Saturday, April 20, 2019

NAIBU WAZIRI MAVUNDE AWATAKA KIDATO CHA SITA SIMIYU WASIKUBALI NDOTO ZAO KUKATISHWA


Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Ajira, Mhe.Anthony Mavunde ametoa wito kwa wanafunzi wa kidato cha sita Mkoani Simiyu kutokubali mtu yeyote kufifisha wala kukatisha ndoto zao badala yake wasome kwa bidii.

Mavunde ametoa wito huo wakati akizungumza na wanafunzi zaidi ya 1000 kutoka  shule kumi na mbili za sekondari za  kidato cha sita walioko katika kambi ya kitaaluma, shule ya sekondari ya wasichana Maswa.

Mavunde amesema Taifa lolote duniani linajengwa na vijana na hasa vijana wasomi hivyo wanapaswa kusoma kwa bidii, ili wasiwaangushe, wazazi na jamii inayowazunguka  ambayo inawategemea, huku akipongeza uongozi wa mkoa kuanzisha kambi za kitaaluma ambazo zimeoneka kuusaidia mkoa kupanda katika ufaulu.

“wanafunzi msikubali ndoto zenu zikatishwe, someni kwa bidii mfikie ndoto zenu, Taifa wazazi na jamii inayowazunguka inawategemea, msiwaangushe viongozi wenu waliofanya mkawa hapa, Mkoa wa Simiyu ndio umetuonesha kuwa kumbe kambi za kitaaluma zinawezekana” alisema Mhe. Mavunde.

Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony  Mtaka amewapongeza walimu wote kwa kazi nzuri wanayoifanya  na kueleza  lengo la kuanzishwa kambi za kitaaluma ambazo amesema zimeonekana kuwa na mwamko mkubwa kwa wanafunzi.

“Sisi tulitafakari watoto wetu wanatoka kwenye mazingira ya kawaida tukajiuliza kwa nini wasikae kwenye madarasa yaliyo na sakafu na dari safi wakasoma, tumejaribu kwenye shule za O’level (kidato cha nne) tumeona mwamko wa watoto kusoma” alisema Mhe. Mtaka.

Kwa upande wao viongozi na wadau mbalimbali wa elimu waliowatembelea wanafunzi hao pia walipata nafasi ya kuwausia wanafunzi hao wa kidato cha sita na kuwasisitiza juu ya umuhimu wa kufanya bidii ili kufikia malengo  yao.

“ Tunajadiliana hapa ili kuwa na uelewa wa pamoja, ninataka kuwaambia kuwa hakuna mafanikio yanayokuja kwa bahati mbaya iwe  katika masomo hata katika maisha,” alisema Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisha.

“Mnaweza kutimiza ndoto zenu bila kujali mahali mtu anapotoka, najua wengi wetu hapa tumetoka katika familia za kawaida, tumesoma shule za kawaida kabisa lakini tulifanikiwa, hata ninyi mnaweza ni suala la kuamua tu” alisema Happiness Lugiko Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki.

Naye Askofu wa Kanisa la Waadventista Wasabato Jimbo Kuu la kusini, Mch. Mark Malekana amesema ili wanafuzi hao waweze kufikia ndoto zao wanapaswa kuwa na dhamira ya kushinda, wasome kwa bidii, wawe na nidhamu, washinde hofu wanapokuwa kwenye mitihani na wamwamini Mungu.

Mwanafunzi Kelista Joseph kutoka shule ya sekondari Itilima amesema maswali mbalimbali ambayo wamekuwa wakiyafanyia kazi yatawasaidiana mwishowe watafanya vizuri  na wanaamini kama walivyoahidi toka siku ya kwanza ya kambi kwamba watapata ‘Division One’ wote.

Kambi ya Kitaaluma kwa wanafunzi wa Kidato cha Sita mwaka 2019 Mkoani Simiyu inatarajiwa kufungwa rasmi Aprili 28, 2019 na baadaye wanafunzi watarejea katika shule zao kwa ajili ya maandalizi ya Mtihani wa Taifa unaotarajia kuanza Mei 06, 2019.

MWISHO

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Ajira, Mhe.Anthony Mavunde  akizungumza na wanafunzi wa Kidato cha Sita walio katika kambi ya Kitaaluma Mkoani Simiyu wakati aliwapowatembelea wanafunzi hao wilayani Maswa, Aprili 19, 2019.


Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka(kushoto) akipokea mchango wa shilingi milioni moja kutoka kwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Ajira, Mhe.Anthony Mavunde aliochangia kwa ajili ya kambi ya kitaaluma ya wanafunzi wa kidato cha sita inayoendelea katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Maswa.
Baadhi ya wanafunzi wa Kidato cha Sita mkoani Simiyu wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Ajira, Mhe.Anthony Mavunde wakati alipowatembelea wanafunzi hao Aprili 19, 2019. katika kambi ya Kitaaluma inayoendelea katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Maswa.
Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya akizungumza na baadhi ya wanafunzi  wa Kidato cha Sita shule ya Sekondari ya Wasichana Maswa wakati viongozi mbalimbali wa Serikali walipowatembelea wanafunzi  walio katika kambi ya kitaaluma kwa wanafunzi wote wa kidato cha sita Mkoani Simiyu inayoendelea katika shule hiyo.
Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya akizungumza na wanafunzi wa Kidato cha Sita Mkoani Simiyu walio katika kambi ya kitaaluma inayoendelea katika shule ya sekondari ya wasichana Maswa (hawapo pichani) wakati viongozi mbalimbali wa Serikali walipowatembelea shuleni hapo.
Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki Mhe. Happiness Lugiko  akizungumza na wanafunzi wa Kidato cha Sita Mkoani Simiyu walio katika kambi ya kitaaluma inayoendelea katika shule ya sekondari ya wasichana Maswa (hawapo pichani)wakati viongozi mbalimbali wa Serikali walipowatembelea shuleni hapo.
Baadhi ya viongozi wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya waanfunzi wa kidato cha sita mwaka 2019 mkoani Simiyu, walio katika kambi ya kitaaluma inayoendelea katika shule ya sekondari ya wasichana Maswa wakati viongozi hao walipowatembelea shuleni hapo Aprili 19, 2019.
 Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akimshika ng’ombe aliyetolewa na Mhe. Pili Ndimila Diwani wa Viti maaluma Wilayani Maswa, kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha sita mkoani Simiyu walio katika kambi ya kitaaluma inayoendelea katika shule ya sekondari ya wasichana Maswa.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu. Mhe. Anthony Mtaka(wa tatu kushoto) akimtambulisha Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Ajira, Mhe.Anthony Mavunde kwa wanafunzi wa Kidato cha Sita Mkoani Simiyu walio katika kambi ya kitaaluma inayoendelea katika shule ya sekondari ya wasichana Maswa (hawapo pichani) wakati viongozi mbalimbali wa Serikali na wa dini walipowatembelea shuleni hapo.
Askofu wa Kanisa la Waadventista Wasabato Jimbo Kuu la kusini, Mch. Mark Malekana akiwaombea wanafunzi wa Kidato cha Sita Mkoani Simiyu walio katika kambi ya kitaaluma inayoendelea katika shule ya sekondari ya wasichana Maswa wakati viongozi mbalimbali wa Serikali na wa dini walipowatembelea shuleni hapo.
Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akizungumza na baadhi ya wanafunzi wa kidato cha sita waliokatika kambi ya kitaaluma inayoendelea katika shule ya sekondari ya wasichana Maswa wakati viongozi mbalimbali wa Serikali na wa dini walipowatembelea shuleni hapo Aprili 19, 2019.
Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akizungumza na baadhi ya wanafunzi wa kidato cha sita waliokatika kambi ya kitaaluma inayoendelea katika shule ya sekondari ya wasichana Maswa wakati viongozi mbalimbali wa Serikali na wa dini walipowatembelea shuleni hapo Aprili 19, 2019.
Kalista Joseph Mwanafunzi  wa Kidato cha Sita kutoka Shule ya Sekondari Itilima akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake wa mkoa wa Simiyu waliopo katika kambi ya kitaaluma inayoendelea katika shule ya sekondari ya wasichana Maswa wakati viongozi mbalimbali wa Serikali na wa dini walipowatembelea shuleni hapo Aprili 19, 2019.
Mmoja wa wanafunzi wa Kidato cha Sita kutoka Shule ya Sekondari Simba wa Yuda akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake wa mkoa wa Simiyu waliopo katika kambi ya kitaaluma inayoendelea katika shule ya sekondari ya wasichana Maswa wakati viongozi mbalimbali wa Serikali na wa dini walipowatembelea shuleni hapo Aprili 19, 2019.
Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka(wa nne kushoto) na vingozi wengine wa dini na wa serikali wakizungumza na baadhi ya wanafunzi wa Kidato cha Sita mkoa wa Simiyu waliopo katika kambi ya kitaaluma inayoendelea katika shule ya sekondari ya wasichana Maswa, wakati viongozi hao walipowatembelea shuleni hapo Aprili 19, 2019.
Baadhi ya viongozi na wanafunzi wakishuhudia ng’ombe wawili waliotolewa na wadau wa elimu kwa ajili ya kuchangia kambi ya kitaaluma ya wanafunzi wa kidato cha sita inayoendelea katika shule y sekondari Maswa.
Baadhi ya viongozi wa dini na Serikali wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wanafunzi wa Kidato cha Sita mkoa wa Simiyu waliopo katika kambi ya kitaaluma inayoendelea katika shule ya sekondari ya wasichana Maswa, wakati viongozi hao walipowatembelea shuleni hapo Aprili 19, 2019.


Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya(mwenye miwani) na  Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka wakiwa na baadhi ya wanafunzi wa Kidato cha Sita mkoa wa Simiyu waliopo katika kambi ya kitaaluma inayoendelea katika shule ya sekondari ya wasichana Maswa, wakati viongozi wa Serikali na wa dini walipowatembelea shuleni hapo Aprili 19, 2019.

Mkurugenzi wa Utawala na Fedha wa BRELA, Bw. Bakari Mketu akizungumza na wanafunzi wa Kidato cha Sita Mkoani Simiyu walio katika kambi ya kitaaluma inayoendelea katika shule ya sekondari ya wasichana Maswa (hawapo pichani)wakati viongozi mbalimbali wa Serikali na viongozi wa  dini walipowatembelea shuleni hapo Aprili 19, 2019.
Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya akisalimiana na Silya Jasamila(19)binti aliyenusurika kuozeshwa na baba yake mzazi mara baada ya kuhitimu kidato cha nne , ambaye kwa sasa anatunzwa na kulelewa na viongozi wa Serikali katika Shule ya sekondari Maswawakati akisubiri kuchaguliwa kujiunga na kidato cha tano, wakati balozi huyo alipowatembelea wanafunzi wa kidato cha sita walio katika kambi ya kitaaluma shuleni hapo Aprili 19, 2019

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Ajira, Mhe.Anthony Mavunde(wa pili kushoto) akiteta jambo na   Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya wakati viongozi mbalimbali wa serikali na dini walipowatembelea wanafunzi wa Kidato cha sita mkoani Simiyu(hawapo pichani) Aprili 19, 2019 katika kambi ya Kitaaluma inayoendelea katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Maswa. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, mhe. Anthony Mtaka na kulia ni Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Mhe. Happiness Lugiko.
Kutoka kulia Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, mhe. Anthony Mtaka, Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dkt. Seif Shekalaghe na Afisa Elimu Mkoa, Mwl. Ernest Hinju wakifurahia jambo wakati wa ziara ya viongozi mbalimbali katika kambi ya kitaaluma kwa wanafunzi wa kidato cha sita inayoendelea katika shule ya sekondari ya wasichanaMaswa.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, mhe. Anthony Mtaka(mwenye kipaza sauti) akimtambulisha Askofu wa Kanisa la Waadventista Wasabato Jimbo Kuu la kusini, Mch. Mark Malekana kwa wanafunzi wa Kidato cha Sita mkoa wa Simiyu waliopo katika kambi ya kitaaluma inayoendelea katika shule ya sekondari ya wasichana Maswa, wakati viongozi wa Serikali na wa dini walipowatembelea shuleni hapo Aprili 19, 2019.
Baadhi ya wanafunzi wa kidato cha sita walio katika kambi ya kitaaluma inayoendelea katika shule ya sekondari ya wasichana Maswa wakiimba wimbo wa Tanzania Tanzania, wakati viongozi wa Serikali na wa dini walipowatembelea shuleni hapo Aprili 19, 2019.

Friday, April 19, 2019

NAIBU WAZIRI MAVUNDE ATOA WITO KWA ATAPE KUSHIRIKI UJENZI WA UCHUMI WA VIWANDA


Naibu waziri ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Ajira, Mhe. Anthony Mavunde ametoa wito kwa kwa Chama  cha  wanataaluma na wajasiliamali wa Kanisa la Wadventista Tanzania (ATAPE) kushiriki katika uchumi wa viwanda ili kuongeza nafasi za ajira kwa vijana na kupunguza umaskini.

Mavunde ameyasema hayo wakati akifungua mkutano wa 20 wa chama  hicho ambao Kitaifa unafanyika mkoani Simiyu na kuhudhuriwa na zaidi ya wanachama 1500 kutoka maeneo yote nchini.

