Tuesday, December 14, 2021

RC Kafulila Aagiza Wazawa Malampaka Wapewe Kipaumbele














Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. David Kafulila akizungumza na Wananchi wa Malampaka- Maswa

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. David Kafulila ameagiza wazawa wa Malampaka wapewe kipaumbele kwenye ajira ya Ujenzi wa reli ya kisasa(SGR), Mwanza/ Isaka.

Maagizo hayo yametolewa, mara baada ya mamia ya wananchi wa  mji wa Malampaka wilaya ya Maswa, kumlilia mkuu wa mkoa awasaidie kupata ajira kwenye kituo cha ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Mwanza kwenda Isaka kilichopo kwenye mji huo, inayojengwa na kampuni ya CCECC ya nchini China.

Wananchi hao walitoa kilio chao katika mkutano wa hadhara uliondaliwa na Mkuu wa mkoa kwa ajili ya kusikiliza malalamiko yao kuhusu kubaguliwa kwao katika masuala ya ajira pamoja na kuwepo kwa vitendo vya rushwa kwenye mradi huo unaofanyika mjini Malampaka.

Wananchi  hao walimweleza Mkuu wa Mkoa kuwa wakati mradi huo unatambulishwa kwa mara ya kwanza kwao na viongozi wa serikali walielezwa kuwa wakazi wa eneo hilo ambapo panajengwa bandari ya nchi kavu watapatiwa kipaumbele kwenye masuala ya ajira.

Walisema kuwa kwa sasa shughuli zimekwisha anza lakini waliopatiwa ajira ni watu wachache tu ambao hawazidi 15 kulinganishwa na idadi watu 300 walioko kwenye kambi hiyo. Ambapo wengi wao wametoka nje ya mkoa wa Simiyu.

'Mwanzoni tulielezwa kuwa mradi utakapoanza kipaumbele kitatolewa kwa wananchi ambao wanaishi katika eneo ambalo mradi unatekelezwa lakini cha kushangaza mambo yamekwenda kinyume kabisa wengi wa waajiriwa wanatoka nje kabisa ya mkoa wa Simiyu,"

"Sisi tumekuwa tukibaguliwa katika masuala ya ajira na jambo baya zaidi katika kupata ajira hizo vitendo vya rushwa vimeshamiri sana,"alisema Juma. 

Kutokana na malalamiko hayo Mkuu wa Mkoa ameagiza vyombo vya dola kufutailia suala la rushwa kama lipo na kutaka wahusika watakaobainika kuchukuliwa hatua za kusheria.

Aidha ametaka kupelekewa majina ya watu walioajiriwa kama wanatoka mkoa wa Simiyu au la kwani Serikali imekuwa ikitaka wanufaika wa kwanza wawe wanaoishi kwenye eneo la mradi.

MWISHO.



0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!