Waziri wa Afya
Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Ummy Mwalimu ameagiza Wakala wa
Majengo nchini TBA kurejesha fedha ilizokabidhiwa na wizara yake kwenye ofisi
za TBA mjini Bariadi ili zitumike kukamilisha mradi wa ujenzi wa hospitali ya
rufaa ya mkoa wa Simiyu ambao kasi ya ujenzi wake kwa sasa hairidhishi.
Waziri Ummy ametoa kauli
hiyo katika ziara yake ya siku moja mjini Bariadi, mkoani Simiyu kukagua ujenzi
wa jengo litakalotumika kutoa huduma za maabara, upasuaji na mionzi na kusema
kuwa serikali imejiwekea malengo ifikapo Julai
Mosi wananchi waanze kupata huduma kwani tayari fedha zote za mradi huo
zimekwishalipwa.
“Wizara tayari imeshalipa zaidi ya shilingi
bilioni moja kwa TBA lakini cha ajabu wao wameleta shilingi milioni 430 tu, na
matokeo yake ndio haya, ukiangalia muda tuliopewa kukamilisha kazi hii si
rafiki, sasa ninawaagiza TBA walete hiyo pesa site ili kazi iendelee”.
“ Hivi jamani kwa kasi
hii kweli tunaweza kuendelea kuweka matumaini kwa hawa ndugu zetu, ukiangalia mheshimiwa
Rais ametupatia shilingi bilioni 2.5 tujenge jengo la mama na mtoto sasa kwa
utaratibu huu wa kusuasua mnadhani tutafika kweli, mimi nadhani umefika wakati
tutumie force account kwenye mradi huu, Bariadi kuna mafundi wengi wazawa wenye
uwezo mkubwa wa kutufanyia kazi hii”, alisisitiza Waziri Ummy.
Kuhusu mpango wa
serikali wa kuboresha huduma za rufaa katika hospitali zote za mkoa nchini,
Waziri Ummy amesema wizara imedaa utaratibu ambapo kila hospitali itapata
madaktari bingwa 16 katika fani 8 yaani madaktari 2 kila fani wakiwemo
madaktari bingwa wa akina mama, watoto, Mishipa ya fahamu, mifupa, njia ya
mkojo, dawa za usingizi na mionzi.
“ Tunataka tuwe na
maabara kubwa za kisasa pamoja na jengo la mionzi kama tunalojenga hapa Simiyu
katika kila hospitali ya rufaa ya mkoa, tunamshukuru sana mheshimiwa rais kwa
kutupatia shilingi bilioni 3.5 kwa ajili ya ujenzi wa jengo uchunguzi, ninaomba
kila mmoja wenu kwa nafasi yake ahakikishe miradi yote inayotumia fedha za
serikali inatekelezwa kwa ufanisi”, aliongeza Waziri Ummy.
Akijibu maombi ya
viongozi wa chama na serikali wa mkoa wa Simiyu kuhusu tatizo la usafiri kwa
watumishi watakaopangiwa kufanya kazi katika hospitali ya rufaa ambayo kwa sasa
haina nyumba za watumishi, Waziri Ummy amewahakikishia kuwa Wizara itaangalia
uwezekano wa kuipatia hospitali hiyo basi maalumu la watumishi halikadhalika
itaweka bajeti ya ujenzi wa nyumba za watumishi katika mwaka wa fedha ujao.
Akiwa katika hospitali
ya wilaya ya Bariadi ya Somanda, Waziri Ummy alielezea kutoridhiswa na
utaratibu wa kutoa huduma katika wodi ya wazazi na kumwagiza mganga mkuu wa
mkoa kuzifanyia marekebisho kasoro zote zilizobainika ili huduma zinazotolewa
ziendane ni miongozo ya wizara.
Kwa upande wake mkuu wa
mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka amemhakikishia Waziri Ummy kuwa, mkoa utasimamia kikamilifu utakelezaji wa
mradi huo na kusisitiza kuwa pale ambapo pamebainika kuwa na dosari
atahakikisha zinarekebishwa ili kuongeza ufanisi katika mradi huo.
“Mhe Waziri mimi nina
amini kukamilika kwa hospitali hii ni mkombozi kwa maelfu ya wananchi wetu wa
mkoa wa Simiyu, sasa wajiandae kupata
huduma bora zikiwemo za bima ya afya ambazo zimeboreshwa kwa kiwango kikubwa,
kwa ujumla tunaamini zitawahamasisha watu wengi zaidi kujiunga na huduma hiyo”, alisisitiza RC Mtaka.
Waziri wa Afya
Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amekamilisha ziara yake
mkoani Simiyu na Kuelekea katika mikoa ya Geita na Shinyanga.
Waziri wa Afya
Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Ummy Mwalimu Akiongozana na Mkuu wa
Mkoa wa Simiyu Kukagua Ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu katika eneo
la Nyaumata Kilomita chache kutoka mjini Bariadi
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu
Anthony Mtaka Akimpa Maelezo Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na
Watoto Ummy Mwalimu akipewa maelezo kuhusu Ujenzi wa Jengo jipya litakalotumika
kutoa huduma za maabara, upasuaji na mionzi katika eneo
la Nyaumata Wilayani Bariadi.
Waziri wa Afya
Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Ummy Mwalimu na mwenyeji wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony
Mtaka wakielekea kukagua Jengo la hospitali ya rufaa ya Mkoa lililokamilika
katika eneo la Nyaumata Wilayani Bariadi.
0 comments:
Post a Comment