Vyama vya Siasa, wagombea na wananchi wamekumbushwa kuendelea kufuata sheria za nchi katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu kwani sheria hazijasimama hivyo wajihadhari na vitendo vinavyoweza kusababisha vurugu kwa kisingizio cha uchaguzi.
Hayo yamebainishwa jana na Mkurugenzi msaidizi wa huduma za sheria kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini (NEC),Bw. Baraka Leonard wakati akisoma hotuba ya Mwenyekiti wa tume hiyo kwenye ufunguzi wa mkutano wa wadau wa uchaguzi uliofanyika katika ukumbi wa uliopo kwenye jengo la ofisi ya mkuu wa mkoa wa Simiyu mjini Bariadi.
"niwahakikishie wananchi tume ya uchaguzi imejipanga kusimamia uchaguzi mkuu Oktoba ,2020 kwa kufuata katiba, sheria na miongozo iliyopo na tuna Imani kila mdau atatimiza wajibu wake katika hili " alisema na kuongeza kuwa:
"nivitake vyama vya saisa na wagombea kuzingatia maadili ya uchaguzi katika kampeni zao ikiwemo kuepuka lugha za kashfa na maneno ya uchochezi, kuepuka kufanya kampeni zinazoashiria ubaguzi katika misingi ya jinsi, ulemavu, ukabila, udini, maumbile na rangi" aliongeza.
Mbali na hayo aliwatoa hofu wapiga kura wote wenye mahitaji maalumu kwani tayari maelekezo yametolewa kwa watendaji wa uchaguzi kwa kutoa kipaumbele kwa wenye ulemavu, wajawazito, akina mama wanaonyonyesha ,waliokwenda na watoto vituoni, wazee na wagonjwa huku akiongeza kuwa kila mwenye sifa ya kupiga kura ajitokeze na kadi yake kupiga kura katika kituo alichojiandikisha ili kutimiza haki yake ya msingi ya kikatiba.
Kwa upande wake afisa elimu ya mpiga kura kutoka NEC Nuru Riwa alisema tume hiyo itaandaa jalada la nuka nundu (tactile ballot folder) kwa kila kituo cha kupigia kura kwa ajili ya wasiiona ,wenye huku wenye ulemavu wa miguu kituturi kimetengenezwa lengo likiwa kuwapa nafasi na wenye ulemavu kupiga kura.
Riwa aliongeza kuwa upigaji kura utafanyika katika vituo 80,155 na jumla ya watendaji wa vituo 320,620 watasimamia na kuendesha zoezi la upigaji kura vituoni hapo.
Awali mjumbe kutoka shirikisho la vyama vya watu wenye ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) mkoa wa Simiyu Alex Benson aliiomba tume kuweka mazingira rafiki kwa viziwi ili kundi hilo liweze kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi huo huku akitolea mfano wawepo wataalam wa lugha ya alama kwenye vituo na kundi hilo liitwe kwa umoja wao kupewa elimu kwani elimu inayotolewa kwanjia nyingine ikiwemo matangazo yanayotumia vipaza sauti hayawafikii.
Akichangia kwenye mkutano wa wadau hao Semeni Kingi ambaye ni mwakilishi wa kundi la wenye ualbino aliiomba tume ya taifa ya uchaguzi kuhakikisha majina ya wagombea wa nafasi za Urais, ubunge na udiwani yanaandikwa kwa herufi kubwa kwenye karatasi za kupigia kura ili kuwarahisishia wenye uoni hafifu kusoma kiurahisi.
MWISHO.
0 comments:
Post a Comment