“ATAPE kupitia wataaluma na wajasiriamali mnayo nafasi kubwa ya kukusanya rasilimali na kuhakikisha mnafanya vitu vyenye mchango chanya kwa Taifa hususani katika kutengeneza ajira kwa vija na kupunguza umaskini”

“Angalieni fursa zinazowazunguka  ili miaka 20 ya uwepo wa ATAPE iende sambamba na uwekezaji na mafanikio mtakayoyapata, nitoe wito msiwe nyuma kushiriki katika ujenzi wa uchumi wa viwanda, Simiyu wanajenga viwanda vikubwa Maswa cha chaki na vifungashio, wtajenga kiwanda cha vifaa tiba amkeni changamkieni” alisema Mhe. Mavunde.

Hata hivyo ameongeza kuwa kama serikali inatambua mchango mkubwa walioutoa ATAPE  kwa kuendelea kuisaidia serikali kutengeneza nafasi za ajira  kupitia uwekezaji walioufanya kwenye meaneo mbalimbali ikiwemo kilimo, misitu na utoaji wa elimu ya ujasiliamali bure hatua iliyopelekea idadi kubwa ya watanzania kujiajiri pasipo kusubiri kuajiriwa.

“ATAPE imethubutu nitoe wito kwa madhehebu mengine kuiga mfumo huu wa kuwaleta pamoja wanataaluma na wajasiriamali ili wawe chachu ya mabadiliko kiuchumi waweze kufanya vitu vyenye manufaa kwa waumini na jamii kwa ujumla, epukeni dhana potofu ya kusema hatutoweza mjiamini mtaweza tu”

Awali akimkaribisha Naibu waziri,  Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony  Mtaka amesema kuwa kama mkoa uliona kila sababu ya kuzialika taasisi mbalimbali ikiwemo BRELLA , Shirika la bima la Taifa , EFTA lengo likiwa kuwafikia wajasiliamali na kuongeza kuwa ni vema wana ATAPE  wakajifunza kutenda badala ya kuzungumza

“Ifike mahali mtofautishe mahubiri na ujasiliamali ni lazima mkizungumza mjifunze kutenda ….hivi karibuni ujenzi wa chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) kinaanza kujengwa wanachuo 1000 wanatarajiwa kusoma hapo, nendeni pale mkajenge  hosteli punguzeni porojo” alisema Mtaka.

Aidha, Mtaka ametoa wito kwa Wajasiriamali kusajili biashara zao ili ziweze kutambuliwa na wazikatie bima kwa ajili ya kuepuka hasara pindi biashara zao zinapokumbwa na majanga hususani majanga ya moto.

Mwenyekiti wa ATAPE Taifa, Bw. Freddie Manento amesema kuwa chama hicho kimefanikiwa kuwekeza zaidi ya shilingi bilioni moja kupitia miradi ya maendeleo waliyiwekeza katika maeneo mbalimbali hapa nchini na kuongeza kuwa wamewekeza kwenye miradi ya kilimo afya, maji, ujasiliamali na elimu.

“Tuna mashamba zaidi ya ekari 10,000 ambayo tumelima korosho ,miti na mihogo ,tumewekeza mradi wa maji kigamboni jijini Dar es salaam hivyo tunavyoadhimisha miaka hii 20 ya ATAPE tuna kila sababu ya kujivunia maana miradi hii yote imetoa ajira nyingi kwa watanzania wenzetu zikiwemo za kudumu na za mkataba” alisema Maneto.

Kwa upande wake Askofu wa Kanisa la Waadventista Wasabato, Mark Malekana amewataka waumini wa kanisa hilo kufanya kazi kwa bidii ili kukwepa dhambi ya umaskini na kuwataka kuunga mkono juhudi za Serikali iliyopo madarakani katika kujiletea maendeleo.

Naye Irene Kweka ni miongoni mwa wajasiliamali walioshiriki mkutano huo amesema kuwa mkutano huo umemsaidia kuongeza wateja wapya kujifunza kupitia kubadilishana uzoefu  sambamba na kuongeza kipato.

