Friday, April 19, 2019

WAFANYABIASHARA WAHIMIZWA KUSAJILI BIASHARA BRELA ZITAMBULIWE, ZIFANYWE KWA USHINDANI


Wafanyabiashara hapa nchini wametakiwa kusajili biashara zao kwa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) ili ziweze kutambuliwa kirahisi na  waweze kufanya biashara kwa ushindani wa Kitaifa na Kimataifa.

Hayo yamebainishwa na baadhi ya wafanyabiashara Mjini Bariadi Mkoani Simiyu mara baada ya kutembelewa na Maafisa kutoka BRELA katika maeneo yao ya biashara kwa lengo la kufuatilia masuala mbalimbali ya Wakala huo ikiwa ni pamoja kutoa elimu na kuangalia mwitikio wa mfumo wa usajili wa biashara kupitia mtandao (Online Registration System-ORS).

“ Kuna faida sana kwa mfanyabiashara kusajili biashara yake BRELA kwanza inatambulika, usajili pia utamsaidia kupata urahisi hasa kwa makampuni yanayotaka kuingia mkataba na yeye, akihitaji huduma za kifedha katika benki na utamsaidia kutangaza biashara yake popote”

“Kampuni yoyote inayotaka kuingia mkataba na sisi ni lazima inaomba nyaraka za usajili wa BRELA, tukitaka huduma za kifedha kwenye benki nao wanahitaji nyaraka za BRELA, yapo manufaa makubwa kusajili BRELA” Lucy Sabu Mkurugenzi Msaidizi, Hoteli ya Sweet Dream Bariadi.

Naye Bi Neema Joseph Meneja wa Kituo cha mafuta JBS Bariadi ameshukuru BRELA kwa kuanzisha usajili wa biashara kupitia mtandao(Online Registration System-ORS) jambo ambalo amesema litawawasaidia wafanyabiasha kufanya usajili mahali walipo badala ya kusafiri kufuata huduma hiyo Dar es salaam kama ilivyokuwa awali.

Aidha, Bi. Neema ameomba BRELA iendelee kutoa elimu kuhusu umuhimu wa usajili wa biashara kwa wafanyabiashara na matumizi ya mfumo mpya wa usajili kupitia mtandao ili uweze kufahamika vizuri zaidi kwa wafanyabiashara.

Mkurugenzi wa Utawala na Fedha kutoka BRELA, Bw. Bakari Mketu amesema mara baada ya kutoa elimu ya usajili miezi miwili iliyopita kiwango cha usajili kimeongezeka na kufikia asilimia 80 ya lengo walilojiwekea kwa robo zote tatu ndani ya mwaka .

“Tumesajili kampuni 4678  zaidi ya  66% huku malengo yakiwa kusajili 7110 na kusajili majina ya biashara 8022 zaidi ya  49%  huku malengo yakiwa kusajili majina 1640 kwa robo zote tatu  .... kwanza tulikuwa tunapanda taratibu ...tutaendelea kuwaelimisha wateja wetu ili kuhakikisha wateja wote wanakuwa uelewa wa kutosha.

Katika hatua nyingine Mketu ametoa rai kwa wanasheria kuzingatia sheria katika utekelezaji wa majukumu yao ikiwa ni pamoja na masuala yanayohusiana na Usajili, ili kuepuka usumbufu kwa wafanyabiashara.

‘’Sheria ni taaluma ambayo bado inaheshimika sana, kujifunza kila siku ndio taaluma inavyotaka sisi hatuwezi kuwafundisha kazi…lakini tunaomba wazingatie sheria wakati wakifanya majukumu yao, mathalani kuna mwanasheria alifanya zoezi la kubadili hisa za mteja (share transfer) pasipo kufuata utaratibu ambao umeainishwa kisheria na TRA”  alisema Mketu.

Naye Suzana Senso kutoka BRELA amesema ni vema Wanasheria wanapofanya kazi kujiridhisha kwanza juu ya taratibu na sheria zinazotakiwa kufuatwa katika kazi husika ili waweze kuwasadia wateja wao kwa kuzingatia sheria na taratibu.

“Naomba nitoe rai kwa wanasheria, ukipata kazi uliza  wengine taratibu zilivyo  ili uweze kumsaidia mteja, huyu mama alitaka kuhamisha hisa (share transfer) mwanasheria akaja akachomoa nyaraka na kuweka nyingine akamweleza kuwa utaratibu umekamilika wakati utaratibu ulipaswa ufanyike TRA; kutokana na uelewa  wa mama na afisa biashara mkoa wao walitutafuta, najiuliza ni wangapi wanakutana na changamoto hizi” alihoji Bi. Suzan Senso. 

Aidha, Bi. Elizabeth Samweli kutoka Kampuni ya Mlashi General Supplies alikiri kukumbwa na changamoto hiyo ya  mwanasheria  kufanya zoezi la kuhamisha hisa pasipo kufuata utaratibu uliowekwa kisheria na kushukuru BRELA kwa namna walivyomsaidia mara baada ya kuwaeleza changamoto hiyo; huku akisisitiza BRELA kuendelea kutoa elimu.

Maafisa kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) wako Mjini Bariadi Simiyu kwa ajili ya kuendelea kutoa elimu juu ya usajili wa biashara kwa wafanyabiashara mkoani hapa pamoja na wajasiriamali walio katika Mkutano Mkuu wa 20 wa Chama cha Waadventista Wasabato(ATAPE) ambao unafanyika Mkoani Simiyu.

MWISHO

Mkurugenzi wa Utawala na Fedha kutoka BRELA, Bw. Bakari Mketu na Bi. Suzan Senso wakifuahia jambo na Bi. Elizabeth Samweli kutoka Kampuni ya Mlashi General Supplies mfanyabiashara wa Mjini Bariadi walipomtembelea dukani kwake, wakati wakiwa katika ziara kutembelea wafanyabiasara na kutoa elimu juu ya masuala ya usajili, ikiwemo matumizi ya mfumo mpya wa usaji kwa njia ya mtandao(Online Registration System-ORS).

Mkurugenzi wa Utawala na Fedha kutoka BRELA, Bw. Bakari Mketu akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya ziara yake kutembelea wafanyabiasara na kutoa elimu juu ya masuala ya usajili, ikiwemo matumizi ya mfumo mpya wa usaji kwa njia ya mtandao(Online Registration System-ORS)..Mjini Bariadi Simiyu.
Bi. Suzan Senso kutoka BRELA(kulia) akimsikiliza Bi .Neema Joseph Meneja wa Kituo cha Mafuta cha JBS Mjini Bariadi wakati wa ziara yake na Mkurugenzi wa Utawala na Fedha kutoka BRELA, Bw. Bakari Mketu kwa wafanyabishara iliyolenga kutoa elimu juu ya masuaa ya usajili ikiwemo matumizi ya mfumo mpya wa usaji kwa njia ya mtandao(Online Registration System-ORS)..
Bi. Suzan Senso kutoka BRELA(kulia) akiangali nyaraka za Usajili wa Hoteli ya Sweet Dream wakati wa ziara yake na Mkurugenzi wa Utawala na Fedha kutoka BRELA, Bw. Bakari Mketu kwa wafanyabishara iliyolenga kutoa elimu juu ya masuala ya usajili ikiwemo matumizi ya mfumo mpya wa usaji kwa njia ya mtandao (Online Registration System-ORS) (kushoto) ni Mkurugenzi Msaidizi wa Sweet Dream Hotel  Bi.Lucy Sabu.

0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!