Moto ambao hadi
sasa chanzo chake hakijafahamika umeteketeza maduka nane , stoo pamoja na mali
za wafanyabiashara ambazo thamani yake
haijafahamika, katika Mji mdogo wa Lamadi wilaya ya Busega Mkoani Simiyu ,
usiku wa tarehe 02 Juni.
Akizungumzia jinsi
moto huo ulivyoanza mmoja wa wakazi wa Lamadi aliyeshuhudia tukio hilo, Bw.
John Balele amesema moto ulianza kuwaka katika moja ya chumba cha duka majira
ya saa mbili usiku na baadaye ukaanza kusambaa katika vyumba vingine lakini
hawakuweza kufahamu chanzo chake maana vyumba vyote vilikuwa vimefungwa.
“Huu moto umetokea
majira ya saa mbili hivi tulivyouona tukapiga simu polisi, askari polisi wakaja
na askari wa zimamoto, watu wa Zimamoto wamejitahidi kuwahi kufika na
wametusaidia sana kutuelekeza namna ya kukabiliana na moto huu tukafanikiwa kuuzima
na kuokoa baadhi ya mali japo mali
nyingi zimeteketea; binafsi nawashukuru sana wananchi wenzangu wa Lamadi kwa
moyo wao wa kujitolea” alisema John Balele.
Diwani wa kata ya Lamadi,
Mhe. Laurent Bija amewashukuru wananchi kwa namna walivyojitoa kushirikiana na
jeshi la polisi na kikosi cha Zimamoto na uokoaji katika kuukabili moto huo na
kulinda baadhi ya mali zilizookolewa kwa uaminifu .
Aidha, Diwani huyo
ametoa pole kwa wafanyabiashara ambao mali zao zimeteketea na akatoa wito kwa
wafanyabiashara wote katika Kata hiyo kuwa na vifaa vya kuzimia moto katika
maeneo yao ya biashara, ili viweze kuwasaidia katika hatua za awali za
kukabiliana na moto pindi unapotokea.
Akizungumza
wananchi wa Lamadi waliojitokeza kuzima moto huo wakishirikiana na Jeshi la
Zimamoto na Uokoaji na Jeshi la Polisi Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony
Mtaka amewapa pole wafanyabiashara ambao wamepoteza mali zao katika ajali hiyo
ya moto na akawashukuru wananchi wa Lamadi kwa ushirikiano na uaminifu
waliounesha wakati wa kuzima moto huo.
Mtaka
amesema kwa kuwa chanzo cha moto huo hakijafahamika Serikali kupitia TANESCO na
Zimamoto itaendelea kutafuta na kubaini chanzo na tarehe 03 Juni, 2018 Serikali
itafanya tathmini kujua madhara yaliyosababishwa na moto huo.
“
Nawapa pole wananchi wa Lamadi bado hatujajua chanzo hasa, wenzetu wa TANESCO
na Zimamoto watatusaidia kujua chanzo, kuhusu madhara kwa kuwa sasa ni usiku
kesho Serikali itafanya tathmini ili na sisi tuone namna ya kuzungumza na
wenzetu wa benki na kuona busara gani itumike kuwasaidia wafanyabiashara waliokopa
namna ya kurejesha, wakati wanajipanga upya” alisema
Mkuu
huyo wa Mkoa pia ametoa wito kwa Taasisi za Bima hapa nchini kupanua wigo na kuwafikia
wafanyabiashara na kuona namna sahihi ya kuwa msaada kwao pale wanapokutana na
majanga yasiyoepukika yakiwemo ya moto, huku akisisitiza wafanyabiashara
kuchukua tahadhari ya moto ikiwa ni pamoja na kuhakikisha vifaa vyote vya umeme
vimezimwa wanapofunga biashara zao.
Katika
hatua nyingine ametoa wito kwa Jeshi la
Zimamoto kuendelea kutoa elimu ya majanga ya moto hasa kwenye maeneo ya masoko
ili waweze kuchukua tahadhari ya moto na akawataka wale wanaojenga majengo ya
biashara kupata ushauri wa kitaalam juu ya ujenzi wa majengo yao.
Kamanda
wa Zimamoto Mkoa wa Simiyu, Gervas Fungamali amesema Jeshi la polisi
litaendelea kutoa elimu kwa wananchi hususani
juu ya umuhimu wa kuwa na vifaa vya kuzimia moto na kuchukua tahadhari ya moto
katika maeneo yao.
Moto
ukiteketeza baadhi ya maduka nane katika eneo la lamadi Wilayani Busega mkoani
Simiyu jana usiku.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akiangalia
moja ya vyumba vilivyoteketekea kwa moto Mjini Lamadi mara baada ya kufika eneo
la tukio jana usiku.
Baadhi
ya wananchi wa Lamadi wilayani Busega wakipakia kwenye gari baadhi ya mali
zilizookolewa wakati wa kuzima moto
ulioteketeza vyumba vinane vya maduka jana usiku.
Baadhi
ya wananchi wa Lamadi wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony
Mtaka(hayupo pichani) mara baada ya kuzimwa kwa moto ulioteketeza vyumba nane
vya maduka Mjini Lamadi jana usiku.
Kamanda
wa Zimamoto Mkoa wa Simiyu, Gervas Fungamali akizungumza na wananchi wa Lamadi
mara baada ya kuzimwa kwa moto ulioteketeza maduka nane MjiniLamadi wilayani
Busega jana usiku.
Baadhi
ya vyumba vinane vya maduka vilivyoungua na moto jana usiku
Mkuu
wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka(kushoto) akizungumza na waandishiwa
habari mara baada ya kuzimwa kwa moto
ulioteketeza vyumba nane vya maduka Mjini Lamadi jana usiku
Mkurugenzi
wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega, Bw. Anderson Njiginya akizungumza na Mkuu
wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka mara baada ya kufika eneo ambalo vyumba
nane vya maduka viliteketea kwa moto Mjini Lamadi.
0 comments:
Post a Comment