MWISHO
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Ajira, Mhe. Anthony Mavunde akizungumza na Wanachama wa Chama cha Wanataaluma na Wajasiriamali wa Kanisa la Waadventista Wasabato Tanzania(ATAPE), wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 20 wa Chama hicho unaofanyika Mjini Bariadi Mkoani Simiyu.
Baadhi ya Wanachama wa Chama cha Wanataaluma na Wajasiriamali wa Kanisa la Waadventista Wasabato Tanzania(ATAPE), wakiimba wimbo wa pamoja wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 20 wa Chama hicho unaofanyika Mjini Bariadi Mkoani Simiyu.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Ajira, Mhe. Anthony Mavunde (wa pili kulia) akifurahia jambo na viongozi wa Serikali na Kanisa la Waadventista Wasabato baada ya kufungua Mkutano Mkuu wa 20 wa Chama Wanataaluma na Wajasiriamali wa Kanisa la Waadventista Wasabato Tanzania(ATAPE) unaoendelea Mjini Bariadi, (wa pili kulia) Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Ajira, Mhe. Anthony Mavunde(wa nne kushoto) akiwa na baadhi ya Kanisa la Waadventista Wasabato na viongozi wa Chama cha Wanataaluma na Wajasiriamali wa Kanisa hilo wakishuhudia onesho la Vijana watengeneza njia(Pathfinders) kabla ya kufungua Mkutano wa Chama cha Wanataaluma na Wajasiriamali wa Kanisa la Waadventista Wasabato Tanzania(ATAPE)Mjini Bariadi(wa tatu kushoto) Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka.
Vijana watengeneza njia(Pathfinders) wakitoa heshima kwa Mgeni Rasmi Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Ajira, Mhe. Anthony Mavunde(hayupo pichani)  muda mfupi kabla ya kufungua Mkutano wa Chama cha Wanataaluma na Wajasiriamali wa Kanisa la Waadventista Wasabato Tanzania(ATAPE)Mjini Bariadi.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Ajira, Mhe. Anthony Mavunde akiangalia baadhi ya bidhaa za wajasiriamali katika Viwanja vya Shule ya Sekondari ya Kusekwa Memorial, muda mfupi kabla ya kufungua Mkutano wa Chama cha Wanataaluma na Wajasiriamali wa Kanisa la Waadventista Wasabato Tanzania(ATAPE)Mjini Bariadi.
Mwenyekiti wa Chama cha Wanataaluma na Wajasiriamali wa Kanisa la Waadventista Wasabato Tanzania(ATAPE) Bw. Freddie Manento akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Ajira, Mhe. Anthony Mavunde(mwenye skafu) juu ya masuala mbalimbali yanayofanywa na chama hicho mara baada ya kutembelea banda lao,  muda mfupi kabla ya kufungua Mkutano mkuu wa chama hicho unaoendelea mjini Bariadi.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Ajira, Mhe. Anthony Mavunde akiangalia mikanda ya ngozi inayotengenezwa na kikundi cha vijana kutoka Mkula wilayani Busega, muda mfupi kabla ya kufungua Mkutano Mkuu wa 20 wa Chama cha Wanataaluma na Wajasiriamali wa Kanisa la Waadventista Wasabato Tanzania(ATAPE) Mjini Bariadi.
Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Mhe. Happiness Lugiko akizungumza na Wanachama wa Chama cha Wanataaluma na Wajasiriamali wa Kanisa la Waadventista Wasabato Tanzania(ATAPE), wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 20 wa Chama hicho unaofanyika Mjini Bariadi Mkoani Simiyu.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akizungumza na Wanachama wa Chama cha Wanataaluma na Wajasiriamali wa Kanisa la Waadventista Wasabato Tanzania(ATAPE), wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 20 wa Chama hicho unaofanyika Mjini Bariadi Mkoani Simiyu.
Kwaya ya Ushuhuda kutoka Kakola Mkoani Geita ikiimba wimbo maalum wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 20 wa Chama cha Wanataaluma na Wajasiriamali wa Kanisa la Waadventista Wasabato Tanzania(ATAPE), unaofanyika Mjini Bariadi Mkoani Simiyu.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Ajira, Mhe. Anthony Mavunde akisalimiana na Askofu wa Kanisa la Waadventista Wasabato Mark Malekana mara baada ya kuwasili Mjini Bariadi kwa ajili ya kufungua Mkutano Mkuu wa 20 wa Chama cha Wanataaluma na Wajasiriamali wa Kanisa la Waadventista Wasabato Tanzania(ATAPE).
Askofu wa Kanisa la Waadventista Wasabato Mark Malekana(katikati) akionesha zawadi iliyotolewa na Chama cha Wanataaluma na Wajasiriamali wa Kanisa la Waadventista Wasabato Tanzania(ATAPE) kwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka, mara baada ya ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 20 wa Chama hicho unaofanyika Mjini Bariadi.
Baadhi ya Wanachama wa Chama cha Wanataaluma na Wajasiriamali wa Kanisa la Waadventista Wasabato Tanzania(ATAPE), wakiimba wimbo wa pamoja wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 20 wa Chama hicho unaofanyika Mjini Bariadi Mkoani Simiyu.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Ajira, Mhe. Anthony Mavunde akiangalia baadhi ya bidhaa za wajasiriamali katika Viwanja vya Shule ya Sekondari ya Kusekwa Memorial, muda mfupi kabla ya kufungua Mkutano wa Chama cha Wanataaluma na Wajasiriamali wa Kanisa la Waadventista Wasabato Tanzania(ATAPE)Mjini Bariadi.
Vijana watengeneza njia(Pathfinders) wa Kanisa la Waadventista Wasabato wakimvisha skafu Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Ajira, Mhe. Anthony Mavunde mra baada ya kuwasili Mjini Bariadi, kwa ajili ya kufungua Mkutano Mkuu wa 20 wa Chama cha Wanataaluma na Wajasiriamali wa Kanisa la Waadventista Wasabato Tanzania(ATAPE).




