Jumla ya Wanafunzi 12,399 mkoani Simiyu
wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kwa mwaka 2019 katika shule za
Serikali za kutwa na bweni kwa awamu ya kwanza.
Hayo yamebainishwa na Katibu Tawala wa
Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini Desemba 14, 2019 wakati akitoa taarifa ya
uchaguzi wa wanafunzi wa Kidato cha kwanza kwa mwaka 2019 Mjini Bariadi.
Sagini amesema jumla ya wanafunzi
waliofaulu Mtihani wa Darasa la Saba ni 24,983 sawa na asilimia70.68 ya
wanafunzi wote waliofanya mtihani, ambapo amebainisha kuwa wanafunzi 12, 584
kati ya 24,983 waliofaulu hawajachaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza
kutokana na uhaba wa miundombinu ya elimu.
Sagini amesema lengo la Serikalini
kuhakikisha wanafunzi wote waliofaulu wanaenda sekondari hivyo, amewaagiza
Wakurugenzi wa Halmashauri zote mkoani Simiyu kuhakikisha kuwa wanafanya
jitihada katika ujenzi na ukamilishaji wa miundombinu, ili wanafunzi wote
waliofaulu mtihani wa darasa la saba waweze kuanza kidato cha kwanza kwa
wakati.
"Lengo la Serikali ni kuhakikisha
wanafunzi wote waliofaulu mtihani wa darasa la saba wanapata nafasi ya kujiunga
kidato cha kwanza ; nimetoa maelekezo kwa Wakurugenzi wa Halmashauri
kukamilisha miundombinu inayohitajika ili wanafunzi watakaochaguliwa awamu ya
pili waweze kuripoti shuleni kabla ya Februari 15, 2019"
"Nawasihi wazazi na walezi wa wanafunzi
watakaokosa nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza kwa awamu ya kwanza kuwa
wavumilivu wakati Halmashauri zinajiandaa kuwapokea wanafunzi hao"
alisema Sagini.
Afisa Elimu Mkoa wa Simiyu, Mwl. Ernest
Hinju amesema ufaulu umeongezeka kutoka asilimia 67.73 mwaka 2017 hadi kufikia
asilimia 70.68, ambapo wavulana wameonekana kufanya vizuri zaidi kwa ufualu wa
asilimia 74.61 na wasichana asilimia 67.57.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa
Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Mhe. Bahame Kaliwa amesema mahitaji ya miundombinu
yameongezeka kutokana na ufaulu kuongezeka kila mwaka, hivyo jitihada
zitafanyika ili kuhakikisha miundombinu inayohitajika inajengwa na wanafunzi
wenye sifa za kwenda kidato cha kwanza wanapata nafasi.
Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari Chenge, Mwl.Mhinga
Bulenzi amesema wamefanya mikutano kadhaa na wazazi na wakakubali kushirikiana
na Serikali katika ujenzi wa miundombinu ya elimu ili wanafunzi wote waliofaulu
mtihani wa darasa la saba na hawakuchaguliwa kwa awamu ya kwanza waanze kidato
cha kwanza ifikapo Februari 15, 2019.
Jumla ya wanafunzi 35,346 kati yao wasichana wakiwa 19,743 na wavulana
15,603 walifanya mtihani wa Taifa wa kuhitimu darasa la saba mwaka huu 2018
mkoani Simiyu.
MWISHO
Katibu Tawala wa Mkoa
wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini (wa pili kushoto) akitoa taarifa ya uchaguzi wa wanafunzi wa kidato
cha kwanza mwaka 2019, Desemba 14, 2018 Mjini Bariadi.
Afisa Elimu wa Mkoa wa
Simiyu, Mwl. Ernest Hinju akitoa taarifa ya hali ya ufaulu katika Mtihani wa
kuhitimu darasa la saba mwaka 2018, katika kikao cha uchaguzi wa wanafunzi wa
kidato cha kwanza mwaka 2019 kilichofanyika Desemba 14, 2018 Mjini Bariadi.
Makamu Mwenyekiti wa
Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Mhe. Bahame Kaliwa (kushoto) na Makamu
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Mhe. Paul Maige wakifuatilia kwa makini nyaraka zenye taarifa ya uchaguzi wa wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2019, katika
kikao kilichofanyika Desemba 14, 2018 Mjini Bariadi.
Baadhi ya wajumbe wa
Kikao cha uchaguzi wa wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2019, wakimsikiliza
Mwenyekiti wa Kikao hicho na Katbu Tawala Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini
akifungua kikao hicho Desemba 14, 2018 Mjini
Bariadi.
Baadhi ya waandishi wa
habari na wajumbe wa Kikao cha uchaguzi wa wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka
2019, wakimsikiliza Mwenyekiti wa Kikao hicho na Katbu Tawala Mkoa wa Simiyu,
Bw. Jumanne Sagini akifungua kikao hicho Desemba 14, 2018 Mjini Bariadi.
0 comments:
Post a Comment