Mkuu wa Mkoa wa
Simiyu ambaye pia ni rais wa chama cha riadha nchini Anthony Mtaka amewaagiza
viongozi wa riadha kanda ya ziwa kuweka mpango mkakati endelevu wa kuwatambua
na kuwaandaa kikamilifu wachezaji watakaoshiriki katika mashindano mbalimbali
ndani na nje ya nchi.
Mhe Mtaka ametoa
kauli hiyo katika kikao na viongozi wa vyama vya riadha kanda ya ziwa
kilichofanyika mjini Bariadi ambapo amesema chama cha riadha kinakabiliwa na
mashindano mbalimbali ikiwemo mbio za nyika za dunia zitakazofanyika nchini
Denmark, mashindano ya Afrika yatakayofanyika nchini Morocco pamoja na
mashindano ya relay yatakayofanyika nchini Japan hivyo ni muhimu maadalizi
yakafanyika mapema ili kuwaandaa wachezaji kisaikolojia na hatimaye waweze
kurejea na ushindi.
Adha Mhe Mtaka
amesema chama hicho kimeandaa utaratibu mzuri wa kuwapata wachezaji wenye
viwango ambapo yatafanyika majaribio nchi nzima ili kuwawezesha viongozi na
makocha kubaini vipaji vipya ili wachezaji hao waweze kujumuishwa kwenye timu
ya Taifa.
“ Naomba niwahakikishia
hatuwezi kupata wachezaji wazuri kama tutakaa tunalalamika, nendeni mkafanye
majaribio katika ngazi za mikoa yenu, chagueni wachezaji wazuri ambao tutakuwa
na uhakika watarejea na ushindi”.
“ Binafsi
ninawaahidi nitawapa msaada wowote mnaohitaji, sote tunafahamu kanda ya ziwa
kuna wachezaji wazuri sana, kinachohitajika ni kuweka mfumo mzuri wa kuwatambua
na ndio maana tumeamua safari hii tutakuwa na makocha watano kwenye kambi zetu
za taifa ambazo tunatarajia kuziweka katika mikoa ya Arusha na Pwani, mimi
ninaamini tukidhamiria kuleta mabadiliko katika mchezo huu tunaweza ”,
alisisitiza Mtaka.
Kwa upande wao
wajumbe wa kikao hicho akiwemo mwanariadha
mkongwe ambaye ni mchezaji wa kwanza kushiriki katika michezo ya Olympic
mwaka 1964, Mzee Thomas Daniel walimweleza rais wa chama hicho kuwa ukosefu wa
viwanja vyenye ubora, kutokuwepo kozi ya makocha wa ngazi ya juu, uhaba wa
vifaa pamoja na kozi maalumu kwa ajili ya makocha ni miongoni mwa changamoto
zinazohitaji kupatiwa majawabu ili kuongeza hamasa katika mchezo huo.
Kikao hicho cha siku
moja kilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa vyama vya riadha kanda ya ziwa
kutoka mikoa ya Simiyu, Mwanza, Mara na Geita.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu na rais wa chama cha riadha
nchini Anthony Mtaka akiwakaribisha wajumbe wa kikao cha kuweka mikakati ya
kuboresha riadha ofisini kwake mjini Bariadi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu ambaye pia ni rais wa chama
cha riadha nchini Anthony Mtaka akiwa kwenye kikao na viongozi wa vyama vya
riadha kanda ya ziwa mjini Bariadi.
Baadhi ya viongozi wa riadha kutoka mikoa ya Simiyu,
Mara, Mwanza na Geita wakiwa katika kikao na rais wa chama hicho mjini Bariadi.
0 comments:
Post a Comment