Tuesday, January 25, 2022

WAKURUGENZI, WAKUU WA WILAYA ELIMISHENI WANANCHI KUHUSU FURSA MBALIMBALI ZA MIKOPO - RC KAFULILA.





Picha ya Pamoja kuanzia kushoto Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bariadi Mji, Meneja wa NMB Bariadi,Mkuu wa wilaya ya Bariadi na Mkurugenzi wa Halmshauri ya Bariadi Mji wakiwa wameshika hundi ya mfano kutoka benki ya NMB

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bariadi Mji Bw. David Masanja ( Kushoto) akimkabidhi hundi ya Mfano Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe David Kafulia (Kulia), ikiwa na kiasi cha fedha kitakachokopeshwa kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu- Halmashauri ya Bariadi Mji

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. David Kafulila (kulia)  akikabiidhi hundi ya Mfano kwa wawakilishi wa makundi  ya wanawake, Vijana na watu wenye ulemavu. 
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. David Kafulila (Kulia) akiteta jambo pamoja na mkuu wa Wilaya ya Bariadi Mhe.Lupakisyo Kapange wakati wa tafrija hiyo.


Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. David Kafulila akizungumza na washiriki wa tafrija hiyo leo katika ukumbi wa Bariadi  Conference -Bariadi Simiyu






Makundi mbalimbali ya washiriki kwenye hafla hiyo.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. David Kafulila,ameyasema hayo leo, wakati wa hafla ya utoaji mikopo kwa vikundi vya wajasiriamali vilivyopo katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi. Akizungumza, Mhe.Kafulila ameeleza lengo la Serikali katika utoaji wa mikopo ya aina hiyo ni kuwawezesha wananchi  wasiokidhi vigezo vya kukopeshwa na benki, kujikwamua kiuchumi kwa kuwapa fursa mbalimbali yakiwemo makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, kwa kuwapatia mikopo ya fedha za asilimia 10 ya mapato ya ndani yaliyokusanywa na halmashauri za miji. 

 Fedha hizo hutokana na tozo na ushuru mbalimbali ambao hukusanywa na kuwekwa pamoja hatimaye 10% yake kutolewa kama mikopo kwa makundi maalum. "Fedha hizo ni mikopo na sio msaada, hivyo mnawajibika kuzirejesha kwa wakati ili ziweze kukopeshwa kwa vikundi vingine, vitakavyokidhi vigezo. Nawaasa mjitahidi kuhakikisha mnatekekeleza miradi mliyoianzisha kwa ufanisi na kurejesha fedha mlizokopeshwa kama sheria, kanuni, taratibu na miongozo inavyowataka". Amesema Kafulila. 

Mhe.Kafulila leo, amepokea hundi ya mfano kutoka benki ya NMB, hundi ambayo amekabidhiwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bariadi Mji, Bw. Adrian Jungu wakiwa pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Mhe. Lupakisyo Kapange pamoja na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bariadi Mji Bw.David Masanja, hundi  yenye thamani ya Tsh. 256,090,000/-, fedha ambazo zitakopeshwa kwa jumla ya vikundi 53 vyenye wanufaika 364 ikiwa ni  awamu ya kwanza katika mwaka wa fedha 2021/2022. 

Fedha hizo zitagawanywa kwa makundi maalum yenye mchanganuo ufuatao, wanawake vikunndi 37 watakopeshwa kiasi cha Tsh.180,100,000/-, vijana vikundi 11 vitakopeshwa Tsh. 49,420,000/- na watu wenye ulemavu vikundi 5 watakopeshwa Tsh. 26,570,000/-.

Akizungumzia changamoto wanazokabiliana nazo katika utoaji wa mikopo ya 10%,Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bariadi Mji. Bw. Adrian Jungu, amezitaja changamoto hizo kuwa, mapato ya ndani kuwa madogo ikilinganishwa na mahitaji ya makundi maalum ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ambao wanaotakiwa kukopeshwa, baadhi ya vikundi kukosa uaminifu katika kurejesha mikopo, baadhi ya vikundi kubadilisha matumizi ya fedha walizokopeshwa kulingana na miradi waliyoombea mikopo, badala yake kugawana fedha au kuanzisha miradi mipya ambayo hawana uzoefu nayo na hivyo kushindwa kurejesha mikopo hiyo.

 Aidha Bw. Jungu ameeleza mikakati mbalimbali ambayo Halmashauri ya Bariadi Mji imejipanga kufanya ili kukabiliana na changamoto hizo ikiwa ni pamoja na kuendelea kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kuongeza mapato ya ndani, kuboresha mbinu za ukusanyaji mapato kwenye vyanzo vilivyopo,kuendelea kutoa elimu kwa vikundi ili viiweze kuzingatia taratibu na miongozo iliyowekwa na kufuatilia marejesho ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani wadaiwa sugu. Hadi sasa, mashauri 6 ya madai yamefunguliwa mahakamani na tayari vikundi 2 kati ya 6 vilivyoshtakiwa vimelipa na kumaliza deni walikokuwa wanadaiwa.Halmashuri ya Bariadi Mji inadai kiasi cha Tsh. 35,057,450/- kutoka kwenye vikundi 15. 

 Ili kuhakikisha ufanisi katika utoaji wa mikopo hiyo Mhe Kafulila amewaagiza wakurugenzi wote wa halmashauri na wakuu wote wa wilaya za Mkoa wa Simiyu kuwahamasisha na kuwaelimisha wananchi ili waelewe na waitumie fursa hiyo kwani kuna watu wengi ambao hawajui kuhusu fursa hizo. Kuna benki ambazo zinatoa mikopo kwa riba ndogo hivyo ni vyema kwa vikundi ambavyo vimekidhi vigezo vikatumia fursa hiyo na kukopa  kutoka kwenye benki hizo.

Mhe. Kafulila amewataka wakuu hao wote kutumia zoezi la upandaji miti kama kigezo kimojawapo cha kupata mkopo. Wanakikundi wanatakiwa wapande miti ama ya kivuli ama ya Matunda na kuonyesha eneo walilopanda miti hiyo kisha ndio wapewe mkopo, hii itaharakisha na kurahisiha sana Simiyu ya Kijani. 

 Aidha Mhe Kafulila amewataka viongozi hao kujua watu wao wanajishughulisha na nini. "Jengeni dhana pana ya uelewa juu ya shughuli mbalimbali wanazofanya wananchi wa eneo lenu.Maafisa biashara wote ni jukumu lenu kuvijua vikundi vyote vinavyohusika na Mikopo.Maafisa biashara wote ni lazima muwe walezi wa vikundi hivi".Amesisitiza Kafulila. Mwisho.

0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!