Sunday, March 26, 2017

SULUHU YA MGOGORO WA MWEKEZAJI MWIBA HOLDINGS NA WANANCHI MEATU YAPATIKANA

Hatimaye suluhu ya mgogoro baina ya mwekezaji wa kampuni ya  MWIBA Holdings na wananchi wa vijiji saba vinavyounda Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori (WMA) ya Makao wilayani Meatu,  juu ya utata wa mkataba wa kumiliki ardhi, uanzishwaji wa ranchi ,mahusiano mabovu  na kusogezwa  kwa alama za mipaka katika makazi ya wananchi  imepatikana

Suluhu hiyo imepatikana baada ya kufanyika kikao cha pamoja wilayani Meatu kati ya Kamati ya Siasa ya CCM, Viongozi na Watendaji wa Serikali (Wilaya ya Meatu na Mkoa wa Simiyu), Mwakilishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Watendaji wa Kampuni ya MWIBA Holdings na Viongozi wa Vijiji vinavyounda Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Makao, ambacho kimeongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka

 Pande zote mbili (Mwekezaji na wananchi) zimekubaliana kuondoa kesi inayohusu mgogoro huo kwa Msuluhishi Jaji Mstaafu Thomas Mihayo na kurejea tena katika meza ya  maridhiano ili kujadili namna ya kuondoa tofauti na dosari zote zilizoonekana awali.

Mtaka ameipongeza Kampuni ya MWIBA Holdings kurejea katika meza ya mariadhiano na wananchi na ameagiza kufanyika mabadiliko katika Menejimenti ya Kampuni hiyo  kwa kuwa baadhi ya watendaji wametajwa kuwa chanzo cha   migogoro  ambayo imekuwa ikiwanufaisha wao wenyewe  huku ikichochea uhasama kati ya kampuni hiyo na wananchi

“....Nawaeleza Wakurugenzi, baadhi ya wasaidizi wenu wanawachafua sana, wanatengeneza migogoro na wananchi wetu kwa manufaa yao wenyewe; mkitaka kufanya kazi na sisi chukueni hatua kwa watumishi wenu, tunataka wawekezaji lakini hatuko tayari kuona wananchi wananyanyaswa kwa namna yoyote ile” alisema Mtaka.

Naye Mbunge wa Jimbo la Meatu Salum Khamis amesema  nia yake ni kuona wananchi hawabugudhiwi hivyo akatoa rai kuwa maridhiano yatakayofanyika kati ya pande hizo mbili yafanyike kwa umakini sana ili makubaliano yatakayofikiwa yalinde haki za wakazi wa Meatu na yasiwe chanzo cha migogoro.

Wakati huo huo baadhi ya wananchi wamesema mipaka waliyoshiriki kuweka wakati wa uanzishwaji wa Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori (WMA) ya Makao, ilitolewa kinyemela na watumishi wakiwemo viongozi wa Jumuiya hiyo kwa kushirikiana na mwekezaji huyo na kusogeza  nyuma alama hizo kwa kilomita 10 kutoka eneo la hifadhi kuelekea eneo la makazi ya wananchi

Wananachi hao wamesema kuwa mipaka ambayo imekuwa ikileta migogoro ni mpaka ulioko katika kijiji cha Bulongoja kwenye bikoni namba 314, ambapo walisema kuwa bikoni hiyo iliondolewa na kusogezwa nyuma zaidi ya kilometa 10 kutoka ndani ya hifadhi kuelekea kwenye makazi yao.

Akitoa ufafanuzi wa suala hilo, Katibu Tawala Mkoa, Ndg.Jumanne Sagini amesema atatuma timu ya wataalam Ngazi ya Mkoa ambao watashirikiana na wataalam wa wilaya ya Meatu watakaokwenda kuhakiki mipaka hiyo  kwa kuzingatia ramani na kuirejesha ilipokuwa, huku akisisitiza wataalam hao kuzingatia weledi.

Kwa upande wake Mkurugenzi kutoka Kampuni ya Mwiba Holdings Company  Abdulkadir Mohamed  amekubali kumaliza mgogoro huo na kufanya mabadiliko ya menejimenti yake  ili waweze  kufanya uwekezaji wa utalii na mazingira kwa uhuru.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Mhe.Dkt.Titus Kamani amewaasa viongozi na watendaji  wa Serikali mkoani humo kutekeleza wajibu wao katika kuwaletea wananchi maendeleo na wasiruhusu kwa namna yoyote migogoro ikachukua nafasi kubwa kuliko maendeleo ya wananchi.

Jumuiya Hifadhi ya wanyamapori (WMA) Makao inaundwa na vijji saba ambavyo ni Makao, Sapa, Mwangudo, Mbushi, Iramba ndogo, Jinamo na Mwabagimu.

