Katibu
Mkuu wa Chama cha Mpinduzi (CCM) Taifa Dkt. Bashiru Ally amewaonya baadhi ya Wakuu
wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa
Halmashauri, na Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Umma, ambao wameanza kukaa
vikao kwa ajili ya kutafuta majimbo kabla ya wakati wa Chama hicho kutangaza
mchakato wa kutafuta wagombea wapya wa ubunge na udiwani.
Dkt.
Bashiru ameyasema hayo Januari 05, 2019 wakati akizungumza na viongozi na
wanachama wa CCM pamoja na Viongozi na watendaji wa Serikali katika wilaya ya
Bariadi na Itilima wakati akiwa katika ziara yake mkoani Simiyu.
Dk Bashiru amesema ikiwa
viongozi hao wataendelea kufanya hivyo atawataja hadharani na akasisitiza kuwa
ni vema wakaridhika na nafasi walizopewa na Rais wa Tanzania, Mhe. Dkt. John
Pombe Magufuli kwani kushindwa kufanya hivyo ni kumdharau aliyewateua.
“Wapo wakuu wa mikoa, wakuu wa
wilaya, Makatibu tawala wa mikoa, wakurugenzi wa halmashauri, na wakuu wa taasisi
na mashirika ya umma, wameanza kukaa vikao kwa ajili ya kutafuta majimbo, CCM
hatujatangaza mchakato wa kutafuta wabunge au madiwani wapya, uko wakati
nitawatangaza hadharani, mridhike na nafasi zenu mlizopewa na Mhe. Rais”
alisema
Katika hatua nyingine Dkt. Bashiru amesema kuelekea
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwaka huu 2019 Viongozi wa CCM wajipange
katika kuhakikisha viongozi wa Vijiji na Mitaa wanachaguliwa katika misingi ya
demokrasia kwa kuzingatia sifa zao na si fedha zao(rushwa).
“ Katika mwaka huu wa kumuenzi Mwalimu Nyerere baada ya
miaka 20 tunataka kufanya mchakato wa kusimamia uchaguzi uwe tofauti, wakati wa
kuteua tuzingatie sifa na tuwapime viongozi kwa maisha yao na vitendo vyao......”
alisema Dkt. Bashiru.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya
ya Itilima, Mhe. Benson Kilangi ameishukuru Serikali ya awamu ya tano kwa kutoa zaidi ya shilingi bilioni 26 katika
kipindi cha miaka mitatu, kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Naye Mbunge wa Jimbo la Itilima Mhe.Njalu
Silanga, ameishukuru Serikali kwa kuboresha miundombinu ya barabara ambapo
amebainisha kuwa kupitia Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA)
barabara katika jimbo hilo zimetengenezwa zinapitika na zipo ambazo zinaendelea
kufanyiwa matengenezo.
Naye Katibu wa CCM
Mkoa, Bw. Donald Magesa akitoa taarifa
ya Chama, utekelezaji wa Ilani ya CCM mkoani humo umefanyika vizuri huku
akisisitiza kuwa Viongozi wa Chama na Serikali wamejipanga kwa kushirikiana na
wananchi kukamilisha maboma yaliyojengwa ili kila mwanafunzi aliyefaulu darasa
la saba mwaka 2018 aweze kuanza kidato cha kwanza.
Katibu Mkuu wa CCM
Taifa, Dkt. Bashiru Ally yuko Mkoani Simiyu kuanzia Januari 05,2019 kwa ziara
ya kikazi ya siku mbili yenye lengo la kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM
mkoani humo.
MWISHO.
Katibu Mkuu wa CCM
Taifa, Dkt. Bashiru Ally(kulia) akiteta jambo na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa
Simiyu, Mhe. Enock Yakobo wakati akiwa katika ziara yake ya kukagua utekelezaji
wa Ilani ya CCM mkoani hapa Januari 05, 2019.
Katibu Mkuu wa CCM
Taifa, Dkt. Bashiru Ally(wa tano kulia) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi
ya watumishi na viongozi wa Serikali wa Mkoa wa Simiyu mara baada ya k kikao
chake na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi na Serikali mkoani Simiyu kilichofanyika Mjini Bariadi
Januari 05, 2019.
Kutoka kushoto Mbunge
wa Maswa Mashariki, mhe. Stanslaus Nyongo, Mbunge wa Itilima, Mhe. Njalu
Silanga, Mbunge wa Meatu, Mhe. Salum Khamis na Mbunge wa Maswa Magharibi, Mhe.
Mashimba Ndaki wakifuatilia kikao cha Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Dkt. Bashiru
Ally na viongozi na watendaji wa Chama Cha Mapinduzi na Serikali mkoani Simiyu kilichofanyika Mjini Bariadi
Januari 05,2019 wakati wa ziara yake mkoani hapa.
Baadhi ya viongozi wa
CCM wa Mkoa wa Simiyu wakicheza nyimbo za Chama wakati wakijiandaa kumpokea
Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Dkt. Bashiru Ally(hayupo pichani) katika Mji mdogo wa
Lamadi wilayani Busega, kwa ajili ya kuanza ziara ya siku mbili mkoani hapa
Januari 05 na Januari 06 , 2019.
0 comments:
Post a Comment