Friday, June 8, 2018

KONGWA WAFANYA ZIARA MKOANI SIMIYU KUTEMBELEA MIRADI YA VIJANA ILI KUJIFUNZA


Viongozi kutoka Wilaya ya Kongwa Mkoani Dodoma wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Mhe. Deo Ndejembi pamoja na baadhi ya viongozi wa vikundi vya vijana wilayani humo wamefanya ziara Mkoani Simiyu ili kujifunza namna vikundi vya vijana vinavyotekeleza miradi yake.

Timu hiyo imefanya ziara ya siku mbili hadi Juni 08, 2018  katika miradi inayotekelezwa na vijana kwa kushirikiana na Halmashauri ambayo ni Kiwanda cha Chaki,  Kiwanda cha kutengeneza bidhaa za ngozi wilayani Maswa na Mradi wa kiwanda cha kusindika maziwa wilayani Meatu.

Mkuu wa wilaya ya Kongwa amesema wameamua kuja Simiyu kwa kuwa vikundi vyake vimeonekana vikifanya vizuri katika miradi yake, hivyo wamewaleta vijana wao ili wapate uzoefu na ari itawasukuma kubuni miradi yao na kujua namna bora ya kuiendesha.

"Tumeona tuje tujifunze kutoka Simiyu maana mkoa wa Simiyu umeonesha mfano wa namna vikundi vya vijana vinavyotakiwa kutekeleza miradi yake, tumeona kwenye vyombo vya habari na kwingineko mkipata sifa nyingi kutokana na miradi yenu kuonesha matokeo, nia yetu vijana waje waone wajifunze wapate hasira ya kufanya kitu cha kwao" alisema Ndejembi.

Ndejembi amesema ni matamanio yake kuona vijana wa Kongwa wanaanzisha miradi ya viwanda kama ilivyo kwa Maswa na Meatu kwa kuwa wilaya hiyo ndiyo inayofanya vizuri katika kilimo na ufugaji Mkoani Dodoma ambapo uzalishaji wa malighafi ya viwanda hivyo uko vizuri pia.

Ameongeza kuwa baada ya ziara hiyo vijana wake wamejifunza hivyo watakapofika wilayani Kongwa wataenda kufanya miradi ambayo itakuwa ya mfano na endelevu kwa kuwa tayari wana wafadhili waliokubali kutoa fedha kwa ajili ya kuanzisha miradi hiyo.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, Dkt. Omary Nkullo amesema Halmashauri itahakikisha inatoa fedha kuwawezesha vijana kutekeleza miradi yao na itawasimamia ili waweze kufikia ndoto zao.

Akizungumza kwa niaba ya vijana kutoka Kongwa waliofika Simiyu kujifunza, Bw. Zamoyoni George amesema kuja kwao Simiyu hakutakuwa bure bali itakuwa chachu ya kuanzisha miradi endelevu na yenye tija ambayo hata vijana wa Simiyu wataenda kujifunza kwao.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Mhe. Dkt. Seif Shekalaghe amewapongeza wilaya ya Kongwa kuona umuhimu wa kujifunza na kuwashauri kuwa fedha wakazozitoa kwa vijana kupitia asilimia tano za mapato ya Halmashauri, zielekezwe kutekeleza miradi ambayo italeta tija na kurejesha fedha za Halmashauri kwa wakati.

Aidha, Dkt. Shekalaghe amesema  Maswa itaendelea kuboresha ubora na biashara ya chaki (MASWA CHALKS)  na kuomba Wilaya ya Kongwa kuanza kununua Chaki za Maswa na kutumia katika shule zake, huku akisisitiza timu hiyo ya Kongwa pia kwenda kutangaza bidhaa za Ngozi zinazozalishwa Kijiji cha Senani wilayani humo.

Mkurugenzi wa Wilaya ya Meatu, Bw. Fabian Manoza akitoa maelezo juu ya  kiwanda cha maziwa amesema Halmashauri ina mpango wa kukipanua kiwanda hicho na Benki ya Maendeleo ya Kilimo imekubali kutoa mkopo wa shilingi bilioni 6 kwa ajili ya upanuzi wa kiwanda hicho na kuboresha teknolojia ya uzalishaji ili kifikie uwezo wa kuzalisha lita 15,000 kwa siku kutoka lita 800 za sasa.

Mkoa wa Simiyu ni mkoa uliojipambanua kama mkoa wa Viwanda kupitia Falsafa yake ya “Wilaya Moja Bidhaa Moja Kiwanda Kimoja” ambapo umedhamiria kujenga uchumi wa viwanda kwa kutumia malighafi yake inapatikana hapa nchini.

Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Mhe. Dkt. Seif Shekalaghe (katikati)akitoa maelezo kwa Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Mhe. Deo Ndejembi na baadhi ya vijana kutoka Kongwa waliofika kutembelea kiwanda cha chaki wilayani humo, wakati wa ziara yao ya kutembelea miradi ya vijana Mkoani Simiyu kwa lengo la kujifunza.
Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Mhe. Dkt. Seif Shekalaghe(kulia) akimuonesha  Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Mhe. Deo Ndejembi kiatu kilichotengenezwa na Kikundi cha Vijana Senani wilayani Maswa, wakati wa ziara ya Viongozi na Vijana wa Wilaya ya Kongwa kutembelea miradi ya vijana Mkoani Simiyu kwa lengo la kujifunza.
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Mhe. Deo Ndejembi (kushoto) akiangalia chupa ya maziwa yanayosindikwa wilayani Meatu, baada ya kutembelea Kiwanda cha kusindika maziwa ‘Meatu Milk’ wakati wa Ziara yake na vijana wa Wilaya ya Kongwa ya kutembelea miradi ya vijana Mkoani Simiyu kwa lengo la kujifunza.
Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Meatu, Bw. Fabian Manoza akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Mhe. Deo Ndejembi zawadi ya maziwa, mara baada ya kutembelea Kiwanda cha Kusindika Maziwa wilayani humo,  wakati wa Ziara yake na vijana wa Wilaya ya Kongwa ya kutembelea miradi ya vijana Mkoani Simiyu kwa lengo la kujifunza.
Mmoja wa Vijana kutoka kikundi cha Maswa Family akitoa maelezo kwa Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Mhe. Deo Ndejembi na baadhi ya vijana kutoka Kongwa(wa tatu kulia) waliofika kutembelea kiwanda cha chaki wilayani humo, wakati wa ziara yao ya kutembelea miradi ya vijana Mkoani Simiyu kwa lengo la kujifunza
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Mhe. Deo Ndejembi (wa pili kulia) akiuliza jambo wakati alipotembea eneo la kufungashia chaki wakati alipotembelea kiwanda cha chaki wilayani Maswa, wakati wa ziara yao ya kutembelea miradi ya vijana Mkoani Simiyu kwa lengo la kujifunza.
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Mhe. Deo Ndejembi (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Mhe. Dkt. Seif Shekalaghe(kushoto) na Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Mhe.Dkt. Joseph Chilongani mara baada ya kumaliza ziara yake pamoja na viongozi wa Vijana wa wilaya ya Kongwa iliyokuwa na lengo la kutembelea miradi ya vijana Mkoani Simiyu kwa lengo la kujifunza.
Vijana kutoka Wilaya ya Kongwa wakipata maelezo ya hatua mbalimbali za utengenezaji wa viatu walipotembelea kiwanda cha kutengeneza bidhaa za ngozi kilichopo Kijiji cha  Senani wilayani Maswa, wakati wa ziara yao ya kutembelea miradi ya vijana Mkoani Simiyu kwa lengo la kujifunza, (kulia) Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kongwa, Dkt. Omary Nkullo.
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Mhe. Deo Ndejembi (kushoto) akizungumza na Viongozi wa Kikundi cha Vijana Senani wilayani Maswa (hawapo pichani) wakati wa ziara ya Viongozi na Vijana wa Wilaya ya Kongwa ya kutembelea miradi ya vijana Mkoani Simiyu kwa lengo la kujifunza.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Bw. Fabian Manoza(kulia) akitoa maelezo kwa Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Mhe. Deo Ndejembi(kushoto) na baadhi ya vijana kutoka Kongwa waliofika kutembelea kiwanda cha maziwa(Meatu Milk) wilayani humo, wakati wa ziara yao ya kutembelea miradi ya vijana Mkoani Simiyu kwa lengo la kujifunza.
Vijana kutoka Wilaya ya Kongwa wakipata maelezo ya hatua mbalimbali za utengenezaji wa viatu walipotembelea kiwanda cha kutengeneza bidhaa za ngozi kilichopo Kijiji cha  Senani wilayani Maswa, wakati wa ziara yao ya kutembelea miradi ya vijana Mkoani Simiyu kwa lengo la kujifunza, (wa pili kulia) Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kongwa, Dkt. Omary Nkullo.
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Mhe. Deo Ndejembi (wa pili kushoto) akizungumza na Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Mhe. Dkt. Joseph Chilongani (kulia) wakati wa Ziara yake na vijana wa Wilaya ya Kongwa ya kutembelea miradi ya vijana Mkoani Simiyu kwa lengo la kujifunza.

0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!