Thursday, January 19, 2017

BENKI YA NMB YAKUBALI KUTOA MKOPO KUFANIKISHA KILIMO CHA UMWAGILIAJI BUSEGA

Na Stella Kalinga
Benki ya NMB imesema iko tayari kutoa mkopo kwa ajili ya kufanikisha kutekelezaji wa mradi wa Kilimo cha Umwagiliaji unaotarajiwa kuanza kutekelezwa mwaka huu katika wilaya ya Busega Mkoani Simiyu.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Idara ya Kilimo Biashara wa Benki wa Benki ya NMB, Bw. Saif Ahmed katika kikao Maalum kilichofanyika Makao makuu ya Benki hiyo Jijini Dar es Salaam kati ya Uongozi wa Benki hiyo na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Simiyu ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Mhe.Anthony Mtaka.

Mtaka amesema kwa kuwa wilaya ya Busega ina maji ya uhakika kutoka Ziwa Victoria serikali imedhamiria kukifanya kilimo cha umwagiliaji kuwa kipaumbele kwa mwaka 2017 ambapo itawasaidia wakulima katika upatikanaji wa miundombinu ya maji na pembejeo za kilimo.

Mtaka ameongeza kuwa kutokana na Benki ya NMB kuwa na fedha za kusaidia shughuli za kilimo kupitia Dirisha la Kilimo,  uongozi wa mkoa wa Simiyu unaomba Benki hiyo kuona namna itakavyosaidia mafanikio ya utekelezaji wa mradi wa kilimo cha umwagiliaji.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka amesema Serikali mkoani humo imekusudia kuwatoa wananchi katika fikra za kulima kwa ajili ya chakula pekee  na kuboresha kilimo kwa kulima kibiashara.

“Tunataka kutengeneza ‘model’ yetu katika kilimo cha umwagiliaji ili wananchi wetu walime kibiashara, wenzetu kwenye maeneo mengine wanafanya na wamefanikiwa na sisi tufanye, kwa kuwa tumedhamiria tutafanya” alisema Mtaka.  

Akizungumza na viongozi wa Mkoa wa Simiyu, Mkuu wa Idara ya Kilimo Biashara wa Benki ya NMB  Bw. Saif Ahmed benki iko tayari kuunga mkono juhudi za mkoa wa Simiyu katika kilimo cha umwagiliaji Busega Mkoani humo, ambapo amependekeza mradi huo ukatekelezwa kwa ushirika kati ya Benki hiyo,Serikali na wananchi.

Naye Meneja Mwandamizi Idara ya biashara za Serikali wa NMB Makao Makuu, Suzan Shuma Nguya, amesema Benki hiyo itaunga mkono juhudi za Serikali ya Mkoa wa Simiyu katika Utekelezaji wa mradi huo, wakiamini kuwa utakuwa mfano na kuwapa fursa kusaidia utekelezaji wa miradi kama hiyo katika Halmashauri nyingine hapa nchini.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Busega Mhe.Vumi Magoti amesema atashirikiana na viongozi wengine kuwahamasisha wananchi kuchimba mitaro itakayopelekea maji mashambani kama sehemu ya moja ya mchango wao katika utekelezaji wa mradi wa kilimo cha umwagiliaji.

Mkuu wa Mkoa na wajumbe wote wa kamati ya ulinzi na Usalama ya mkoa wameahidi kuwaunga mkono wananchi katika uchimbaji wa mitaro mara utekelezaji wa shughuli hiyo utakapoanza.


Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu,Ndg.Jumanne Sagini ameuomba uongozi wa NMB kuwaruhusu wataalam wao kushirikiana na wataalam wa Mkoa  huo katika ukamilishaji wa andiko na utekelezaji wa mradi huo ili kuwasaidia wananchi wa Busega na Simiyu kwa ujumla kuwa na usalama wa chakula na kujipatia fedha kwa kilimo biashara.
: Mkuu wa Idara cha Kilimo Biashara wa Benki wa NMB Bw. Saif Ahmed (kulia) akizungumza na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Simiyu ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Mhe.Anthony Mtaka na uongozi wa Benki hiyo katika kikao Maalum kilichofanyika Makao makuu ya Benki hiyo Jijini Dar es Salaam
 
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka (kulia) akizungumza jambo katika kilichofanyika ukumbi wa Mkutano wa Benki ya NMB  makao makuu jijini Dar es Salaam kati ya viongozi wa Benki  hiyo na Viongozi wa Mkoa wa Simiyu.
Baadhi ya Viongozi wa Mkoa wa Simiyu Simiyu wakimsikiliza Mkuu wa Idara cha Kilimo Biashara wa NMB Bw. Saif Ahmed katika kikao kilichofanyika ukumbi wa Mkutano wa Benki hiyo makao makuu jijini Dar es Salaam kati ya viongozi wa Benki  hiyo na Viongozi wa Mkoa wa Simiyu.

0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!