Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda na Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. Festo
Dugange wameshiriki kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Simiyu (RCC), ambapo
walitumia fursa hiyo kuwasilisha masuala ya kilimo na afya kwa viongozi wa
chama na serikali, wakuu wa Taasisi za Umma na binafsi, viongozi wa Dini na
wadau wengine wa maendeleo.
Akizungumzia
kuhusu kilimo cha zao la pamba katika kikao hicho kilichofanyika Desemba 15,
2020 Mjini Bariadi Prof. Adolf Mkenda amesema Wizara ya kilimo itafanya mapitio
ya mifumo mbalimbali ya kitaasisi ili kuongeza
tija katika uzalishaji wa pamba kufikia
lengo la kuzalisha tani milioni moja ndani ya miaka mitano ijayo.
Miongoni
mwa mifumo aliyoibainisha Profesa Mkenda ni pamoja na mfumo wa kushughulikia
pembejeo za kilimo huku akibainisha kuwa Wizara yake inaendelea kufanya uchunguzi ili kuona kama uwezekano
wa kuzalisha viuatilifu nchini ili
kupunguza uagizaji wa viuatilifu kutoka nje ya nchi na kuweza kudhibiti ubora
wa viuatilifu hivyo.
“
Katika kufikia tija kwenye zao la pamba pia tunapitia upya na kwa haraka sana
mfumo mzima wa kitaasisi wa kuzalisha na kugawa mbegu za pamba, utaratibu mpya
hautakuwa umekamilika kwa kipindi hiki cha msimu huu, lakini tumekusudia na
tumekubaliana tutafanya mapitio ili wakulima wapate mbegu bora kwa wakati,” alisema
Profesa Mkenda.
Awali
Kabla ya kuzungumza katika kikao hicho
Prof. Mkenda, wajumbe wa Kikao cha RCC waliwasilisha changamoto mbalimbali
katika kilimo cha pamba ikiwa ni pamoja na tatizo la upungufu wa mbegu na mbegu
kutowafikia wananchi kwa wakati.
“Kumekuwa
na changamoto ya upungufu wa mbegu kwa wakulima, ninashauri ili mbegu ziwafikie
wakulima wote na kwa wakati, makampuni yanayozalisha mbegu yazipeleke kwa
Mkurugenzi ambaye ndiye mwenye wataalam wa kilimo wanaofahamu idadi ya wakulima
na ukubwa wa maeneo wanayolima,” alisema Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Benson
Kilangi.
“Pamoja
na kutatua changamoto ya pamba, tunaomba serikali iajiri maafisa ugani ili wananchi waweze kupata huduma za ugani na
kuzalisha kwa tija,tutakapozalisha kwa tija tutapata mavuno mengi na mkulima atanufaika
pamba yake, suluhisho la bei ya pamba ni kujenga kiwanda cha nguo mkoani
Simiyu,” Mhe. Esther Midimu Mbunge Viti Maalum.
Kwa
upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. Festo Dugange
ametoa rai kwa Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya ya Busega, Bariadi na
Itilima kuanza kununua vifaa tiba kwenye Hospitali za Wilaya zilizojengwa kwa
kutumia mapato ya ndani huku akibainisha
kuwa Serikali imetenga shilingi milioni 500 kwa kila hospitali kwa ajili ya
ununuzi wa vifaa tiba.
Dkt. Dugange pia amesema
katika miaka mitano ijayo Serikali ina mpango wa kujenga vituo vya kutolea
huduma za afya takribani 655 huku akifafanua kuwa itaanza na ukamilishaji wa
maboma yaliyojengwa na kwa nguvu za wananchi na kuomba Halmashauri kuweka
mpango wa kuanza kukamilisha maboma hayo.
Dkt.Dugange amesisitiza juu
ya umuhimu wa kuimarisha usimamizi wa mifumo ya ukusanyaji mapato katika vituo vya kutolea huduma za afya,
ambapo amebainisha kuwa makusanyo yakiwa mazuri yatazipunguzia Halmashauri
mzigo wa utegemezi kwa Serikali Kuu na wadau mbalimbali wa afya na kuwezesha
vituo hivyo kujiendesha ikiwa ni pamoja na kuwa na uwezo wa kununua dawa.
Akifunga kikao cha RRC Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony
Mtaka amewashukuru viongozi hao kushiriki katika kikao hicho, huku akitoa wito
kwa viongozi wote wa Mkoa huo kuifanya elimu kuwa ajenda ya kudumu ya mkoa na
ujenzi wa vyumba vya madarasa kuwa ni kipaumbele chao cha kwanza ili kila
mwanafunzi aliyefaulu aweze kwenda shule.
MWISHO.
Waziri wa kilimo, Mhe. Profesa. Adolf Mkenda
akizungumza na viongozi wa Chama na Serikali, wakuuwa Taasisi za Umma na
binafsi, viongozi wa Dini na wadau wengine wa maendeleo katika kikao cha Kamati
ya Ushauri ya Mkoa wa Simiyu(RCC), kilichofanyika jana Desemba 15, 2020 Mjini
Bariadi.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, Dkt. Festo
Dugange akizungumza na viongozi wa Chama na Serikali, wakuu wa Taasisi za Umma
na binafsi, viongozi wa Dini na wadau wengine wa maendeleo katika kikao cha
Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Simiyu (RCC), kilichofanyika jana Desemba 15, 2020
Mjini Bariadi.
Baadhi ya wajumbe wa kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Simiyu (RCC), wakifuatilia kikao hicho kilichofanyika jana Desemba 15, 2020 Mjini Bariadi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akifunga kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Simiyu(RCC), kilichofanyika jana Desemba 15, 2020 Mjini Bariadi.Kutoka kushoto Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony
Mtaka, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Mhe. Enock Yakobo na Mjumbe wa
Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) mkoa wa Simiyu, Mhe. Gungu Silanga wakiteta
jambo katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Simiyu (RCC),
kilichofanyika jana Desemba 15, 2020 Mjini Bariadi.
Mkuu wa Wilaya ya Busega Mhe. Tano Mwera akichangia hoja katika kikao
cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Simiyu (RCC), kilichofanyika jana Desemba 15,
2020 Mjini Bariadi.
0 comments:
Post a Comment