 
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na  Kamati ya Siasa ya CCM, Viongozi na Watendaji wa Serikali (Wilaya ya Meatu na Mkoa wa Simiyu), Watendaji wa  Mwekezaji Kampuni ya MWIBA   Holdings na Viongozi wa Vijiji vinavyounda Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Makao(hawapo pichani) katika kikao cha kutafuta suluhu ya mgogoro wa mwekezaji huyo wananchi wilayani Meatu.
Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM, Viongozi na Watendaji wa Serikali (Wilaya ya Meatu na Mkoa wa Simiyu) na Viongozi wa Vijiji vinavyounda Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Makao wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka (hayupo pichani) katika kikao cha kutafuta suluhu ya mgogoro wa mwekezaji wa Kampuni ya MWIBA Holdings  na wananchi wilayani Meatu.
Watendaji wa Kampuni ya  MWIBA Holdings (waliokaa sehemu ya juu) wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka (hayupo pichani) katika kikao kilichofanyika  kutafuta suluhu ya mgogoro wa mwekezaji huyo na wananchi wilayani Meatu.
Mbunge wa Jimbo la Meatu Salum Khamis akizungumza na Kamati ya Siasa ya CCM, Viongozi na Watendaji wa Serikali (Wilaya ya Meatu na Mkoa wa Simiyu), Watendaji wa Kampuni ya MWIBA  na Viongozi wa Vijiji vinavyounda Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Makao(hawapo pichani) katika kikao cha kutafuta suluhu ya mgogoro wa mwekezaji huyo wananchi wilayani Meatu.
Mwenyekiti wa kijiji cha Makao akichangia jambo katika kikao kilichofanyika kwa lengo la kutafuta suluhu ya mgogoro kati ya Kampuni ya MWIBA Holdings na wananchi wa Makao kilichofanyika Wilayani Meatu.
Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Ndg.Jumanne Sagini akifafanua jambo katika kikao kilichofanyika wilayani Meatu kwa lengo la kutafuta suluhu ya mgogoro kati ya Kampuni ya MWIBA Holdings na wananchi wa Makao wilayani humo.

Mkuu wa Wilaya ya Meatu,Mhe.Dkt.Joseph Chilongani akifafanua jambo katika kikao kilichofanyika wilayani humo kwa lengo la kutafuta suluhu ya mgogoro kati ya Kampuni ya MWIBA Holdings na wananchi wa Makao.


Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu,Ndg. Fabian Manoza  akifafanua jambo katika kikao kilichofanyika wilayani humo  kwa lengo la kutafuta suluhu ya mgogoro kati ya Kampuni ya MWIBA Holdings na wananchi wa Makao
Mwenyekiti wa  CCM Mkoa wa Simiyu, Dkt. Titus Kamani akifafanua jambo katika kikao kilichofanyika wilayani Meatu kwa lengo la kutafuta suluhu ya mgogoro kati ya Kampuni ya MWIBA na wananchi wa Makao wilayani humo.
Mkurugenzi kutoka Kampuni ya MWIBA Holding, Ndg. Abdulkadir Mohamed akifafanua jambo katika kikao kilichofanyika wilayani humo kwa lengo la kutafuta suluhu ya mgogoro kati ya Kampuni hiyo na wananchi wa Makao-Meatu.

): Katibu wa CCM Mkoa wa Simiyu, Joyce Masunga akifafanua jambo katika kikao kilichofanyika wilayani Meatu kwa lengo la kutafuta suluhu ya mgogoro kati ya Kampuni ya MWIBA na wananchi wa Makao wilayani humo, (kulia) Mwenyekiti wa CCM Meatu, Mhe.Juma Mwibuli.
Katibu wa Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Makao, Robert Simon akiwasilsha taarfa ya Jumuiya hiyo katika kilichofanyika wilayani Meatu kwa lengo la kutafuta suluhu ya mgogoro kati ya Kampuni hiyo na wananchi wa Makao-Meatu.
Baadhi ya wananchi wakitoa maelezo ya kusogezwa kinyemela kwa mipaka ya Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Makao tofauti na ile ya awali walioshuhudia ikiwekwa wakati wa uanzishwaji wa jumuiya hiyo, katika kikao ilichofanyika kwa lengo la kutafuta suluhu ya mgogoro kati ya Kampuni hiyo na wananchi wa Makao-Meatu.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) na Mbunge wa Jimbo la Kisesa wilaya ya Meatu akichangia jambo katika kikao kilichofanyika wilayani humo kwa lengo la kutafuta suluhu ya mgogoro kati ya Kampuni ya MWIBA na wananchi wa Makao wilayani humo.

0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!