Monday, January 3, 2022

TARURA,Hakikisheni Mnawapa Kazi Wakandarasi Wenye Uwezo- RC KAFULILA

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.David Kafulila ameyasema hayo leo hii, wakati wa tafrija fupi ya  kusaini mikataba ya shughuli za matengenezo ya Barabara kwa fedha za tozo za mafuta, iliyoandaliwa na TARURA Mkoa wa Simiyu. 

Mhe. Kafulila, ameeleza hayo wakati akishuhudia usainishaji wa mikataba ya miradi 19 ya matengenezo ya barabara yenye thamani ya Tsh.7.5 bilioni. Kati ya miradi hiyo 19, miradi 18 itatekelezwa kwa fedha za tozo za mafuta, ambazo thamani yake ni Tsh.7.1bn sawa na asilimia 95. Mhe. Kafulila amebainisha, kulingana na taarifa za wataalam wa masuala ya tozo, wataalam hao husema kuwa, ukitoza lazima uonyeshe manufaa ya hizo tozo kwa wananchi, na  leo tunajionea uhalisia kwani 95% ya fedha zinatokana na tozo zitatumika katika shughuli za matengenezo ya Barabara Mkoani Simiyu.“Hivyo ni vyema kila mkandarasi kutekeleza mkataba kwa jinsi mlivyosaini, kwani  uzoefu wa mikataba midogomidogo na baadhi ya wakandarasi ambao hawana vifaa kufanya kazi chini ya kiwango.Nielekeze Mamlaka za barabara TARURA mhakikishe mnawapa kazi wakandarasi wenye uwezo. Maana chini ya hapo sio kwamba tutavunja mkataba na huyo mkadarasi bali pia na wewe kama kiongozi, utawekwa kwenye kiulizo  yaani (black listed)” Amesema Kafulila.

Mkuu wa Mkoa amewataka Wakandarasi kuondokana na mazoea na kazi na badala yake kufanya kazi kwa wakati na weledi na kutolea mfano makandarasi wa Matongo ambaye kazi yake ipo chini ya kiwango na hivyo kumtaka Kaimu  Meneja wa TARURA, atoe maelezo ndani ya  siku 3 kwanini mkandarasi huyo asifutiwe mkataba.”Sitosita kufuta mikataba yote kama mnaleta ujanja ujanja. Wakandarasi wote mnatakiwa muwe na ratiba ya utekelezaji wa kazi zenu, nikipita nipate maelezo ya kina mmefikia wapi na kwa nini.Tekelezeni mikataba yenu kwa ufanisi na viwango”Amesisitiza Mhe. Kafulila.


Wakati huo huo Mhe.Kafulila amewataka Wakuu wote wa Wilaya za Mkoa wa Simiyu kuhakikisha wanafuatilia utekelezaji wa mikataba yote inayofanywa kwenye Wilaya zao , kwani hizo ni fedha za Serikali. “Mradi wowote wa Serikali unaotekelezwa kwenye Wilaya yako ni wajibu wako kujua mkandarasi ni nani, mradi unagharimu kiasi gani, utachukua muda kiasi gani, na ratiba ya utekelezaji. Hii itasaidia kujua kazi gani inafanyika lini na baada ya muda gani itakuwa imefikia wapi.

Nae Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Mhe. Lupakisyo Kapange amewataka Wakandarsi hao kutilia maanani maelekezo ya Mkuu wa Mkoa na kuendana na kasi yake.

Akizungumza Kaimu Meneja TARURA- Simiyu Eng. Mathias Mgolozi , ameeleza kuwa bajeti iliyoidhinishwa kwa mwaka wa fedha 2021/2022 kwa Mkoa wa Simiyu ni Tsh.18.38 bn kati ya hizo kiasi cha Tsh 5.698 bn ni fedha kwa ajili ya za matengenezo ya barabara,Tsh.4.2 bn  kutoka mfuko wa jimbo, na Tsh.8.2 bln fedha ya tozo. “kwa siku ya leo jumla ya Mikataba 19 itasainiwa. Utekelezaji wa mikataba 18 yenye thamani ya Tsh.7.1 bn itatekelezwa kutokana na  fedha ya tozo, wakati mkataba mmoja wa mradi wa daraja la Ngashanda wenye thamani ya Tsh.429,975,500/- utatekelezwa kutokana na  fedha maalum za mradi huo. Miradi yote 19 itawanufaisha wananchi wa majimbo 8 ya mkoa wa Simiyu. Mkoa wa Simiyu una Mtandao wa barabara wenye kilometa za Mraba zipatazo 4163.83.Kati ya hizo KM 1355.26 ambazo ni sawa na 33% ndizo zinazohitaji matengenezo. Matengenezo  ya KM 923.96  yanategemea fedha za ukarabati wa barabara, KM 280.6 fedha za tozo na KM 150.7 mfuko wa jimbo. Utekelezaji wa mikataba hii utaanza 17/1/2022 na kukamilika 31 Julai ,2022.

Aidha,mwakilishi wa Wakandarasi hao Eng. Lameck Okesh kutoka kampuni ya Nice Construction Limited , amesema kuwa wapo tayari kutekeleza majukumu yao kama walivyokubaliana na kuiomba Serikali kuwalipa kwa wakati. Mwisho.



Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.David Kafulila (mwenye Mkasi), akikata utepe ikiwa ni ishara ya kuzindua usainishaji wa Mikataba ya matengenezo ya Barabara kwa fedha za Tozo za Mafuta.Hafla iliyoandaliwa na ofisi za TARURA Mkoa wa Simiyu.Akishuhudiwa na wa kwanza kulia Kaimu Meneja TARURA- Simiyu Eng. Mgolozi, Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Mhe. Kapange,katibu Tawala mkoa wa Simiyu Bi. Prisca Kayombo,  na mkandarasi kutoka Mwanza 

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.David Kafulila, akikata utepe ikiwa ni ishara ya kuzindua usainishaji wa Mikataba ya matengenezo ya Barabara kwa fedha za Tozo za Mafuta.Hafla iliyoandaliwa na ofisi za TARURA Mkoa wa Simiyu. 


Wa kwanza kulia aliyeketi Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. David Kafulila akishuhudia usainishaji wa mkataba kati ya Mwanasheria wa TARURA- Simiyu na Mkandarasi , waliosimama nyuma na kushuhudia zoezi hilo ni mainjinia toka TARURA- SIMIYU

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. David Kafulila akimkabidhi mmoja wa Wakandarasi mkataba uliokwisha sainiwa tayari kuanza kazi 17/1/2022-31/07/2022

Meza Kuu


Wakandarasi kutoka kampuni mbalimbali

Watumishi wa TARURA-Simiyu




0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!