Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani na
maradhi ya moyo kutoka Wizara ya afya Prof. Harun Nyagori ametoa wito kwa
Watanzania kutochanganya dawa za hospitali na kienyeji wakati wa matibabu yao
ili kuepuka athari kubwa za kiafya zinazoweza kujitokeza.
Prof Nyagori ameyasema hayo Aprili 18,
2019 wakati akizungumza na
waandishi wa habari katika Mkutano Mkuu wa chama cha wanataaluma na
wajasiriamali wa Kanisa la Waadventista Wasabato(ATAPE),unaofanyika mjini
Bariadi.
Amesema kuwa uchanganyaji wa dawa za
hospitali na za kienyeji ni hatari kwa afya ya binadamu, hivyo ni vema wagonjwa
mbalimbali wa magonjwa ya ndani na maradhi ya moyo kuamua kufanya maamuzi ya
matumizi ya dawa upande mmoja ili wasije kujisababishia madhara makubwa zaidi.
“Ni vema wagonjwa wasichanganye dawa za
hospitali na za kienyeji, japo dawa nyingi za hospitali zinatengenezwa na
Mitishamba lakini utofauti wa dawa za hospitali na dawa za kienyeji ni kwamba wanapotumia
dawa za kienyeji wanatumia pasipokujua kiwango cha kemikali zilizopo na aina ya
sumu iliyopo kwenye dawa hizo”
“Nimeona wagonjwa wengi wanaochanganya
dawa za hospitali na za kienyeji wanapata madhara mbalimbali mwilini, wengine
figo zao zimeshindwa kufanya kazi vizuri, wengine maini yameharibika, sukari
imezidi kupanda; kwa hiyo nawashauri kama wakiamua kutumia dawa za hospitali
watumie hizo na kama wameamua kutumia mitishamba wazitumie hizo tu wasichanganye”
alisema Dkt. Nyagori.
Sambamba na hilo Prof Nyagori, pia
amesema kuwa katika siku sita za mkutano mkuu wa ATAPE unaoendelea Mkoani
Simiyu, ametoa wito kwa wananchi na wakazi wa Simiyu kujitokeza kwa wingi
kupima afya zao.
Ameongeza kuwa ndani ya siku mbili
ambazo wamekuwa wakitoa huduma hizo za magonjwa ya ndani na maradhi ya moyo, jumla
ya wagonjwa 269 walijitokeza kupima afya zao na kati ya hao 103 waligundulika
kuwa shinikizo la damu,62 walikuwa na sukari na 140 wenye uzito uliopindukia.
Nao baadhi ya wananchi waliojitokeza
kupima afya zao wameshukuru huduma hizo kutoka kwa madaktari bingwa kusogezwa
karibu yao kupitia mkutano wa ATAPE huku wakieleza kufurahishwa na huduma hizo kutolewa
kwa gharama nafuu.
“Binafsi nimefurahishwa na huduma za
madaktari bingwa ambazo nimezipata kupitia mkutano huu wa ATAPE, nimepima na
nimeweza kujua afya yangu, kilichonifurahisha zaidi ni kwamba nimetumia
shilingi elfu kumi tu kupima shinikizo la damu, sukari na vipimo vingine”alisema
Mchungaji Marco Barnabas.
“Huduma zinazotolewa hapa ni nzuri na
zinatolewa kwa gharama nafuu kabisa nitoe wito kwa Wanasimiyu kujitokeza kwa
wingi kuja kupima afya zao, ili waweze kutambua hali za afya zao na kupata
ushauri wa wataalam bingwa” alisema Namkunda
Mburuja.
Mkutano Mkuu wa Mkuu wa chama cha
wanataaluma na wajasiriamali wa Kanisa la Waadventista
Wasabato(ATAPE),unaendelea mjini Bariadi
na unatarajiwa kuhitimishwa Jumapili ya tarehe 21/04/2019; wanataaluma
mbalimbali wanaendelea kutoa huduma, huku wajasirimali wakiendelea kuuza bidhaa
mbalimbali katika viwanja vya shule ya Sekondari Kusekwa memorial
MWISHO
Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani na
maradhi ya moyo kutoka Wizara ya afya, Prof. Harun Nyagori akimhudumia
Bi. Eveline Mshanga wakati alipokuwa akitoa huduma za magonjwa ya moyo katika
Mkutano wa ATAPE mjini Bariadi.
Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani na
maradhi ya moyo kutoka Wizara ya afya, Prof. Harun Nyagori akiwaelezea
jambo waandishi wa habari alipozungumza nao wakati akitoa huduma za magonjwa ya
moyo katika Mkutano wa ATAPE mjini Bariadi.
0 comments:
Post a Comment