WAFANYABIASHARA WAHIMIZWA KUSAJILI BIASHARA BRELA ZITAMBULIWE, ZIFANYWE KWA USHINDANI


Wafanyabiashara hapa nchini wametakiwa kusajili biashara zao kwa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) ili ziweze kutambuliwa kirahisi na  waweze kufanya biashara kwa ushindani wa Kitaifa na Kimataifa.

Hayo yamebainishwa na baadhi ya wafanyabiashara Mjini Bariadi Mkoani Simiyu mara baada ya kutembelewa na Maafisa kutoka BRELA katika maeneo yao ya biashara kwa lengo la kufuatilia masuala mbalimbali ya Wakala huo ikiwa ni pamoja kutoa elimu na kuangalia mwitikio wa mfumo wa usajili wa biashara kupitia mtandao (Online Registration System-ORS).

“ Kuna faida sana kwa mfanyabiashara kusajili biashara yake BRELA kwanza inatambulika, usajili pia utamsaidia kupata urahisi hasa kwa makampuni yanayotaka kuingia mkataba na yeye, akihitaji huduma za kifedha katika benki na utamsaidia kutangaza biashara yake popote”

“Kampuni yoyote inayotaka kuingia mkataba na sisi ni lazima inaomba nyaraka za usajili wa BRELA, tukitaka huduma za kifedha kwenye benki nao wanahitaji nyaraka za BRELA, yapo manufaa makubwa kusajili BRELA” Lucy Sabu Mkurugenzi Msaidizi, Hoteli ya Sweet Dream Bariadi.

Naye Bi Neema Joseph Meneja wa Kituo cha mafuta JBS Bariadi ameshukuru BRELA kwa kuanzisha usajili wa biashara kupitia mtandao(Online Registration System-ORS) jambo ambalo amesema litawawasaidia wafanyabiasha kufanya usajili mahali walipo badala ya kusafiri kufuata huduma hiyo Dar es salaam kama ilivyokuwa awali.

Aidha, Bi. Neema ameomba BRELA iendelee kutoa elimu kuhusu umuhimu wa usajili wa biashara kwa wafanyabiashara na matumizi ya mfumo mpya wa usajili kupitia mtandao ili uweze kufahamika vizuri zaidi kwa wafanyabiashara.

Mkurugenzi wa Utawala na Fedha kutoka BRELA, Bw. Bakari Mketu amesema mara baada ya kutoa elimu ya usajili miezi miwili iliyopita kiwango cha usajili kimeongezeka na kufikia asilimia 80 ya lengo walilojiwekea kwa robo zote tatu ndani ya mwaka .

“Tumesajili kampuni 4678  zaidi ya  66% huku malengo yakiwa kusajili 7110 na kusajili majina ya biashara 8022 zaidi ya  49%  huku malengo yakiwa kusajili majina 1640 kwa robo zote tatu  .... kwanza tulikuwa tunapanda taratibu ...tutaendelea kuwaelimisha wateja wetu ili kuhakikisha wateja wote wanakuwa uelewa wa kutosha.

Katika hatua nyingine Mketu ametoa rai kwa wanasheria kuzingatia sheria katika utekelezaji wa majukumu yao ikiwa ni pamoja na masuala yanayohusiana na Usajili, ili kuepuka usumbufu kwa wafanyabiashara.

