuwa litahitajika kwa wingi.

          Aidha, Mtaka amewataka wananchi kutunza akiba ya chakula waliyonayo pamoja na kulima mazao yanayostahimili ukame na yale yanayokomaa kwa muda mfupi kwa kuwa,  kwa mujibu wa Mamlaka ya hali ya hewa nchini  mwaka 2017 hautakuwa na mvua za kutosha na hakutakuwa na chakula cha msaada.

Naye Mkuu wa wilaya ya Meatu, Mhe.Dkt.Joseph Chilongani amesema Serikali wilayani humo kwa kushirikiana na Bodi ya Pamba imeichagua kata ya Mwabusalu kuwa kituo cha kuzalisha mbegu bora, hivyo wananchi wategemee kupata mbegu bora itakayowazesha kupata mavuno bora.  

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, amefanya ziara wilayani Meatu kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu ya elimu hususani ujenzi wa vyumba vya madarasa, ambapo ameunga mkono juhudi za Serikali na wananchi katika ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa kuchangia mifuko 120 ya saruji.


Katika ziara hiyo pia  amezungumza na wananchi wa wilaya hiyo kupitia mkutano wa hadhara ambapo alipata fursa ya kusikiliza kero mbalimbali kutoka kwa wananchi, ambapo kero nyingi ziliigusa Idara ya Ardhi. Baada ya Mkuu wa Mkoa kutoridhishwa na majibu yaliyotolewa na Idara ya Ardhi, alitoa siku 14 kwa wananchi kupeleka kero zao kwa Mkuu wa Wilaya na akaahidi kufanya mkutano wa hadhara tena kwa tarehe itakayopangwa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, akiwa na timu ya wataalam kutoka Ofisi ya Mkoa ili kutatua kero za wananchi hao.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Meatu (hawapo pichani) kwenye Mkutano wa Hadhara uliofanyika  jana katika Kituo cha Mabasi cha mjini Mwanhuzi wakati wa ziara yake wilayani humo.
Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Dkt.Joseph Chilongani akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Meatu (hawapo pichani) kwenye Mkutano wa Hadhara uliofanyika jana katika Kituo cha Mabasicha mjini Mwanhuzi wakati wa ziara ya Mkuu wa mkoa wa Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka wilayani humo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri  ya Wilaya ya Meatu, Ndg.Fabian Manoza akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Meatu (hawapo pichani) kwenye Mkutano wa Hadhara uliofanyika jana, katika Kituo cha Mabasi cha mjini Mwanhuzi wakati wa ziara ya Mkuu wa mkoa wa Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka wilayani humo.
Baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Meatu wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka kwenye Mkutano wa Hadhara uliofanyika jana katika Kituo cha Mabasi cha mjini Mwanhuzi wakati wa ziara ya yake wilayani humo.
Baadhi ya Viongozi wa Wilaya ya Meatu wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka(hayupo pichani) kwenye Mkutano wa Hadhara uliofanyika jana, katika Kituo cha Mabasi cha mjini Mwanhuzi wakati wa ziara ya yake wilayani humo.
Mwenyekiti wa wa Halmashauri  ya Wilaya ya Meatu, Mhe.Pius Machungwa  akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Meatu (hawapo pichani) kwenye Mkutano wa Hadhara uliofanyika jana ,katika Kituo cha Mabasi cha mjini Mwanhuzi wakati wa ziara ya Mkuu wa mkoa wa Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka wilayani humo.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Meatu, Mhe.Juma Mwibule akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Meatu (hawapo pichani) kwenye Mkutano wa Hadhara uliofanyika jana katika Kituo cha Mabasi cha mjini Mwanhuzi wakati wa ziara ya Mkuu wa mkoa wa Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka wilayani humo.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na baadhi ya viongozi  wa Wilaya ya Meatu (hawapo pichani) mara baada ya kukagua ujenzi wa vyumba vya madarasa katika Shule ya msingi Mshikamano wakati wa ziara yake wilayani humo.
Baadhi ya vyumba vya madarasa vilivyojengwa kwa ushirikiano wa Serikali na Wananchi katika Shule ya Msingi Mshikamano wilayani Meatu.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka  akiwa na baadhi ya viongozi wa Wilaya ya Meatu alipotembelea eneo linapojengwa banda la ng’ombe bora wa kisasa wa maziwa watakaofungwa kwa ajili ya kusaidia Mradi wa kiwanda cha kusindika maziwa ya “ MEATU MILK”    

0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!