Thursday, January 27, 2022

“Eleweni Changamoto za Wananchi katika Maeneo yenu, na Muwe Watatuzi”- RC KAFULILAMkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. David Kafulila ameyasema hayo wakati wa kikao kazi cha Watendaji wa Kata, Vijiji na Mitaa  wa Halmashauri ya Bariadi Mji na Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi kilichofanyika hivi karibuni.

Mhe.Kafulila ambaye alikuwa mgeni rasmi wakati wa kikao kazi hicho alisisitiza umuhimu wa Watendaji kupewa mafunzo ya mara kwa mara nje ya eneo la kazi pamoja na mafunzo kazini.

 “Kila Mtendaji kata,kijiji na mtaa lazima ajue Sheria ambayo imemfanya awepo kazini. Unapaswa kujua 'ABC' za uendeshaji ofisi. Lazima vikao vyote vya kisheria vifanyike, kuwe na ajenda za vikao na kumbukumbu za vikao hivyo.Lazima muwe na mpango kazi,hizo ndio zana za kazi.Lazima upange kazi zako na uje wiki ijayo utashughulikia nini? Mkiwa viongozi mnapaswa kuelewa changamoto zinazowakabili wananchi wa kwenye maeneo yenu,na kuwa watatuzi wa changamoto hizo.".Ameeleza Kafulila. 

Akielezea agenda nne za Mkoa wa Simiyu na Wilaya zake.Mhe. Kafulila amezitaja ajenda hizo kuwa ni makusanyo, kilimo, ukame/chakula na upandaji miti. 

Akizungumzia agenda namba moja ambayo ni Makusanyo, Mhe. Kafulila amewataka Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi kushindanisha Vijiji kwa asilimia za makusanyo na mashindano hayo yafanyike kila robo mwaka na hatimae kuzitambua halmashauri zilizofanya vizuri aidha kwa kuwapa vyeti au barua ya Pongezi. Hili lifanyike katika Halmashauri zote. Kila Halmashauri iwe na lengo la makusanyo. 

Kuhusu kilimo,Mhe. Kafulila amewataka wakuu hao kujipanga na killimo  cha alizeti. "Matumaini yetu ni kuzalisha alizeti tani 200,000-250,000 ikilinganishwa na tani 81,000 ambazo zilizalishwa Mwaka Jana. Suala la kilimo cha  Pamba na Alizeti linatakiwa kuwa agenda ya eneo lako.Kila kitongoji ni vyema kuwa na majina ya wakulima na kujua  wamelima nini kama ni alizeti au pamba".Amesisitiza Kafulila.

Aidha ili kukabiliana na changamoto ya chakula kutokana na ukame ambao umesababisha bei za chakula kuwa juu,Mhe. Kafulila amewaelekeza Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi kuwahamasisha na kuwaelimisha wananchi wao juu ya umuhimu wa kilimo cha mazao ya chakula ambayo hayahitaji mvua nyingi. "Nimeshaongea Mamlaka ya kilimo Morogoro, baaada ya kutoa Pamba shambani itabiidi wakulima walime dengu.Mamlaka ya kilimo itatoa mbegu, zana na pembejeo za kuwawezesha ili waweze kishiriki kilimo bora.

Akizungumzia ajenda ya tatu, Mhe.Kafulila ameitaja ajenda hiyo kuwa upandaji wa miti. Simiyu ni miongoni mwa  mikoa 5 Tanzania Bara inayoongoza kwa ukataji wa miti, hivyo ili kuepukana na janga la jangwa ni vyema kila kijiji  kiwe na agenda ya upandaji wa miti. Akitaja ajenda namba nne, Mhe.Kafulila ameitaja ajenda hiyo kuwa ni  Elimu," fuatilieni na kusimamia kikamilifu agenda ya Elimu. Wiki ijayo tutakutana kuzungumzia kwa kina kuhusu matokeo.Watendaji wa kata na vijijini wekeni macho yenu kwenye suala la Elimu."Amesisitiza Kafulila.

Mhe. Kafulila amewapongeza watendaji wa kata, vijiji, mitaa, mkuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri hizo mbili kwa uchapakazi. Aidha amewahakikishia wakuu hao imani kubwa aliyonayo kwao ya kwamba wana uwezo mkubwa wa kufanya mambo mengi makubwa zaidi wakiamua."Mnachohitaji ni kuwatambua watu wa chini kwa kazi nzuri wanazofanya.Wapeni hata barua au cheti cha kuwapongeza. Maeneo yote wanayofanikiwa wapeni moyo na wanapokosea wachukulieni hatua kali.Wanaofanya vizuri wapeni hamasa kubwa.Uwezo wa kubadilisha vijiji, Wilaya, upo mkononi mwetu.”

Akizungumzia kusudi la kikao kazi hicho, Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Mhe. Lupakisyo Kapange ameeleza nia ya kikao kazi hicho ni  kujengeana uwezo na kuzindua kauli mbiu ya Halmshauri ya Bariadi Mji na  Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi isemayo: "Serikali mlangoni Mwako". Mwisho.

0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!