Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa
Simiyu umepanga kutumia kiasi cha shilingi bilioni 11.4 katika bajeti ya mwaka
wa fedha 2020/2021 kwa ajili ya matengenezo ya barabara na madaraja.
Hayo yamebainishwa na Meneja wa TANROADS mkoa wa
Simiyu, Mhandisi. Albert Kent wakati akiwasilisha taarifa katika kikao cha Bodi
ya Barabara ya Mkoa wa Simiyu, kilichofanyika jana Desemba 15, 2020 Mjini
Bariadi.
“Bajeti iliyopangwa kwa mkoa wa Simiyu ni shilingi
bilioni 11.44 na kuna ongezeko kidogo mwaka jana tulikuwa na bilioni 10.9; tumepanga
kufanya kazi kwenye barabara zenye urefu wa kilomita 923.6 pamoja na madaraja
mawili,” alisema Mhandisi Kent.
Kwa upande wake Mratibu wa Wakala wa Barabara
Vijijini na Mijini (TARURA), Dkt. Eng. Philemon Msomba amesema katika mwaka wa
fedha 2019/2020 TARURA imetengeza kilometa 690.31 za barabara huku bajeti ya
mkoa ikiwa bilioni 5. 056 na katika mwaka wa fedha 2020/2021 TARURA imeingia
mikataba 18 yenye jumla ya shilingi 3,048,528,759/=
Dkt. Msomba ameongeza kuwa jumla ya kiasi cha shilingi milioni 750
kimeidhinishwa kwa ajili ya ujenzi wa madaraja mawili ya Mwadobana na Ngashanda
kwa mwaka wa fedha 2020/2021
Mbunge wa Jimbo la Meatu, Mhe. Leah Komanya
akichangia hoja katika kikao cha Bodi ya Barabara ya Mkoa amesema “Ninaiomba Serikali
katika bajeti zijazo ipandishe hadhi kipande cha barabara ya Mwabuzo-Igunga,
ili tuweze kuleta maana ya kuunganisha barabara hii katika kuinua uchumi wa wananchi
wa wilaya ya Meatu.”
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesisitiza
usimamizi wa miradi ya barabara huku akiitaka TANROADS kuona uwezekano wa
kutenga bajeti kwa ajili ya ujenzi wa
mzani wa kisasa katika eneo la Malampaka kwa kuwa ni eneo litakalopitiwa na
reli ya kisasa (SGR).
TANROADS Mkoa wa Simiyu ina jukumu la kutunza na
kuendeleza barabara zenye urefu wa kilometa 923.65 barabara kuu ikiwa ni
kilometa 334.33, barabara za mkoa kilometa 521.62 na barabara moja ya wilaya yenye
urefu wa kilometa 67.7; ambapo TARURA inahudumia mtandao wa barabara wenye
jumla ya kilometa 4,038.16.
MWISHO
Meneja
wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Simiyu, Mhandisi. Albert Kent
akiwasilisha taarifa ya wakala huo katika kikao cha Bodi ya Barabara ya Mkoa,
kilichofanyika jana Desemba 15, 2020 mjini Bariadi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,
Mhe. Anthony Mtaka (kulia) na Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bibi. Miriam
Mmbaga wakifuatilia hoja zilizokuwa zikiwasilishwa na wajumbe wa kikao cha Bodi
ya Barabara ya Mkoa kilichofanyika jana Desemba 15, 2020 Mjini Bariadi.
0 comments:
Post a Comment