Wednesday, September 9, 2020

RAS SIMIYU ATAKA MAJENGO YA UPASUAJI, WODI YA WAZAZI HOSPITALI YA WILAYA BUSEGA YAKAMILISHWE

     Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bi. Miriam Mmbaga amemwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega, Bw. Anderson Njiginya kutoa fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa majengo ya upasuaji na wodi ya wazazi katika Hospitali ya Wilaya ili kuboresha hali ya utoaji wa huduma kwa wananchi katika hospitali hiyo. 

Mmbaga ametoa agizo hilo Septemba 09, 2020 wakati zoezi la usimamizi shirikishi alipotembelea hospitali hiyo kukagua maendeleo ya ujenzi wa majengo hayo ambayo yanapaswa kukamilika na kuanza kutoa huduma ifikapo Septemba 30, 2020.

“Nampongeza Mkurugenzi kwa kujiongeza, badala ya kusubiri kibali kutoka HAZINA kulipa fedha za kukamilisha ujenzi wa majengo haya, amejiwekea utaratibu wa kuwalipa mafundi wetu, nimeelekeza kuwa aongeze kiwango anachotoa kwa kila juma ili kuongeza kasi ya ujenzi na hatimaye majengo haya yaweze kukamilika na kutumika kwa huduma kusudiwa,” alisema Mmbaga.

Aidha, Mmbaga ameongeza kuwa ukamilishaji wa majengo hayo uende sambamba na utunzaji wa mazingira ambao utajumuisha upandaji miti, bustani za maua na utunzaji wa miti asili huku akitoa pongezi kwa Mhandisi wa Ujenzi wa Halmashauri hya Wilaya ya Busega kwa usimamizi mzuri katika ujenzi wa hospitali hiyo na kumuagiza Mkurugenzi kumthibitisha katika cheo chake.

Wakati huo huo Mmbaga ameelekeza Timu ya usimamizi wa afya ngazi ya wilaya (CHMT) kuimarisha usimamizi katika mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) uliboreshwa hususani watoa huduma ngazi ya jamii wanaohusika katika usajili ili wananchi waweze kupata huduma zilizokusudiwa  na serikali.

Katika hatua nyingine Mmbaga ametembelea kikundi kinachojihusisha kilimo cha umwagiliagi kilichopo kijiji cha Chamgasa na kuelekeza wataalam wa fedha na uchumi waweze kutoa elimu kwa wakulima hao juu ya utunzaji na matumizi ya fedha ili wanapopewa mikopo na wadau waweze kutekeleza miradi ambayo itakuwa endelevu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega, Bw. Anderson Njiginya amesema atahakikisha fedha zinatolewa kwa wakati kwa mafundi wanaoendelea na ujenzi wa majengo ya Upasuaji na wodi ya wazazi katika hospitali ya wilaya ili shughuli za ujenzi zisikwame.

Kwa upande wake Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dkt. Khamis Kulemba ameipongeza Timu ya usimamizi wa afya ngazi ya wilaya (CHMT) kwa namna inavyotekeleza majukumu yake huku akisisitiza watumishi wote wa afya kuendelea kutoa huduma stahiki  kwa wananchi.

Nao baadhi ya watumishi wa afya katika kituo cha afya Lukungu wameomba miundombinu katika vituo vya kutolea huduma za afya iboreshwe ili kutoa huduma kulingana na hadhi za vituo hivyo na wananchi wapate huduma wanazotarajia kuzipata katika vituo husika.

MWISHO.

Katibu tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bi. Miriam Mmbaga akizungumza na baadhi wajumbe wa Timu ya usimamizi wa masuala ya afya mkoa wa Simiyu na wilaya ya Busega wakati wa ziara ya Katibu Tawala wa Mkoa iliyolenga kufanya usimamizi shirikishi katika hospitali hiyo kukagua maendeleo ya ujenzi wa majengo hayo ambayo yanapaswa kukamilika na kuanza kutoa huduma ifikapo Septemba 30, 2020.
Mhandisi wa Ujenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega akitoa maelezo kwa Katibu tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bi. Miriam Mmbaga katika jengo la mionzi la Hospitali ya Wilaya hiyo wakati wa ziara ya Katibu Tawala wa Mkoa iliyolenga kufanya usimamizi shirikishi katika hospitali hiyo kukagua maendeleo ya ujenzi wa majengo hayo ambayo yanapaswa kukamilika na kuanza kutoa huduma ifikapo Septemba 30, 2020.

TAFADHALI TAZAMA PICHA MBALIMBALI KATIBU TAWALA WA MKOA AKIWA KATIKA USIMAMIZI SHIRIKISHI, ALIPOKUTANA NA WATUMISHI IDARA YA AFYA, KIKUNDI CHA UMWAGILIAJI CHAMGASA NA PICHA ZA BAADHI YA MAJENGO YA HOSPITALI YA WILAYA YA BUSEGA



















0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!