‘’Sheria ni taaluma ambayo bado inaheshimika sana, kujifunza kila siku ndio taaluma inavyotaka sisi hatuwezi kuwafundisha kazi…lakini tunaomba wazingatie sheria wakati wakifanya majukumu yao, mathalani kuna mwanasheria alifanya zoezi la kubadili hisa za mteja (share transfer) pasipo kufuata utaratibu ambao umeainishwa kisheria na TRA”  alisema Mketu.

Naye Suzana Senso kutoka BRELA amesema ni vema Wanasheria wanapofanya kazi kujiridhisha kwanza juu ya taratibu na sheria zinazotakiwa kufuatwa katika kazi husika ili waweze kuwasadia wateja wao kwa kuzingatia sheria na taratibu.

“Naomba nitoe rai kwa wanasheria, ukipata kazi uliza  wengine taratibu zilivyo  ili uweze kumsaidia mteja, huyu mama alitaka kuhamisha hisa (share transfer) mwanasheria akaja akachomoa nyaraka na kuweka nyingine akamweleza kuwa utaratibu umekamilika wakati utaratibu ulipaswa ufanyike TRA; kutokana na uelewa  wa mama na afisa biashara mkoa wao walitutafuta, najiuliza ni wangapi wanakutana na changamoto hizi” alihoji Bi. Suzan Senso. 

Aidha, Bi. Elizabeth Samweli kutoka Kampuni ya Mlashi General Supplies alikiri kukumbwa na changamoto hiyo ya  mwanasheria  kufanya zoezi la kuhamisha hisa pasipo kufuata utaratibu uliowekwa kisheria na kushukuru BRELA kwa namna walivyomsaidia mara baada ya kuwaeleza changamoto hiyo; huku akisisitiza BRELA kuendelea kutoa elimu.

Maafisa kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) wako Mjini Bariadi Simiyu kwa ajili ya kuendelea kutoa elimu juu ya usajili wa biashara kwa wafanyabiashara mkoani hapa pamoja na wajasiriamali walio katika Mkutano Mkuu wa 20 wa Chama cha Waadventista Wasabato(ATAPE) ambao unafanyika Mkoani Simiyu.

MWISHO

Mkurugenzi wa Utawala na Fedha kutoka BRELA, Bw. Bakari Mketu na Bi. Suzan Senso wakifuahia jambo na Bi. Elizabeth Samweli kutoka Kampuni ya Mlashi General Supplies mfanyabiashara wa Mjini Bariadi walipomtembelea dukani kwake, wakati wakiwa katika ziara kutembelea wafanyabiasara na kutoa elimu juu ya masuala ya usajili, ikiwemo matumizi ya mfumo mpya wa usaji kwa njia ya mtandao(Online Registration System-ORS).

Mkurugenzi wa Utawala na Fedha kutoka BRELA, Bw. Bakari Mketu akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya ziara yake kutembelea wafanyabiasara na kutoa elimu juu ya masuala ya usajili, ikiwemo matumizi ya mfumo mpya wa usaji kwa njia ya mtandao(Online Registration System-ORS)..Mjini Bariadi Simiyu.
Bi. Suzan Senso kutoka BRELA(kulia) akimsikiliza Bi .Neema Joseph Meneja wa Kituo cha Mafuta cha JBS Mjini Bariadi wakati wa ziara yake na Mkurugenzi wa Utawala na Fedha kutoka BRELA, Bw. Bakari Mketu kwa wafanyabishara iliyolenga kutoa elimu juu ya masuaa ya usajili ikiwemo matumizi ya mfumo mpya wa usaji kwa njia ya mtandao(Online Registration System-ORS)..
Bi. Suzan Senso kutoka BRELA(kulia) akiangali nyaraka za Usajili wa Hoteli ya Sweet Dream wakati wa ziara yake na Mkurugenzi wa Utawala na Fedha kutoka BRELA, Bw. Bakari Mketu kwa wafanyabishara iliyolenga kutoa elimu juu ya masuala ya usajili ikiwemo matumizi ya mfumo mpya wa usaji kwa njia ya mtandao (Online Registration System-ORS) (kushoto) ni Mkurugenzi Msaidizi wa Sweet Dream Hotel  Bi.Lucy Sabu.

DAKTARI BINGWA AWATAHADHARISHA WANANCHI KUTOCHANGANYA DAWA ZA HOSPITALI NA KIENYEJI


Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani na maradhi ya moyo  kutoka Wizara ya afya Prof. Harun Nyagori ametoa wito kwa Watanzania kutochanganya dawa za hospitali na kienyeji wakati wa matibabu yao ili kuepuka athari kubwa za kiafya zinazoweza kujitokeza.

