Wanafunzi wa Kidato cha nne mkoani Simiyu wanatarajia kuanza kambi za kitaaluma tarehe 30 Oktoba 2020, kwa ajili ya kujiandaa na mtihani wa Taifa unaotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 23 Novemba 2020 hadi tarehe 11 Desemba, 2020.
Taarifa hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka wakati akizungumza na Maafisa Elimu, wakuu wa shule na baadhi ya wanafunzi wa kidato cha nne baada ya kufunga kikao maalum cha kutangaza na kutathmini matokeo ya Mtihani wa Utimilifu (Mock) kilichofanyika jana Mjini Bariadi.
Mtaka amesema wanafunzi wote wa kidato cha nne waliopata daraja la I (division one) daraja la IV (division four), daraja la sifuri (division zero) katika Mtihani wa Mock mwaka 2020 na wale wanaotoka katika shule zenye watahiniwa pungufu ya 30 Serikali imeandaa utaratibu kwa ajili yao, hivyo tarehe 30 Oktoba wanapaswa kufika katika vituo vilivyoandaliwa ambavyo ni Shule ya Sekondari Simiyu na Shule ya Msingi Ndekeja.
“Mwaka huu kumekuwa na majanga mengi ya moto, majanga ya moto dawa yake si kufunga kambi za shule na ndiyo maana shule za bweni hazijafungwa, tumekuwa na utaratibu wa kambi za kitaaluma kwa watoto wote wa kidato cha nne wa Mkoa wa Simiyu wa shule za Serikali; maelekezo yangu, kambi za kitaaluma kwenye maandalizi ya kidato cha nne zianze na ziendelee mpaka tutakapoanza mtihani wa Taifa,” alisema Mtaka.
Mtaka amezitaka Kamati za Ulinzi na Usalama za
wilaya zote mkoani Simiyu kuendelea kuchukua tahadhari na kinga zote za majanga
ya moto, huku akibainisha kuwa elimu ya tahadhari ya majanga ya moto imeshatolewa
katika shule zote na vifaa vya kuzimia moto vimefungwa katika baadhi ya shule ikiwemo shule ya
Sekondari Simiyu ambacho ni kituo cha kambi hizo.
Akizungumzia
suala la motisha kwa walimu na wanafunzi watakaofanya vizuri katika mtihani wa Taifa
wa Kidato cha nne amesema mwalimu atapewa shilingi 30,000/= kwa kila alama A
itakayopatikana kwenye somo lake na shilingi 10,000/= kwa alama B.
Ameongeza
kuwa mwanafunzi atakayepata daraja la kwanza pointi saba atapewa shilingi 1,000,000/=
na ikiwa atakuwa miongoni mwa wanafunzi kumi bora Kitaifa ataongezewa shilingi
1,000,000/=na kumfanya apate shilingi 2,000,000/=, ambapo amesisitiza kuwa
mwanafunzi wa kike atakayefanya vizuri kuliko wenzake wote atapewa shilingi
500,000/= na ikitokea msichana aliyeongoza amepata daraja la kwanza pointi saba
atapewa shilingi 1,500,000/=
Shule
ya Serikali ya Sekondari ya Mkoa wa Simiyu itakayoingia katika shule 10 bora Kitaifa
itapewa zawadi ya shilingi 5,000,000/= huku akiahidi kuwapeleka walimu wote ambao
Halmashauri yao itafanya vizuri na kuingia katika nafasi kumi bora Kitaifa kwenda
kufanya utalii wa ndani katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Kwa
upande wake Afisa Elimu wa Mkoa wa Simiyu Mw. Ernest Hinju amesema katika matokeo
ya mtihani wa Taifa wa kidato cha nne mwaka 2019 Simiyu ilishika nafasi ya tano
Kitaifa na matarajio ya mwaka huu ni kushika nafasi ya kwanza Kitaifa, huku
akibainisha kuwa maandalizi yanaendelea vizuri na wazazi wamehamasika
kuwachangia wanafunzi chakula.
Kwa
upande wao walimu na wanafunzi wameshukuru Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony
Mtaka kuruhusu kambi za kitaaluma kwa kuwa kambi hizo zimekuwa msaada sana kwa
wanafunzi hususani wale ambao wanatoka katika mazingira magumu ambayo hawawezi
kujisomea kwa uhuru.
“Awali
tuliposikia kambi zimeahirishwa tulisononeka sana maana kambi zimekuwa msaada
hasa kwa watoto wanaotoka katika mazingira magumu, hata walimu tunabadilishana
utaalamu na mbinu za ufundishaji; tunamshukuru Mhe.RC kuruhusu kambi maana miaka
ya nyuma Simiyu ilikuwa nyuma sana kwa ufaulu; lakini sasa hivi tumetoka huko tumepanda
mfano matokeo ya kidato cha sita mwaka huu tumeshika nafasi ya tatu na kidato
cha nne mwaka 2019 tulishika nafasi ya tano Kitaifa,” Mwl. Khamis Lubugwa.
“Kambi za kitaaluma zimekuwa na msaada sana hususani
kwa watoto wa kike, tunapokuwa kambi tunapata muda mwingi wa kujisomea kuliko
tunapokuwa nyumbani lakini vile vile tunapokuwa kambi inatusaidia kuepukana na
vishawishi mbalimbali maana miongoni mwetu wako wanaotoka mbali, tumejisikia
vizuri kufunguliwa kwa kambi na tunatarajia kufanya vizuri sana,” Nshoma Joseph
mwanafunzi wa kidato cha nne shule ya sekondari Bariadi.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment