RC
Mtaka Awashauri Wachezaji na Viongozi wa Coastal Union kutumia Falsafa ya
Michezo ni Ajira na Biashara Kama Njia ya Kuleta Mapinduzi ya Soka Nchini
Mkuu wa Mkoa wa
Simiyu Anthony Mtaka amewashauri wachezaji wa timu ya Coastal Union ya Tanga kutambua
kuwa michezo ni biashara na pia ni ajira hivyo wanapaswa kujiwekea malengo ya
muda mrefu na mfupi ili waweze kunufaika na matunda ya jitihada zao.
RC Mtaka ametoa kauli
hiyo ofisini kwake mjini Bariadi alipotembelewa na kikosi cha timu hiyo na
viongozi wake kilichokuwa kikitokea mkoani Mara kwenye mechi ya ligi kuu
Tanzania Bara ambako ilipoteza mchezo huo kwa kufungwa magoli 3 -2 na biashara
United.
Katika salamu zake
kwa timu hiyo Mtaka amesema njia pekee ya mafanikio kwa timu hiyo na wachezaji
wake inaanzia kwenye nidhamu ya wachezaji ndani na nje ya uwanja na pia uwepo
wa viongozi makini wanaojitambua na wenye nia ya kuleta mapinduzi ya soka
nchini.
“ Binafsi sikubaliani
na zile kauli mbiu za michezo ni afya au
michezo ni burudani, naendelea kusisitiza michezo ni biashara halikadhalika
michezo ni ajira hivyo kipaji chako ndio mtaji wako”.
“Mkitambua hilo
mtafika mbali, tunayo mifano hai, hebu mtazameni mchezaji kama Mbwana Samatta,
huyu alijitambua mapema, akajiwekea malengo na ndio maana ameweza kufikia hapo
alipo,analipwa mshahara ambao watanzania wachache sana wanaupata”, aliongeza
Mtaka.
“Kumbukeni nidhamu
ndio muhimili mkubwa utakaowapeleka mbali,achaneni na ulimbukeni wa Usimba na
Uyanga, na pia msikubali kuingia katika vishawishi vya kutumia dawa za kulevya,
mkifanya hivyo kwa umri wenu huu nawahikikishia mtafika mbali kuliko
mnavyotegemea”, alisisitiza RC Mtaka.
Aidha Mtaka pia
aliwatolea mfano wachezaji wa zamani kama George Weah ambaye kwa sasa ni rais
wa Liberia na golikipa wa zamani wa TP Mazembe Robert Kidiaba Muteba ambaye
hivi karibuni amechaguliwa kuwa mbunge huko Congo DRC kuwa ni kielelezo cha nidhamu bora michezoni
akisema kuwa kama wangekuwa na sifa mbaya jamii isingeweza kukubali kuwapa
nyadhifa kubwa za kisiasa.
Kuhusu uongozi wa
vyama vya soka nchini, Mheshimiwa Mtaka amesema ipo haja ya kuvitazama kwa
makini zaidi kwani kwa sehemu kubwa ya viongozi wake wanaendesha mambo kijanja
kijanja hali inayodhoofisha jitihada za serikali za kuleta mapinduzi ya soka
nchini.
“ Mara nyingi huwa
najiuliza, hivi kuna haja gani ya kusajili mchezaji wa kigeni kwa mamilioni
wakati kiwango chake ni cha chini kuliko wachezaji wetu wa ndani, hawa viongozi
wana ajenda gani na soka letu mpaka kufikia maamuzi hayo”, alihoji Mtaka.
RC Mtaka ameongeza kuwa njia pekee
itakayosaidia kuleta mabadiliko ya soka nchini ni mabadiliko ya mitazamo ya
viongozi wake ambapo amesema wanapaswa kuweka uzalendo mbele na kuiona michezo
kama fursa inayoweza kutangaza utalii wetu kupitia wachezaji waliowahi kutamba
au wale wanaogonga vichwa vya habari hivi sasa akitolea mfano wa nchi kama
Uganda ambayo baadhi ya mitaa yake imepewa majina ya wachezaji maarufu.
Aidha mheshimiwa Mtaka
ambaye pia ni rais wa chama cha riadha nchini amesema kumekuwa na tofauti kubwa
ya kimaisha kati ya wanariadha waliopata mafanikio kimichezo miaka ya nyuma na
wachezaji wa soka waliowahi kutamba miaka hiyo kutokana na mfumo wa uongozi wa
michezo uliopo.
RC Mtaka amesema
kutokana na hali hiyo wachezaji wengi wa soka wamejikuta wakiwa taabani kimaisha
mara baada ya kustaafu kucheza soka hali ambayo amesema tiba yake itapatikana
endapo viongozi na wadau wa soka wataamua kubadili mitazamo yao na kuingia
katika medani za soka la kibiashara kama ilivyo kwa nchi nyingi zilizoendelea.
Kwa upande wake kocha
mkuu wa Coastal Union Juma Mgunda amekiri kuwepo kwa dosari za kiuongozi katika
usimamizi wa mipango ya soka nchini na kuahidi kuufanyia kazi ushauri wake pale
ambapo umeigusa timu yake.
“ Mheshimiwa mkuu wa
mkoa timu yetu ni timu kongwe na imepitia vipindi vingi vya mpito, lakini kama
ulivyojionea kwa sasa hali ni tofauti, tuna vijana chipukizi wenye uwezo mkubwa
wa kuleta matokeo yatakayo washangaza wengi, binafsi ninaamini tutafika mbali”,
aliongeza Mgunda.
Aidha kuhusu ushiriki
wa mchezaji wa timu hiyo ambaye pia ni mwanamuziki maarufu wa kizazi kipya Ali
Kiba, Mgunda amesema mchezaji huyo ni hazina kubwa ya timu hiyo na kwamba
hawawezi kumtumia kwenye mechi za ugenini ambazo mapato yanachukuliwa na timu
mwenyeji.
“Ali Kiba ni brand ya
Coastal Union, anapoingia uwanjani ni lazima watu wajae kutazama mechi, na sisi
kwa kutambua umuhimu wake tutamtumia kwa mechi za nyumbani tu ili pato lote
liingie mfukoni kwetu”. Alisisitiza Mgunda.
Timu ya Coastal Union
tayari imeondoka mjini Bariadi kuelekea Dar es Salaam kuendelea na michezo yake
ya ligi kuu.
|
0 comments:
Post a Comment