Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Mawasiliano, Dkt. Jim Yonaz
amemkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka kompyuta 100 na vifaa
vingine zikiwemo printa 10, vilivyotolewa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF),
vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 220.
Makabidhiano hayo yamefanyika Aprili 09,
2019 katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mjini Bariadi na kushuhudiwa na
baadhi ya Wakuu wa Taasisi za Umma, Wakuu wa shule na baadhi ya wanafunzi wa
Shule ya Sekondari Bariadi.
Akikabidhi kompyuta hizo Dkt. Yonaz
amewapongeza viongozi mkoani Simiyu kwa kuendelea kufanya ubunifu katika
masuala mbalimbali yanayouwezesha mkoa kukua katika nyanja mbalimbali hususani
katika uchumi na elimu.
Aidha, amesema Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano itaendelea kushirikiana na Mkoa wa Simiyu kuharakisha
maendeleo kupitia Sayansi na Teknolojia.
" Ninaamini kompyuta hizi
zitawasaidia sana wanafunzi hawa na walimu pia yapo mambo yatakayotatuliwa
kupitia kompyuta hizi, ili tuweze kuleta elimu bora, tutengeneze wasomi wazuri
ambao watachangia katika uchumi wa Taifa letu" alisema Dkt. Yonaz.
Akipokea kompyuta hizo Mkuu wa Mkoa wa
Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka ameshukuru kwa msaada huo huku akibainisha kuwa
lengo la Mkoa ni kuwa mkoa ambao uko kiganjani ambao taarifa yoyote inaweza
kupatikana muda wowote.
“Tungehitaji mfahamu kuwa sisi ni miongoni
mwa mikoa michache sana Tanzania yenye Mpango Mkakati wa TEHAMA wa mkoa na (focus)
lengo letu kama mkoa ni kuwa mkoa ambao uko kiganjani, mkoa ambao mtu ataweza kupata
taarifa yoyote wakati wowote” alisema Mtaka.
Mkurugenzi Mkuu wa UCSAF, Mhandisi.
Peter Ulanga amesema UCSAF kwa kushirikiana na Wakala wa Serikali Mtandao
inaandaa mpango wa kutoa mafunzo kwa Maafisa TEHAMA ili kuwawezesha kutekeleza
majukumu yao kibunifu.
Nao walimu na wanafunzi wa shule za
sekondari mkoani Simiyu wameishukuru Serikali kutoa kompyuta hizo na kueleza
namna zitakavyowasaidia.
"Kompyuta hizi kwanza zitatusaidia
kuwezesha mawasiliano hususani katika masuala ya intaneti kwa ajili ya kutuma
na kupokea taarifa mbalimbali kwa wakati na kuchapa majaribio ya
wanafunzi" Mkuu wa Shule ya Sekondari Itilima, Mwl.Flora Shimbi.
"Vifaa hivi vitasaidia sana
wanafunzi kujifunzia kwa vitendo wawapo shuleni na kutafuta 'notes' za masomo
mbalimbali ili waweze kujifunza" Mkuu wa Shule ya Sekondari Bariadi, Mwl.Ally
Simba
"Hizi kompyuta zitatusaidia
kujifunza kwa vitendo na tutaelewa zaidi kuliko kama tungesoma bila kompyuta,
kila atakachokuwa anafundisha mwalimu tutakuwa tunakiona moja kwa moja" alisema
Naomi Mathias Mwanafunzi kutoka Shule ya Sekondari Bariadi.
Kompyuta hizo pamoja na vifaa
vingine vimekabidhiwa kwa baadhi ya Wakuu wa Taasisi, Ofisi za wakuu wa Wilaya,
Ofisi ya mkuu wa mkoa na baadhi ya wakuu wa shule za Sekondari mkoani hapa
mkoani.
MWISHO.
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Mawasiliano, Dkt. Jim Yonaz(kulia) akimkabidhi
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka moja ya kompyuta 100 zilizotolewa na
Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwa Mkoa wa Simiyu.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony
Mtaka akimkabidhi Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini moja ya kompyuta 100 zilizotolewa na Mfuko wa
Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwa niaba ya Ofisi ya Mkoa wa Simiyu.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony
Mtaka akimkabidhi Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Maswa, Mwl. Kuyunga
Jackson moja ya kompyuta 5 zilizotolewa na mkoa kwa shule hiyo kutoka katika
kompyuta 100 Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Mkoa wa Simiyu.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony
Mtaka (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wakuu wa shule, wanafunzi
wa shule ya sekondari Bariadi na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano anayeshughulikia Mawasiliano, Dkt. Jim Yonaz na Mtendaji Mkuu wa
Mfuko wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF), Mhandisi. Peter Ulanga baada ya
makabidhiano ya kompyuta 100, printa 10 na vifaa vingine vilivyotolewa na UCSAF
kwa mkoa wa Simiyu.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony
Mtaka(kulia) akimkabidhi Kaimu Mkuu wa Jeshi la Zimamoto Mkoa wa Simiyu moja
ya kompyuta 5 zilizotolewa na mkoa kwa shule hiyo kutoka katika kompyuta 100 Mfuko
wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Mkoa wa Simiyu.
Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano
kwa wote (UCSAF), Mhandisi. Peter Ulanga(wa tatu kulia), Mkuu wa Mkoa wa
Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano anayeshughulikia Mawasiliano, Dkt. Jim Yonaz na Katibu Tawala Mkoa
wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini wakiwa katika picha moja baadhi ya wanafunzi wa
Shule ya sekondari Bariadi, baada ya makabidhiano ya kompyuta 100, printa 10 na
vifaa vingine vilivyotolewa na UCSAF kwa mkoa wa Simiyu.
Kutoka kulia Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa
Mawasiliano kwa wote (UCSAF), Mhandisi. Peter Ulanga, Naibu Katibu Mkuu, Wizara
ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Mawasiliano, Dkt. Jim Yonaz
na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka wakifurahia jambo na baadhi ya
wanafunzi wa Shule ya sekondari Bariadi kabla ya makabidhiano ya kompyuta 100,
printa 10 na vifaa vingine vilivyotolewa na UCSAF kwa mkoa wa Simiyu.
Sehemu ya kompyuta 100 , printa 10 na vifaa vingine vilivyotolewa na Mfuko wa
Mawasiliano kwa wote (UCSAF) kwa mkoa wa Simiyu na kukabidhiwa kwa Mkuu wa Mkoa
wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka Aprili
09,2019.
0 comments:
Post a Comment