Prof Nyagori ameyasema hayo Aprili 18, 2019  wakati akizungumza na  waandishi wa habari  katika Mkutano Mkuu wa chama cha wanataaluma na wajasiriamali wa Kanisa la Waadventista Wasabato(ATAPE),unaofanyika mjini Bariadi.

Amesema kuwa uchanganyaji wa dawa za hospitali na za kienyeji ni hatari kwa afya ya binadamu, hivyo ni vema wagonjwa mbalimbali wa magonjwa ya ndani na maradhi ya moyo kuamua kufanya maamuzi ya matumizi ya dawa upande mmoja ili wasije kujisababishia madhara makubwa zaidi.

“Ni vema wagonjwa wasichanganye dawa za hospitali na za kienyeji, japo dawa nyingi za hospitali zinatengenezwa na Mitishamba lakini utofauti wa dawa za hospitali na dawa za kienyeji ni kwamba wanapotumia dawa za kienyeji wanatumia pasipokujua kiwango cha kemikali zilizopo na aina ya sumu iliyopo kwenye dawa hizo”

“Nimeona wagonjwa wengi wanaochanganya dawa za hospitali na za kienyeji wanapata madhara mbalimbali mwilini, wengine figo zao zimeshindwa kufanya kazi vizuri, wengine maini yameharibika, sukari imezidi kupanda; kwa hiyo nawashauri kama wakiamua kutumia dawa za hospitali watumie hizo na kama wameamua kutumia mitishamba wazitumie hizo tu wasichanganye” alisema Dkt. Nyagori.

Sambamba na hilo Prof Nyagori, pia amesema kuwa katika siku sita za mkutano mkuu wa ATAPE unaoendelea Mkoani Simiyu, ametoa wito kwa wananchi na wakazi wa Simiyu kujitokeza kwa wingi kupima afya zao.

Ameongeza kuwa ndani ya siku mbili ambazo wamekuwa wakitoa huduma hizo za magonjwa ya ndani na maradhi ya moyo, jumla ya wagonjwa 269 walijitokeza kupima afya zao na kati ya hao 103 waligundulika kuwa shinikizo la damu,62 walikuwa na sukari na 140 wenye uzito uliopindukia.

Nao baadhi ya wananchi waliojitokeza kupima afya zao wameshukuru huduma hizo kutoka kwa madaktari bingwa kusogezwa karibu yao kupitia mkutano wa ATAPE huku wakieleza kufurahishwa na huduma hizo kutolewa kwa gharama nafuu.

“Binafsi nimefurahishwa na huduma za madaktari bingwa ambazo nimezipata kupitia mkutano huu wa ATAPE, nimepima na nimeweza kujua afya yangu, kilichonifurahisha zaidi ni kwamba nimetumia shilingi elfu kumi tu kupima shinikizo la damu, sukari na vipimo vingine”alisema Mchungaji Marco Barnabas.

“Huduma zinazotolewa hapa ni nzuri na zinatolewa kwa gharama nafuu kabisa nitoe wito kwa Wanasimiyu kujitokeza kwa wingi kuja kupima afya zao, ili waweze kutambua hali za afya zao na kupata ushauri wa wataalam bingwa” alisema Namkunda Mburuja.

Mkutano Mkuu wa Mkuu wa chama cha wanataaluma na wajasiriamali wa Kanisa la Waadventista Wasabato(ATAPE),unaendelea  mjini Bariadi na unatarajiwa kuhitimishwa Jumapili ya tarehe 21/04/2019; wanataaluma mbalimbali wanaendelea kutoa huduma, huku wajasirimali wakiendelea kuuza bidhaa mbalimbali katika viwanja vya shule ya Sekondari Kusekwa memorial
MWISHO
Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani na maradhi ya moyo  kutoka Wizara ya afya, Prof. Harun Nyagori akimhudumia Bi. Eveline Mshanga wakati alipokuwa akitoa huduma za magonjwa ya moyo katika Mkutano wa ATAPE mjini Bariadi.
Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani na maradhi ya moyo  kutoka Wizara ya afya, Prof. Harun Nyagori akiwaelezea jambo waandishi wa habari alipozungumza nao wakati akitoa huduma za magonjwa ya moyo katika Mkutano wa ATAPE mjini Bariadi.



Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!